1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika Mashariki kukumbwa na uvamizi mwingine wa nzige

Iddi Ssessanga
19 Februari 2020

Wataalamu wa mazingira wameonya kuwa Afrika Mashariki huenda ikakumbwa na uvamizi wa pili wa nzige wa jangwani katika muda wa wiki chache. Wadudu hao hivi sasa wanataga mayai kwenye njia yao ya uhamaji.

https://p.dw.com/p/3XzMi
Kenia Heuschreckenplage
Picha: picture-alliance/AP Photo/B. Curtis

Kituo cha Utabiri wa Mabadiliko ya Tabianchi na Utekelezaji (ICPAC) kimesema katika taarifa kuwa wadudu hao hivi sasa wanataga mayai kwenye njia yao ya uhamaji kupitia mataifa kadhaa ya Afrika Mashariki, ambayo huenda yakatotoa kati ya mwezi Machi na Aprili na kusababisha kitisho kikubwa kwa msimu ujao wa upandaji mazao na usalama wa chakula. ICPAC iko chini ya Jumuiya ya Maendelea ya Serikali za Mataifa ya Pembe ya Afrika IGAD.

Onyo hilo limekuja baada ya makundi ya mamilioni ya nzige wa jangwani kuivamia Afrika Mashariki katika wiki za hivi karibuni, na kuharibu  mazao na malisho katika eneo ambako tayari kuna uhaba wa chakula kutokana na ukame na mizozo, kulingana na wataalamu. Huku msimu muhimu zaidi wa upandaji na mavuno Afrika Mashariki ukikaribia kuanza kati ya Machi na Mei, uvamizi wa pili wa nzige huenda ukasababisha madhara makubwa kwa mujibu wa ICPAC.

Ein äthiopischer Bauer versucht, Wüstenheuschrecken abzuwehren, die in seiner Khat-Farm am Rande von Jijiga in der Somali-Region fliegen
Mkulima wa Ethiopia akijaribu kuwafukuza nzige waliovamia shamba lake pembezoni mwa Jijiga katika jimbo la Somali, Ethiopia.Picha: Reuters/G. Paravicini

Sudan Kusini yaomba msaada wa kimataifa

Maafisa wamebainisha kuwa mripuko huo, ambao ndiyo mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 25, umeziathiri Ethiopia, Somalia, Kenya, Djibouti, Eritrea, Sudan na hivi karibuni Uganda na Tanzania.  Nchi iliyokumbwa na umaskini mkubwa na mzozo ya Sudan Kusini, ambako watu milioni sita tayari wanateseka kutokana na uhaba wa chakula, lilitangaza Jumanne kuwa wadudu hao wamewasili huko pia.

Waziri wa kilimo Onyoti Adigo aliwaambia waandishi habari katika mji mkuu Juba kwamba nzige hao walikuwa wameingia katika maeneo ya Magwi, Lobone, Panyikwara na Owiny-Kibul katika jimbo la Equatoria Mashariki, karibu na mpaka wa nchi hiyo na Uganda. "Tunatoa wito kwa serikali ya Sudan Kusini na wasamaria wema kuingilia kati," alisema.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Michael Pompeo, aliekuwa ziarani barani Afrika, alitangaza katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa siku ya Jumanne, kwamba Marekani ingetoa kiasi cha dola milioni 8 juu ya msaada wake wa ufadhli kusaidia operesheni za kikanda za kukabiliana na nzige nchini Ethiopia, Kenya na Somalia.

Somalia ruft Notstand aus wegen Heuschreckenplage
Wafanyakazi wa Kisomali wakipuliza nzige kwenye mapori ya miba jangwani ambayo ndiyo mazalio ya nzige wa jangwani.Picha: picture-alliance/dpa/AP/B. Curtis

Kwa mujibu wa shirika la Chakula na Kilimo Duniani FAO, kutapakaa kwa nzige kunaendelea kuongezeka ukubwa katika pande mbili za bahari ya Shamu na kuhamia kwenye maeneo ya mkabala. Kwa sasa nchi za Yemen, Saudi Arabia, Oman na Iran zimeathiriwa pia. Pakistan ilitangaza dharura ya kitaifa kuhusiana na wadudu hao wanaoruka.

Nzige wa jangwani ni miongoni mwa wadudu hatari zaidi wanaohama duniani: Kundi la kilomita moja ya mraba linaweza kula kinacholingana na chakula cha watu 35,000 katika muda wa siku moja, imeonya ofisi ya Umoja wa Mataifa inayohusika na uratibu wa masuala ya kiutu OCHA.

Chanzo: dpae