1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika na zao la Cocoa.

Mohammed AbdulRahman31 Oktoba 2006

Bei zinapangwa na wanunuzi ,nchi za ulaya na Marekani kwa gharama ya wakulima barani Afrika.

https://p.dw.com/p/CHmC
Mkulima wa kiafrika na zao lake la Cocoa
Mkulima wa kiafrika na zao lake la CocoaPicha: TransFair

Afrika hulima zaidi ya 75 ya zao la Cocoa duniani, lakini kwa mujibu wa Shirika la chakula na kilimo la Umoja wa mataifa, bara hilo hutumia lenyewe asili mia 2 tu ya zao hili. Sehemu kubwa iliobakia hupelekwa Ulaya na Marekani, maeneo ambayo baadhi wanasema ndiyo yenye usemi mkubwa wa bei za Cocoa.

Wakosoaji wanasema bei hizo za Cocoa hupangwa na wanunuzi hao wa Ulaya na Marekani bila ya kujadili gharama na jasho la mkulima aliyelima zao hilo. Kwa maneno mengine hakuna zingatio la haki katika upangaji bei. Mbali na hayo Cocoa ya daraja ya chini kutoka Afrika hununuliwa pia kwa bei ya chini mno.

Mhadhiri mmoja wa uchumi wa kilimo katika chuo kikuu cha Ibadan nchini Nigeria, Profesa Abiodun Falusi anasema njia muwafaka zaidi ya kudhibiti kile kinachofanyika katika soko la kimataifa ili kuwa na ushawishi au usemi katika bei ya Cocoa ni kwa Afrika kushajiisha matumizi makubwa kwa wakaazi wake yenyewe

Mataifa ya kiafrika, ingawa ni walimaji wakubwa wa Cocoa pamoja na hayo yanashindwa kuwa na ushawishi katika upangaji bei kwa sababu matumizi ya zao hilo barani mwao ni madogo mno hivyo mahitaji makubwa zaidi ni kwa wanunuzi wakubwa katika nchi za nje. Matokeo yake yanashindwa kuwa na usemi na inakua sawa na kusema “chukua nilichokupa kama bei au acha ule hasara.”

Kwa hakika azimio la kupigania matumizi makubwa a barani Afrika, lilipitishwa Mei mwaka jana mjini Abuja –Nigeria-wakati wa mkutano wa mataifa manane ya kiafrika yanayolima Cocoa. Hayo ni Cote d´Ivoire mlimaji mkubwa kabisa wa Cocoa duniani, Cameroun, gabon, Ghana, Nigeria, sao Tome na Principe , Togo na Uganda.

Nchi hizo zilikubaliana kwamba lengo hilo halinabudi kufikiwa kwa kushajiisha matumizi makubwa ya zao hilo nyumbani na kutoa muamko kwa raia juu ya faida zake kwa afya, pamoja na kushajiisha juu ya utafiti, na maendeleo katika utafutaji masoko kwa Cocoa mpya.

Baadhi ya wajumbe walipendekeza kuepo na utaratibu ambapo, wakulima wakiafrika watakua wakidhibiti bei ya Cocoa sawa na Shirika la mataifa yanayosafirisha mafuta kwa wingi OPEC panapohusika na mafuta.

Zaidi ya hayo mkutano wa Abuja ulitilia mkazo juu ya kuwa na mpango wa kuimarisha biashara ya zao la Cocoa miongoni mwa mataifa ya kiafrika kwa kuzingatia mpango wa mpya wa ushirikiano wa maendeleo barani Afrika-NEPAD na Jumuiya za kimkoa. Mamilioni ya wakaazi barani humo wataweza kunufaika na ushirikiano wa aina hiyo. Wadadisi wanasema hilo likifanikiwa litasaidia nchi zinazolima zao hilo barani Afrika, kuwa na usemi katika upangaji bei wa zao hilo.

Kwa jumla zaidi ya waafrika milioni 20 miongoni mwa mataifa yalio walimaji wakubwa wa zao hilo hutegemea Cocoa kama chanzo cha kuwapatia pato la kukidhi maisha yao ya kila siku.

Katika taarifa ya pamoja baada ya mkutano wa Abuja, nchi walimaji wa zao hilo la Cocoa barani Afrika, zilikubaliana kuyalenga mataifa yasio watumiaji au wanunuzi wao wa jadi wa Cocoa kama vile China na India katika kampeni kabambe ya kimataifa inayolenga kuvutia matumizi makubwa zaidi.