1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Agizo la Polisi kumhusu Maalim Seif laleta taharuki Zanzibar

Salma Said31 Julai 2019

Agizo la polisi la kumtaka Maalim Seif Sharif Hamad apelekwe Makao Makuu ya Polisi ya Madema limezusha taharuki. Polisi walitoa agizo hilo walipongilia kati kongamano la kuadhimisha miaka 9 ya maridhiano ya Zanzibar.

https://p.dw.com/p/3N6PZ
Sansibar Maalim Seif Sharif Hamad CUF Präsidentschaftskandidat
Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Kongamano la kuadhimisha miaka tisa tokea kufanyika kwa Maridhiano ya Kisiasa yaliyoondosha siasa za chuki ubaguzi na uhasama limefanyika Zanzibar huku Jeshi la polisi likiingilia kati kwa kuamuru kongamano hilo lisimamishwe na kutaka muasisi wa Maridhiano hayo Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad atolewe kwenye ukumbi wa Beit Al Yamin na kupelekwa Makao makuu ya Polisi ya Madema.

Kongamano hilo lilioandaliwa na Kamati ya Maridhiano limevunjika wakati ambao tayari mada ilishawasilishwa na Maalim Seif na kushereheshwa na aliyekuwa Mwanasheria Mkuu wa Serikali ya Zanzibar, Othman Masoud Othman ambapo alimsifu Malim Seif kuwa ni kiongozi mwenye hekima kubwa.

Agizo la Polisi lilileta taharuki wakati Mjumbe wa Kamati ya Maridhiano Eddy Riamy alipoutangazia ukumbi mnamo saa sita mchana kwamba wanalazimika kusitisha kongamano hilo kutokana na amri ya polisi.

Kamanda wa polisi wa mkoa wa mjini Magharibi Thobias Sedoyeka baadae alizungumza na waandishi wa habari na kukanusha kwamba walitoa agizo na badala yake polisi waliokuwa katika doria ya kawaida walikuta watu wameshamaliza kongamano lao.

Maafisa wa polisi wakifanya doria visiwani Zanzibar. (Picha ya maktaba)
Maafisa wa polisi wakifanya doria visiwani Zanzibar. (Picha ya maktaba)Picha: picture-alliance/dpa

Kiongozi wa chama cha ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema kwa muda mrefu Malim anatumia busara za hali ya juu kuhakikisha Zanzibar inabaki salama.

Maalim Seif tayari alishawasilisha mada yake na kufuatiwa baadae na Mzee Moyo ambapo wote kwa pamoja walisisitiza umuhimu wa kuendelezwa kwa Maridhiano licha ya kuwa hayapo kutokana na mfumo uliopo ambao unazidisha hasama na chuki za kisiasa kwa watu kubaguana.

Tarehe kama ya leo mwaka 2010, Wazanzibari kupitia kura ya maoni walichagua kwa zaidi ya asilimia 60 kuongozwa kwa mfumo wa serikali ya umoja wa kitaifa ambayo kwa mara ya kwanza iliundwa baada ya uchaguzi mkuu wa Oktoba 2010 na kuongozwa na Dkt. Ali Mohammed Shein huku Maalim Seif akiwa Makamu wa kwanza wa Rais.

Hatua hiyo ilifikiwa baada ya Maalim Seif akiwa Katibu Mkuu wa Chama Cha Wananchi (CUF) kukutana kwa faragha na aliyekuwa Rais wa Zanzibar Amani Abeid Karume na kukubaliana kufuta siasa chafu za ubaguzi chuki na uhasama. Mkutano wao ulifikia kilele Novemba 5, 2009.