1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Kusini yarejesha hatua za kuzuia kuenea kwa COVID-19

Sylvia Mwehozi
29 Desemba 2020

Afrika Kusini imerejesha hatua kali za kuzuia maambukizi ya virusi vya corona kwa kupiga marufuku mikusanyiko, marufuku ya kutotoka nje usiku na uuzaji wa pombe wakati maambukizi yakipindukia milioni moja

https://p.dw.com/p/3nIs6
Südafrika Präsident Ramaphosa
Picha: AFP

Afrika Kusini imekuwa nchi ya kwanza barani Afrika ambapo visa vya maambukizi ya corona vimepindukia milioni moja. Wizara ya Afya ilitangaza kwamba iko katikati ya wimbi la pili la maambukizi, na zaidi ya visa milioni moja vya covid-19 vimesajiliwa tangu mwezi Machi.

Katika hotuba yake kwa taifa aliyoitoa kwa njia ya televisheni Jumatatu rais wa Afrika Kusini Cyril Ramaphosa ametangaza kurejeshwa kwa hatua za kukabiliana na maambukizi zilizoanza mara moja. Hatua hizo ni pamoja na marufuku ya kutotoka nje usiku, marufuku ya uuzaji pombe, kufungwa kwa migahawa yote na zuio la mikusanyiko ya watu.

"Kuanzia sasa, ni lazima kwa kila mtu kuvaa barakoa akiwa maeneo ya umma. Mtu atakayeshindwa kufunika mdomo na pua atakuwa anatenda kosa."

Kama ilivyo kwa Uingereza Afrika Kusini inapambana na aina mpya ya kirusi cha coronaambacho wataalamu wanadai kwamba kinasambaa zaidi kuliko cha hivi sasa. Chama cha wafanyakazi wa afya cha Afrika Kusini kinachowakilisha wauguzi na madaktari, kimeonya kwamba mfumo wa afya wa taifa hilo uko karibu kuzidiwa na mchanganyiko wa idadi kubwa ya wagonjwa wa covid-19 na wagonjwa wengine wanaohitaji huduma ya dharura.

Russland Rostov-On-Don | Soldat wird geimpft | Sputnik V
Mwanajeshi wa Urusi akipatiwa chanjo ya coronaPicha: Sergey Pivovarov/REUTERS

Nchini Urusi idadi ya vifo imeripotiwa kuwa mara tatu zaidi ya hapo awali, na kulifanya taifa hilo kuwa la tatu kuwa na idadi kubwa ya vifo wakati mataifa kadha yakizindua rasmi kampeni ya chanjo ya virusi vya corona. Ubelgiji imeungana na mataifa mengine ya Ulaya katika uzinduzi wa kampeni ya chanjo. Mataifa mengi ya Ulaya yalizindua kampeni hiyo siku ya Jumapili na huku Canada, China, Singapore na Saudi Arabia nazo tayari zimezindua zoezi hilo. 

Hayo yakijiri, shirika la afya ulimwenguni WHO limeonya kwamba majanga zaidi mkubwa yanaweza kujitokeza siku za usoni na hivyo ulimwengu unapaswa kuchukulia kwa uzito suala la kujiweka tayari. Mkuu wa huduma za dharura wa WHO, Michael Ryan aliwaeleza waandishi wa habari kwamba janga la virusi vya corona limeathiri pakubwa ulimwengu lakini kunahitajika matayarisho ya kitu kikubwa kinachoweza kuwa kibaya zaidi katika siku za usoni.

Wasiwasi umeongezeka kufuatia aina mpya ya kirusi cha corona kilichogunduliwa kwa mara ya kwanza huko Uingereza na wataalamu wanaamini kwamba kinasambaa kwa kasi. Baada ya kusambaa katika nchi kadha za umoja wa ulaya, pamoja na Japan na Canada, Korea Kusini ilikuwa nchi ya hivi karibuni kuripoti aina hiyo mpya kirusi.