1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Mashariki kukabiliana na magonjwa ya mlipuko

Grace Kabogo
22 Mei 2019

Jumuiya ya Afrika Mashariki inatarajia kuendesha zoezi la mfano la kukabiliana na magongwa ya mlipuko eneo la mpaka wa Namanga unaoziunganisha nchi za Kenya na Tanzania.

https://p.dw.com/p/3ItOm
Burundi Gesundheitswesen
Picha: picture-alliance/Ton Koene

Zoezi hilo linatazamiwa kuwa na matokeo mazuri na kujenga uwezo wa kupambana na magonjwa ya mlipuko hasa kwa nchi hizo mbili. Taarifa iliyotolewa kwa vyombo vya habari inaeleza kuwa zoezi hilo litafanyika kwa siku nne kuanzia June 11 hadi 14 mwaka huu.

Zoezi hilo linalofadhiliwa  na shirika la kimataifa la maendeleo la Ujerumani GIZ, litawahusisha wadau wapatao 250 kutoka sekta mbalimbali ikiwemo wanaohusika na afya ya wanyama, afya ya binadamu, mazigira, vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini, waandishi habari, wananchi pamoja na viongozi wa kijamii. 

Wananchi watakiwa kuwa watulivu

Watu wanaovuka na kufanya shughuli zao katika mpaka wa Namanga wilaya ya Longido kaskazini mwa Tanzania, na upande wa Kajado nchini Kenya wameombwa kuwa watulivu kwa kipindi hicho cha siku nne za majaribio na kutokuwa na hofu yeyote.

Dokta Irene Lukassowitz kutoka shirika la GIZ, anasema ni gharama kubwa kuandaa zoezi hilo na kwamba maandalizi yake yalianza mwaka mmoja na nusu uliopita na kama wanajamii watapata elimu ya kutosha wanaweza kujikinga na magonjwa ya kuambukiza.

''Kama watu watakuwa na taarifa sahihi watajua ni kwa jinsi gani magonjwa ya milipuko yanaambukizwa hivyo ni rahisi kujikinga. Hicho ndicho tulichojifunza kuhusu ugonjwa wa Ebola huko Afrika Magharibi. Tunatakiwa kuunganisha nguvu na kufanya kazi pamoja ili kupambana na magonjwa haya, na ndio maana tunawaleta watu pamoja ili kukabiliana na magonjwa ya milipuko,'' alisema Dokta Lukassowits.

GIZ Logo
Nembo ya GIZPicha: picture alliance/dpa

Hii sio mara ya kwanza zoezi hili kufanyika, kwani limeshawahi kufanyika katika nchi nyingine za Afrika Mashariki kama vile Burundi na baadhi ya maeneo ya mipakani nchini Tanzania. Zoezi hili pamoja na mambo mengine litasaidia kuonesha uwezo na mapungufu ya kukabiliana na magonjwa ya mlipuko ya kuambukiza maeneo ya mipakani endapo hali hiyo itatokea.

Katika ukanda wa Afrika Mashariki kuna magonjwa mengi ya kuambukiza yanayoathiri wanyama na binadamu kama vile homa ya bonde la ufa, Ebola, kipindupindu na kichaa cha mbwa na ndio sababu jumuiya hiyo inaona upo umuhimu wa wadau mbalimbali kutoka eneo hilo kuunganisha nguvu ili kukabiliana na magonjwa hayo.

Zoezi linatokana na makubaliano ya 2015

Mbele ya waandishi habari mwakilishi wa katibu mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki Dokta Michael Katende amesema zoezi hilo linafuatia makubaliano ya mawaziri wa afya wa nchi wananchama za Jumuiya ya AfriKa Mashariki yaliyofikiwa mwaka 2015 ya kupambana na magonjwa ya milipiko maeneo ya mipakani Dr. Katende ameongeza kuwa.

''Tumesikia kuhusu Ebola huko Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo, wananchi wa Afrika Mashariki pia wanasafiri kwenda Kongo na Wakongo wanakuja huku kwa sababu tuna mipaka ya pamoja. Jumuiya ya Afrika Mashariki ipo kwenye hatari ya kuambukizwa. Ndio mawaziri wetu wakaona ni vizuri kuchunguza ujuzi tulionao wa kukabiliana na magonjwa ya mlipuko endapo yatatokea'', alifafanua Dokta Katende.

Magonjwa hayo ya milipuko yanatajwa kuzikumba nchi nyingi hasa zilizo kusini mwa jangwa la Sahara, na kuwaua maelfu ya watu, kuathiri mifugo, makaazi pamoja na uchumi.