1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini 7.5% nyongeza-mishahara

31 Agosti 2010

Je, wafanyikazi wataridhia ?

https://p.dw.com/p/P07h
Wanachama wa chama cha walimu waandamana.Picha: AP

Watumishi wa serikali wapatao milioni 1.3 nchini Afrika kusini, wanapiga kura kuamua kukubali au kukataa nyongeza ya mishahara ya 7.5% iliopendekezwa na serikali.Serikali ya rais Jacob Zuma , imeongeza kima chake kutoka 7 % hadi 7.5%.

Serikali ya Afrika Kusini imeongeza kima cha mishahara cha 7.5% na kuzidisha malipo ya ruzuku za nyumba za kila mwezi hadi Rand 800 kutoka Rand 700.Vyama vya wafanyikazi nchini,vikidai nyongeza ya mishahara ya 8.6% na Rand 1000 ruzuku za nyumba.

Kujitolea sasa kwa serikali kumekuja wakati wa mazungumzo yalioandaliwa baada ya Rais Jacob Zuma kuwaamuru mawaziri wake kupatana haraka na vyama vya wafanyikazi ili kuukomesha mgomo wa kiasi ya wik 3 sasa ambao umeongoza kufungwa mashule, umezuwia matibabu hospitali na umedhuru shauku ya watiaji-raslimali nchini.

Duru iliopo karibu na vyama vya wafanyikazi, inasema yabainika vitakubaliana na nyongeza hii mpya ya serikali na hivyo, kumaliza mgomo wao.Hadi sasa , serikali ikisema haimudu kuongeza mishahara kupindukia kima kikubwa mara 2 ya kile cha ughali wa maisha.

Msemaji wa Rais Zuma, amearifu kwamba, rais Zuma ameingiwa mno na wasi wasi juu ya athari za mgomo huu wa wiki 3 sasa juu ya huduma za afya na elimu.

"Maoni ya Rais ni kuwa, mgomo huu ukome haraka iwezekanavyo mnamo siku 2 zijazo,"-alisema Zizi Kodwa.

Mgomo wa sasa ni mkubwa kabisa kuwahi kuikumba Afrika kusini tangu 2007 kutokana na siku zilizopotea kufanya kazi,lakini hakujaathiri bado masoko ya fedha nchini hatahivyo, wadau wa soko hilo wanasema kuwa, mgomo huu utaathiri faida za rand-sarafu ya Afrika Kusini na utaweza kuzusha athari mbaya zaidi endapo ukiendelea.

Mgomo huu umechafua zaidi usuhuba kati ya chama-tawala cha rais Zuma (ANC) na Shirikisho kubwa kabisa la wafanyikazi nchini (COSATU)-ambalo lilichangia kumleta madarakani Rais Zuma, lakini likavunjwa moyo nae kwa kutofuata sera za mrengo wa shoto na kuwahurumia wanyonge.

Afrika Kusini -dola kubwa la kiuchumi barani Afrika,imekumbwa na milolongo ya migomo tangu katika makampuni ya kibinafsi hata serikalini mnamo miezi michache iliopita na hii ikabidi kuongoza kufikiwa mapatano yanayopindukia viwango vya mfumuko wa bei.

Shirikisho la wafanyi-kazi la COSATU lilitishia kupanua mgomo huu wiki hii kujumuisha vyama vyote vya wafanyikazi viliopo chini ya paa lake na hivyo, kuhatarisha kuulemaza uchumi wa Afrika Kusini.

Maafikiano yoyote ya kuukomesha mwishoe, mgomo huu yataongeza mno matumizi ya serikali kwa kiasi cha 1-2% na hivyo, kuilazimisha serikali kusaka fedha wakati ikijitahidi kubana matumizi yenye nakisi ya 6.7% ya pato zima la taifa.

Mwandishi: Ramadhan Ali/ RTRE

Uhariri: Othman Miraji