1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Afrika yasonga mbele - Kundi la Jatropha

9 Novemba 2015

Jatropha, ni kikundi kilichoanzishwa mwaka 2011 kwa lengo la kuwakwamua wakazi wa kijiji cha Mwamala kilichopo mkoani Shinyanga nchini Tanzania na hali ngumu ya kiuchumi inayowakabili.

https://p.dw.com/p/1H2Lj
Tansania Shinyanga Maschine
Mtambo wa kutengenezea sabuni kutoka kwa JatrophaPicha: DW/N. Natalis

Kikundi hicho kinatengeneza sabuni, losheni, na mafuta ya kupakaa mwilini. Malighafi inayotumika kutengeneza bidhaa hizo ni pamoja na mafuta yatokanayo na mmea wa mbono.

Mwaka 1999 kilianza kama kikundi cha wakulima wa zao la mtama kikiwa na wananchama 65, kikundi hicho cha wakulima wa zao la mtama kilidumu kwa miaka mitano kikiwa chini ya shirika linalojihusisha na masuala ya kilimo SIDA. Baada ya miaka hiyo mitano katika kikundi hicho ndipo mwaka 2011 shirika hilo likatoa elimu kwa kikundi hicho ya utengenezaji wa sabuni na mafuta yatokanayo na mmea wa mbono au Jatropha kwa lugha ya Kiingereza.

Kikundi hicho kikapewa jina la Jatropha, safari hii kikiwa na wananchama 15. Shughuli zake ni utengenezaji wa sabuni, losheni pamoja na mafuta ya kupaka mwilini.

Makao makuu ya kikundi hicho ni katika kijiji cha Mwamala kilichopo mkoani Shinyanga, Tanzania. Nimetembelea ofisi yao na kujionea shughuli za utengenezaji wa sabuni hizo ambapo kwanza mbegu za mmea wa mbono lazima zikamuliwe ili mafuta yapatikane. Ipo mashine ndogo hapa ambayo ni lazima kutumia nguvu nyingi sana kuisukuma ili kusaga mbegu hizo.

Mwenyekiti wa kikundi hicho, Alfred Tungu, anasema mafunzo waliyoyapata yaliwasidia kuendelea kutengeneza sabuni na mafuta katika kikundi chao.

Tansania Shinyanga Jatropher Gruppe
Mwandishi wa DW Veronica Natalis akizungumza na mwenyekiti wa kundi la Jatropha, Alfred TunguPicha: DW/N. Natalis

Kutokana na ugumu wa kazi hiyo kikundi hicho kwa sasa kimebakiza wanachama wawili tu ambao ni watengenezaji wa bidhaa za sabuni na mafuta.

Mbono kwa kitaalamu Jatropha curcas ni mti wenye mbegu zitoazo mafuta. Huota kwenye maeneo ya nyanda kame na yenye upungufu wa rutuba. Mmea huu hauliwi na mifugo wala wanyama pori na kuufanya ufae kulimwa kwenye maeneo ya wafugaji huria. Mmea huu hutoa mbegu zenye mafuta ambayo hayaliwi bali hutengenezea sabuni, kuendesha mitambo na gesi kama nishati. Kutokana na faida nyingi kwa binaadamu kiafya, kiuchumi na kimazingira, mmea unaweza kuzalishwa kama zao. Mmea huu umetokea Marekani ya Kati na kusambazwa hadi Afrika Mashariki na Wareno.

Tansania Shinyanga Makale Seife
Sabuni ya MakalePicha: DW/N. Natalis

Pamoja na yote hayo, changamoto kubwa inayokikabili kikundi hiki cha Jatropha ni uhaba wa mashine za kisasa za kukamulia mbegu za mafuta, uhaba wa masoko pamoja na uelewa wa jamii kuhusu matumizi ya bidhaa zinazotengenezwa katika maeneo yao.

Mwandishi:Veronica Natalis

Mhariri:Josephat Charo