1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ahueni yaendelea kuheshimiwa Gaza

Frank Wörner6 Agosti 2014

Makubaliano ya kusitisha mapigano kwa masaa 72 katika Ukanda wa Gaza yameendelea kuheshimiwa kwa leo, huku wajumbe wa Israel na Palestina wakijiandaa kwa mazungumzo ya kujaribu kurefusha ahueni iliyopo.

https://p.dw.com/p/1CpTR
Wengi wamekuta nyumba zao zimegeuzwa kifusi
Wengi wamekuta nyumba zao zimegeuzwa kifusiPicha: Reuters

Usitishwaji huo wa mapigano umetoa nafasi ya kupumua kwa pande hizo mbili, yaana wapalestina na waisraeli, ambao wamekuwa vitani kwa takribani mwezi mmoja hadi juzi. Huku ahueni hiyo ikibakiza siku moja tu kumalizika, maafisa wanaokutana mjini Cairo wanakabiliwa na kazi ngumu ya kupata makubaliano ya kuendeleza utulivu tete uliopo kwa muda mrefu zaidi.

Masharti makubwa ya wapalestina ni kuitaka Israel ifungue mpaka ya Gaza na kuacha kuizingira, huku waisraeli wakitaka kuhakikisha kwamba Hamas imenyang'anywa silaha na uwezo wa kijeshi kufanya mashambulizi dhidi yake. Waziri wa mambo ya nje wa Palestina Riyad al-Malki amesema anayo matumaini kuwa usitishwaji mapigano utarefushwa kwa angalau masaa mengine 72 wakati mazungumzo yakiendelea. Marekani pia inatarajiwa kuhusika katika mazungumzo hayo yanayoendeshwa na Misri.

Wapalestina warudi nyumbani, wakuta vifusi

Huku hayo yakijiri, wapalestina katika Ukanda wa Gaza wameitumia ahueni iliyopo kutoka mafichoni na kutembelea maeneo waliyokuwa wakiishi. Wengi wao wanakuta vifusi mahali ziliposimama nyumba zao kabla ya mashambulizi kuanza.

Mtaa wa Shejayiah ulipata hasara kubwa zaidi
Mtaa wa Shejayiah ulipata hasara kubwa zaidiPicha: DW/T. Krämer

Katika mtaa wa Shajaiyeh, mashambulizi ya Israel yameangamiza karibu kila kitu. Mtaa mzima umegeuzwa kifusi, nyumba zilizojengwa kwa zege na vyuma zikiwa zimeangukiana. Harufu ya miili ya watu inayooza inasikika kila mahali, na hakuna dalili ya maisha. Wengi wa wakazi wa mtaa huo walikimbilia katika shule ya Umoja wa Mataifa iliyo karibu, kunusuru maisha yao.

Kwa muda wa wiki tatu waliishi katika hali ya msongamano isiyokuwa na faragha, na walisinzia kwa zamu. Hali yao haitarajiwi kuboreka hivi karibuni kwa sababu licha ya ahueni ya vita, hawana nyumba tena. Mmoja wao ni Umm Ibrahim al-Ejla.

''Natumai vita hivi vimeuonyesha ulimwengu. Watu wengi wamekufa na tumepata hasara kubwa, lakini ni kama hakuna anayeona. Ni hali isiyovumilika kwa watu hapa, na naamini dunia nzima imejionea kilichotokea.''

Dhiki itaendelea

Na bado maisha katika Ukanda wa Gaza ni ya wasiwasi mkubwa. Mkazi mmoja, Raida, anasema kila asubuhi husikiliza radio ya Umoja wa Mataifa, wakiwa na shauku ya kujua kinachofuata.

Katika Hospitali ya Shifa ambayo imetembelewa na mwandishi wa DW, wagonjwa wengi waliopelekwa huko ama wamekwishafariki, au wamehamishiwa katika vituo vingine vya afya. Dr Ghassan al-Sitta ambaye alitoka mjini Beirut kuja kusaidia kuwatibu wahanga wa vita, anasema asilimia 80 ya wagonjwa waliojeruhiwa katika mashambulizi ya Israel wamepata vilema vya maisha.

Miongoni mwao ni wanawake na watoto waliokatwa viungo, wengine wakiwa wameungua sehemu za uso. Yupo pia mtoto wa miaka 8 aliyepoteza macho yake yote mawili, na sehemu kubwa ya uso wake. Wengine wengi hawakuweza kunusurika mashambulizi hayo.

Mwandishi:Daniel Gakuba/Marx, Bettina/AFPE

Mhariri: Sekione Kitojo