1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika katika magezeti ya Ujerumani

Abdu Said Mtullya22 Machi 2013

Pamoja na masuala mengine magazeti ya Ujerumani wiki hii yamechapisha taarifa juu ya aliekuwa kiongozi wa waasi wa M23 Bosco Ntaganda ambae hapo awali alijisalimisha kwenye ubalozi wa Marekani nchini Rwanda,

https://p.dw.com/p/182pS
Bosco Ntaganda aliekuwa kiongozi wa waasi
Bosco Ntaganda aliekuwa kiongozi wa waasiPicha: Reuters

Juu ya kiongozi wa waasi, Bosco Ntaganda gazeti la "Frankfurter Allgemeine"linasema mbabe huyo wa kivita anakabiliwa na madai yaliyotolewa na Mahakama Kuu ya Kimataifa ya mjini The Hague juu ya uhalifu wa kivita ikiwa pamoja na kuwatumia watoto kama askari,ubakaji na mauaji halaiki.

Gazeti la "die tageszeitung" linasema ikiwa Ntaganda kweli atafikishwa mbele ya Mahakama ya Kimataifa ya mjini The Hague atakuwa na mengi ya kuyafichua.

Matumaini ya Wakristo barani Afrika:

Gazeti la "Süddeutsche" linasema katika makala yake kwamba Wakristo barani Afrika wana matumaini makubwa juu ya Kiongozi mpya wa Kanisa Katoliki duniani Baba Mtakatifu Francis wa kwanza.

Gazeti hilo linasema ni maoni ya watu wengi barani Afrika kwamba kuchaguliwa kwa Baba Mtakatifu ambae hatoki barani Ulaya kunatoa ishara kwamba Kanisa Katoliki sasa litakuwa wazi zaidi kwa waumini wote.Gazeti la " Süddeutsche" limemnukuu mfanyabiashara wa magari,Joseph Mainagachemi kutoka Kenya akisema kwamba watu barani Afrika walikuwa na matumaini ya kumwona Mwafrika akichaguliwa kuwa Papa mpya

Pope Francis delivers his message during an audience with the diplomatic corps at the Vatican March 22, 2013. Pope Francis urged the West on Friday to intensify dialogue with Islam and appealed to the world to do more to combat poverty and protect the environment. REUTERS/Tony Gentile (VATICAN - Tags: RELIGION POLITICS)
Papa Francis wa kwanzaPicha: Reuters

.Hata hivyo Mainagachemi ameliambia gazeti la "Süddeutsche" kuwa yeye pia amefurahi kwamba Papa Francis wa kwanza kutoka Amerika ya kusini amechaguliwa kwa sababu hiyo ilikuwa kudura ya Mungu.

Idadi kubwa ya Wakatoliki barani Afrika:

Gazeti la "Süddeutsche" limetilia maanani kwamba hakuna kwingineko duniani ambako idadi ya waumini wa Kanisa Katoliki inaongezeka kwa kasi kama barani Afrika.Gazeti hilo linaeleza kuwa hali hiyo inatokana na mchango unaotolewa na Kanisa Katoliki katika masuala ya kijamii. Pale ambako wajibu wa serikali hauonekani, ndipo Kanisa Katoliki linapoziba pengo,kwa mfano kwa kujenga shule,hospitali na nyumba za yatima. Mfano mkubwa ni katika Jumhuri ya Kidemokrasi ya Kongo.

Mgogoro wa Mali:

Wafaransa wakutana na wafaransa ana kwa ana nchini Mali.

Gazeti la "die tageszeitung" linasema hayo katika taarifa yake juu ya mgogoro wa Mali uliosababishwa na hatua ya wanajeshi kutwaa mamlaka mwaka mmoja uliopita. Gazeti hilo limeeleza kwamba majeshi ya Ufaransa yaliingilia kati nchini Mali baada ya waasi kuiteka sehemu ya kaskazini ya nchi hiyo. Lakini walipoingia katika ngome za waasi kaskazini mwa Mali, wanajeshi hao wa Ufaransa walipambana na baadhi ya waasi waliokuwa na pasipoti za Ufaransa.

Msaada wa Ujerumani kwa majeshi ya Mali:

Gazeti la"Frankfurter Allgemeine" limearifu kwamba msaada wa kijeshi wa Ujerumani kwa majeshi ya Mali utakuwa wa muda mrefu.Gazeti hilo limemnkuu Waziri wa ulinzi wa Ujerumani Thomas de Maizere akiyasema hayo.Gazeti hilo limeeleza kuwa jeshi la Ujerumani litashughulikia usafirishaji na ugavi pamoja na mafunzo kwa ajili ya wanajeshi wa Mali.Na kwa ajili hiyo askari wa Ujerumani 330 watawekwa nchini Mali na katika nchi jirani.

Gazeti la"Frankfurter Allgemeine" limemnukuu Waziri de Maizere aliefanya ziara nchini Mali akisema kwamba inapasa kusubiri na kuona jinsi hali inavyoendelea nchini Mali.Hapo awali Bunge la Ujerumani lilipanga ushriki wa majeshi ya Ujerumani uwe hadi mwanzoni mwa mwaka ujao.

Gazeti hilo pia limeripoti juu ya ziara ya Waziri wa ulinzi wa Ujerumani nchini Senegal.Alikitembelea kikosi cha anga kinachoshirikiana na cha Ubelgiji katika shughuli za usafirishaji ili kuyaunga mkono majeshi ya Ufaransa na nchi za Afrika nchini Mali.


Mwandishi:Mtullya abdu/Deutsche Zeitungen/
Mhariri:Yusuf Saumu