1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini kujiondoa kutoka mahakama ya ICC

Caro Robi
21 Oktoba 2016

Afrika Kusini imeiandikia Umoja wa Mataifa kuwa inajiondoa kutoka uanachama wa mkataba wa Roma unaounda mahakama ya kimataifa inayoshughulikia kesi za uhalifu wa kivita ya ICC.

https://p.dw.com/p/2RVg2
Internationaler Strafgerichtshof in Den Haag Niederlande
Picha: picture-alliance/dpa/J.Vrijdag

Kulingana na nyaraka zilizoonekana na shirika la habari la Reuters, na pia kuchapishwa na gazeti la Mavericks, hatua hiyo itachukua mwaka mmoja kutekelezwa baada ya ombi la Afrika Kusini kujiondoa ICC kupokelewa na Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon.

Msemaji wa Umoja huo amekataa kuthibitisha iwapo wamepokea ombi rasmi lililotiwa saini mnamo tarehe 19 Oktoba na waziri wa mahusiano ya kimataifa na ushirikiano wa Afrika Kusini Maite Nkoana Mashabane.

Clayson Moinyela, Msemaji wa wizara ya mambo ya nje wa Afrika Kusini  pia amekataa kuzungumzia suala hilo akisema waziri wa sheria atafanya mkutano na waandishi habari leo.

Hatua hiyo inakuja siku chache baada ya Rais wa Burundi Pierre Nkurunziza, kutia saini sheria ya kutaka kujiondoa rasmi kutoka mkataba wa Roma baada ya bunge kupiga kura wiki iliyopita kuidhinisha nchi hiyo kujiondoa ICC. Burundi ndiyo itakuwa nchi ya kwanza kujiondoa kutoka mkataba wa Roma ulioanzishwa mwaka 1998.

Mahakama hiyo inayoshughulia kesi za mauaji ya halaiki, uhalifu dhidi ya kibinadamu na uhalifu wa kivita ilianza shughuli zake mwaka 2002 na ina wanachama 124.

Südafrika Kapstadt Jacob Zuma Präsident Anhörung Parlament
Rais wa Afrika Kusini Jacob ZumaPicha: picture-alliance/dpa/N. Bothma

Afrika Kusini ilisema mwaka jana ilitangaza itajiondoa ICC baada ya kushutumiwa vikali kwa kukosa kumkamata Rais wa Sudan Omar al Bashir aliopizuru nchi hiyo kuhudhuria mkutano wa kilele wa Umoja wa Afrika.

Al Bashir anatafutwa  na mahakama hiyo ya ICC kujibu mashitaka ya mauaji ya halaiki na uhalifu wa kivita katika jimbo la Darfur. Nchi kadhaa za Afrika zimeishutumu mahakama hiyo yenye makao yake The Hague, Uholanzi kwa kuwaandama viongozi wa Afrika ikilinganishwa na viongozi kutoka maeneo mengine duniani.

Waraka kwa Umoja wa Mataifa kutoka Afrika Kusini unasema serikali ya nchi hiyo imejitolea kupambana na kutojali sheria na kuwachukulia hatua za kisheria wale waliohusika na uhalifu wa kimataifa na madhila mengineyo.

Afrika Kusini imeendelea kusema kama mwanachama muasisi wa Umoja wa Afrika inadumisha haki za binadamu na njia za amani za kutatua mizozo barani Afrika na kwamba nchi hiyo imeng'amua kutekeleza wajibu wake kuhusuiana na maazimio ya amani ya kutatua mizozo nyakati nyingine haziendani na tafsiri inayotolewa na mahakama ya ICC.

Mwandishi: Caro Robi/Reuters/ap

Mhariri:Gakuba Daniel