1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika na G-20

1 Aprili 2009

Mkutano wa mataifa 20 tajiri na hatima ya Afrika mjini London:

https://p.dw.com/p/HOQI
Brown na Bush: G-20Picha: AP

Mkutano wa kundi la mataifa 20 tajiri ulimwenguni (G-20) mjini London leo, unamtwika mzigo mzito muakilishi wa Afrika katika mkutano huo -waziri-mkuu Meles Zenawi wa Ethiopia -jukumu la kuufanya mkutano wa matajiri hao kutegea sikio kilio cha nchi masikini za Afrika.

Akiwa amealikwa na mwenyeji Uingereza ,Zenawi,ni mwenyekiti wa sasa wa NEPAD- Ushirika mpya kwa Maendeleo ya Afrika. Mbali na Rais Motlante wa Afrika Kusini, kiongozi wa Ethiopia, ni sauti pekee ya Afrika mjini London .

Tayari, waziri-mkuu wa Ethiopia ,Meles Zenawi alikuwa London wiki mbili nyuma kwa mashauriano yaliotangulia mkutano wa leo wa G-20.Alifuatana na maafisa wa kiafrika na walioandaa mkutano wa leo wa kilele pamoja nao waziri mkuu wa Uingereza Gordon Brown.Risala aliotoa Zenawi kwa waziri mkuu Brown, ilikuwa wazi:

Mataifa tajiri hayamudu kutolijali bara la Afrika kutokana na msukosuko wa kiuchumi ulioibuka ulimwenguni. mawazo yake hayo yanaungwamkono na mawaziri wa biashara wa kiafrika waliokutana Addis Ababa hapo Machi 19,katika Makao makuu ya Umoja wa Afrika.Msimamo wao:

"Kutokana na msukosuko wa uchumi duniani, kuna haja sasa kuliko wakati wowote ule kuweka maendeleo ya Afrika katika shina za juhudi za kimataifa za kutunga mikakati ya kuustawisha uchumi ulimwenguni."Taarifa yao ilisema mwishoni mwa kikao chao cha siku 2 mjini Addis Ababa.Zaidi :

"Gharama ya kutolijali bara la Afrika wakati nchi za viwanda za kaskazini zinamimina vitita vya fedha kuinusuru banki moja tu nchini mwao, zitakuwa kubwa mno." Aliona Tfera Adebe,makamo-mkuu wa Idara ya taftishi za kiuchumi katika Banki ya Taifa ya Ethiopia.

Kwahivyo, bara la afrika linapswa leo kuwayakinisha viongozi wa kundi hili la G-20 la mataifa tajiri kujiepusha na kujilinda kibiashara mbali na kuzishawishi kulijumuisha bara la Afrika katika mipango yao ya kuutia jeki uchumi.

Bara la Afrika linachangia 3% ya biashara nzima ya dunia na hii ameonya Dr.Assefa Zewede,mtaalamu wa uchumi yaweza kuongoza lisitiwe bara hili maanani mkutanoni.

Kwani anaaona mataifa tajiri hayatalijali bara la Afrika wakati uchumi wao umekumbwa na misukosuko, kwani "sadaka huanza nyumbani".

Hatahivyo, nchi za afrika zinalitaka kundi la nchi 20 tajiri duniani kutumia fursa hii ya msukosuko kuleta mfumo wa haki na wa usawsa wa biashara duniani.Na huu ndio msimamo anaotazamiwa waziri mkuu Zenawi wa Ethiopia kuuchukua leo mkutanoni.

Ni kweli kuwa bara la Afrika ambao halikuusababisha hata kidogo msukosuko uliozuka wa kiuchumi linalipa tayari gharama yake.Kwa muujibu wa mabingwa wa kibiashara,msukosuko wa uchumi umeshaathiri bidhaa inazosafirisha Afrika ngambo,raslimali zinazotiwa barani humo,bei za mali ghafi,fedha wanazopeleka wafanyikazi wa Afrika waishio ngambo,vipimo vya kubadilisha fedha na nafasi za kazi.

Kwa kuporomoka kwa uchumi ulimwenguni ,ukuaji uchumi barani afrika umeteremka hadi kima cha 5.1% mwaka jana 2008 kutoka kima cha 6 mwaka uliotangulia 2007-hii ni kwa muujibu wa ripoti ya mwaka huu 2009 ya Tume ya uchumi ya UM kwa Afrika.Kima hicho kinatazamiwa hata kupungua zaidi na kuwa 4.1% mwaka huu.

Ripoti inaonya msukosuko huu wa uchumi utaendelea hadi mwishoni mwa mwaka huu 2009,utadhofisha biashara kati ya Afrika na Ulaya na Marekani na kuifanya hata China ipunguze bidhaa inazoagiza kutoka Afrika.Yote hayo yataudumaza uchumi wa Afrika.Afrika nzima kwahivyo, inaninginiza roho yale kwa kikao cha leo cha G-290 mjini London.

Muandishi: Ramadhan Ali

Mhariri:J.Charo