1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini yaaga kombe la Dunia kwa heshima.

22 Juni 2010

Afrika Kusini yailaza Ufaransa 2-1.Je, Ujerumani na Ghana kesho vipi ?

https://p.dw.com/p/O0HM
Bafana Bafana kwaheri 2010.Picha: AP

Baada ya wenyeji Afrika kusini, jana kuaga Kombe la Dunia kwa heshima duru ya kwanza kufuatia ushindi wao wa mabao 2:1 dhidi ya Ufaransa, leo ni zamu ya Black Stars -Ghana kufuta aibu ya bara la Afrika, ikiwa itailaza Ujerumani. Lakini si hatima ya Ghana tu itakayoamuliwa leo,bali hata ile ya Ujerumani.Ujerumani lazima iishinde Ghana ama si hivyo, itakuwa ni mara ya kwanza inaaga Kombe la Dunia duru ya kwanza katika historia yake .

Kocha Joachim Löw,amtegemea leo mjerumani wa asili ya Brazil,Cacau kuvunja tumbuu ya lango la Black Stars.Baada ya kutimuliwa nje ya uwanja na refu kwa kadi nyekundu kwa mshambulizi wake Miroslav Klose, kocha Löw ameamua kuanza na Cacu pamoja na Lukas Podolski,alieizamisha jahazi ya Ujerumani,alipokosa kutia bao la mkwaju wa penalty katika lango la Serbia.

Ghana,ilifanya uzembe kumaliza udhia na mapema ilipocheza na Australia Jumamosi iliopita.Ilikua na nafasi ya kuishinda Australia iliocheza na wachezaji 10 na kuondoka na pointi 6 ambazo zingeinusuru hii leo ikishindwa na Ujerumani.

Badala ya kushambulia na kushinda ,Ghana, iliridhika na sare na Australia iliocheza na wachezaji 10 tu.Hii yasemekana, ilimkasirisha stadi wa Ghana wa Inter Milan, Sulley Muntar.Alikorofishana na kocha wake na nusra akumbwe na hatima ya Anelka wa Ufaransa,kwa madhambi kama hayo-ya kutimuliwa nje ya kikosi . Baadae,Muntari, alitaka radhi.Na leo,Muntari,atazamiwa kuiokoa Ghana,tumaini la mwisho la bara la Afrika.Kwani, ni nyota ya Black Stars na ya bafana bafana zilizon'gara hadi sasa katika mawingu ya Kombe la dunia, miongoni mwa timu 6 za bara la Afrika.

Halafu kuna mvutano kati ya Ujerumani na Ghana ulioanzia muda mfupi kabla kuanza kombe la dunia:Nahodha wa Ujerumani,Michael Ballack aliekua aiongoze Ujerumani kwenye Kombe hili la Dunia, alikanyagwa na Kevin-Prince Boateng na kuumizwa asicheze Kombe la dunia. Ingawa nafasi yake ballack imechukuliwa na Philipp Lahm,mpambano huu haukuepuka madhambi aliofanya Kevin-prince Boteng kwa Ballack.

Endapo Ghana, ikithubutu kumchezesha Kevin leo, mkasa mzima huenda ukahanikiza alao katika vyombo vya habari vya Ujerumani.Nahodha wa zamani wa Ghana ,mzaliwa wa Ujerumani ,Anthony bafoe,asema Ghana leo ndilo tumaini la mwisho la Afrika na nani angebisha hayo.

Lakini, Ghana, yaweza kuvumilia "blitz-Krieg" hujuma kali za wajerumani kutoka kila upande hii leo ?Au watajenga ngome kama ya wakorea ya kaskazini walipocheza na Brazil ?

Mkakati gani,Ghana,itatumia kuzima hujuma za Ujerumani leo,ni vigumu kuagua. Wazi,lakini wajerumani hawataridhika na chochote leo kasoro ya ushindi. kwani, haimo katika kitabu chao cha histria ya dimba la kombe la dunia, kufunga virago na kurudi nyumbani duru ya kwanza.Ghana, inajua hayo.

Mwandishi: Ramadhan Ali /AFPE

Mhariri:Abdul-Rahman