1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ajali ya treni yaua watu kadhaa Bavaria

Grace Kabogo9 Februari 2016

Watu wasiopungua wanane wamekufa na wengine zaidi ya 150 wamejeruhiwa baada ya treni mbili za abiria kugongana karibu na mji wa Bad Aibling mkoani Bavaria, kusini mwa Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1Hrta
Deutschland Zugunglück bei Bad Aibling
Picha: picture-alliance/dpa/U. Lein

Msemaji wa polisi katika mji wa Rosenheim, Martin Winkler amesema kiasi ya watu 40 wamejeruhiwa vibaya, ambapo waliondolewa kwenye eneo la ajali na kupelekwa hospitali, kwa kutumia helikopta nane za uokozi, huku magari ya kubebea wagonjwa yakiwasafirisha majeruhi ambao hawajaumia sana.

Kampuni binafsi ya treni ya Meridian imeeleza katika taarifa yake kwamba ajali mbaya imetokea baada ya treni zake zilizokuwa zinafanya safari zake kati ya mji wa Rosenheim na Holzkirchen kugongana kwenye majira ya saa moja kamili asubuhi na kusababisha treni zote mbili kuacha njia na mabehewa kadhaa kuanguka.

Hata hivyo chanzo cha ajali hiyo iliyotokea karibu na Bad Aibling, umbali wa kilomita 60 kusini mashariki mwa Munich, hakijafahamika mara moja, ingawa msemaji wa polisi wa jimbo la Bavaria, Stefan Sonntag amesema hiyo ni ajali mbaya kuwahi kutokea katika miaka kadhaa kwenye jimbo hilo. Amesema abiria wengine bado wamekwama kwenye mabehewa.

Shughuli za uokozi kuchukua muda

Polisi wa jimbo la Bavaria wameandika katika mtandao wa kijamii wa Twitter kwamba wafanyakazi kadhaa wa huduma za dharura pamoja na madaktari wa dharura wako katika eneo ilipotokea ajali hiyo na njia hiyo ya treni pamoja na barabara mbili zimefungwa. Helikopta kadhaa kutoka Austria pia zinaendelea na juhudi za uokozi.

Msemaji wa serikali ya shirikisho katika jimbo la Bavaria, Matthias Knott amesema eneo hilo halifikiki kwa urahisi, hali inayosababisha juhudi za uokozi kuwa ngumu zaidi. Amesema ajali hiyo imetokea karibu na Mto Mangfall kwenye eneo lenye msitu mnene pamoja na milima.

Shirika la habari la Ujerumani, DPA, limemnukuu Bernd Rosenbusch, mkuu wa Shirika la treni la Bavaria, linaloziendesha treni hizo, akisema kuwa hiyo ni ajali kubwa ya kushtusha. Amesema wanafanya kila linalowezekana kuwasaidia abiria, ndugu pamoja na wafanyakazi.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/APE,RTRE,AFPE

Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman