1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini yakabiliwa na tatizo la wakimzi kutoka Zimbabwe

Josephat Charo9 Agosti 2007

Afrika Kusini inakabiliwa na tatizo kubwa la uhamiaji. Inakadiriwa Wamzimbabwe milioni mbili wamekimbilia Afrika Kusini, wengi wao bila vibali. Wanaishi kinyume cha sheria kwa kuwa watu 20 kati ya watu 5,000 wanaowasilisha maombi ya uhamiaji hufaulu kupata vibali vya kuishi.

https://p.dw.com/p/CB23

Kila siku polisi wa Afrika Kusini huwakamata Wazimbabwe wengi wanaoishi bila vibali na kuwapeleka kwenye kambi ya wahamiaji haramu ya Lindela. Mara moja kila wiki Wazimbabwe takriban 1,000 husafirishwa kwa njia ya treni hadi mpakani, lakini muda mfupi baadaye hurejea tena nchini Afrika Kusini.

Wazimbabwe wanaokwepa kukamatwa, wanaishi kwenye miji mikubwa kama vile Johannesburg bila vibali na katika hali ngumu za kimaisha. Huishi watu 20 katika chumba kimoja na huwa tayari kuhamia mahala pengine. Wote wanaojaribu kutafuta vibali vya kuwawezesha kuishi kihalali nchini Afrika Kusini hukabiliwa na maafisa ambao hawako tayari kuwasaidia na sheria ngumu.

Foleni ya Wazimbawe wanaotafuta uhamiaji huwa ndefu mno mjini Johannesburg. Maafisa wanalazimika kufanya kazi ya ziada ya kutoa visa, pasi za kusafiria na kuyashughulikia maombi ya uhamiaji.

Mwanamume huyu anaeleza kwa nini alilazimika kukimbia Zimbabwe. ´Ilikuwa wakati wa usiku, watu wakaja wakaanza kupekua kila kitu nyumbani mwangu. Wakatupa nguo zangu nje, wakanitesa, wakanipiga, baadaye nikalazimika kukimbia usiku huo huo.´

Kijana huyu naye anaeleza kwa nini alikimbilia Afrika Kusini. ´Nilikimbia shule kwa hiyo nilitarajiwa kujiunga na kambi ya vijana ya waasi. Sikutaka, hivyo nikaona maisha yangu yamo hatarini. Unapokataa kujiunga na kambi hizo huwa ni kama tayari umekufa.´

Wazimbabwe wote wanaosimama kwenye foleni ndefu siku nzima na kila wiki, walikabiliwa na kipigo, kufuatwa na kuteswa pamoja na jamaa wa familia zao. Sababu pekee ni kuwa wanaunga mkono chama kikuu cha upinzani cha Movement for Democratic Change, MDC.

Mwanamume huyu kutoka Zimbabwe amekimbilia Afrika Kusini. ´Ukweli ni kwamba mimi nilikuwa mkurugenzi wa ujasusi wa chama cha upinzani cha MDC nchini Zimbabwe. Nilikamatwa na kuteswa Koromonzi kwa siku nne. Kufikia sasa watu wote waliokamatwa kuhusiana na kesi hiyo nadhani sote tuko hapa, isipokuwa kansela mmoja aliyesalia Zimbabwe. Tuko hapa kwa sababu hatuwezi kukabiliana na moto unaowaka huko.´

Maisha sio mazuri kwa Wazimbabwe nchini Afrika Kusini. Wengi wao walivuka mpaka wakiwa hawana chochote mbali na nguo walizokuwa wamevaa. Wiki kadhaa zilizopita Wazimbabwe takriban 15 walikufa maji wakati walipokuwa wakijaribu kuingia Afrika Kusini kwa kuogelea kwenye mto wa Limpopo unaosemekana kuwa na mamba wengi.

Takriban Wazimbabwe milioni tatu kati ya Wazimbabwe milioni 12 wanaishi uhamishoni. Mashirika ya kutetea haki za binadamu wanakadiria Wazimbabwe milioni mbili wanaishi nchini Afrika Kusini. Mama huyu anaeleza kilio chake.

´Ni jambo la kushangaza sana kwa sababu mtu unatokea nchi ambako utawala wa sheria hauna thamani tena, halafu unakuja unakutana na mambo kama haya. Kusema kweli nilikuwa na matarajio tofauti.´

Naye kijana huyu anawalaumu maafisa wa Afrika Kusini kwa ufisadi. ´Tulivyotendewa hapa si vizuri kwa kweli. Hali ilikuwa mbaya zaidi kuliko nchini Zimbabwe. Kuna ufisadi mwingi sana hapa na wanataka kiinua mgongo. Wanaabudu pesa na ufisadi.´

Wakili Kaajul Ramajathan anayeshughulikia haki za binadamu amethibitisha ufisadi miongoni mwa maafisa wa Afrika Kusini. Amesema tatizo kubwa ni kwamba wakimbizi wote wa Zimbabwe wanakabiliwa na kitisho cha kukamatwa na polisi na anailaumu serikali ya Afrika Kusini kwa kutofanya lolote. Ulaji rushwa imekuwa kazi nyengine ya pembeni.

´Unapompa mtu kibali na kumwambia unaweza sasa kuishi kihalali kwa miaka miwili ijayo, unaua uchumi kwa sababu hamna faida yoyote ya kifedha inayopatikana. ´Sote tunajua kwamba raia kukosa uwezo ni sehemu ya tatizo zima, lakini pia hakuna ari ya kisiasa.´

Barry Gilder kiongozi wa jumuiya ya wahamiaji analumu ukosefu wa sera. ´Hakuna sera dhidi ya Wazimbabwe wanaotaka kuwa wahamiaji. Kuna sheria za uhamiaji zinazowaathiri watu wote wanaoomba uhamiaji.´

Gabriel Shumba, wakili wa haki za binadamu kutoka Zimbabwe alikimbilia Afrika Kusini baada ya kuteswa na kifaa cha umeme. Amekasirishwa sana na jinsi Afrika Kusini inavyolishughulikia tatizo la wakimbizi wa Zimbabwe. Anasema ni aibu kubwa.