1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al Jazeera yaikasirisha Palestina

24 Januari 2011

Nyaraka za siri kwenye mazungumzo ya kutafuta amani kati ya viongozi wa Palestina, Israel na Marekani, zilizoanza kuchapishwa jana na kituo cha Al-Jazeera, zimeanza kuwagawa Wapalestina na kuzusha hasira miongoni mwao.

https://p.dw.com/p/1027t
Spika wa Bunge la Palestina, Abdel-Aziz Dweik
Spika wa Bunge la Palestina, Abdel-Aziz DweikPicha: picture alliance/dpa

Inawezekana, ikawa hii si mara ya kwanza kwa taarifa za siri za utawala wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina kuwekwa hadharani, lakini ni mara ya kwanza kwa kiwango kikubwa kama hiki cha taarifa kutangazwa kwa pamoja na kwa wakati mmoja.

Tayari viongozi wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina wanakishutumu kituo cha Al Jazeera kwamba kina ajenda ya siri ya kuichafua taswira yao, kwa kile wanachokiita 'kutangaza uongo na nusu ukweli'. Rais wa Mamlaka hayo, Mahmoud Abbas ameziita nyaraka hizi ni upuuzi mtupu, ambao unakusudia kuwachangaya watu.

"Sisi hatuna siri yoyote ambayo jamii za Kiarabu hauijui." Amesema Abbas.

Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina akikagua sehemu za ulinzi za mamlaka yake
Rais Mahmoud Abbas wa Mamlaka ya Ndani ya Palestina akikagua sehemu za ulinzi za mamlaka yakePicha: picture-alliance/dpa

Mapema, kiongozi wa ujumbe wa wapatanishi wa Palestina katika mazungumzo yake na Israel, Saeeb Erakat, alikana kabisa kutoa tamko lolote ambalo linamaanisha kuyatoa sadaka kwa Waisraeli, maeneo ambayo Palestina imezingatia kwamba ni yake kwa muda mrefu, likiwemo la Jerusalem ya Mashariki.

"Nataka kuuambia ulimwengu kwamba mimi sina kitu cha kuficha. Mara kadhaa nimesema kuwa Mamlaka ya Palestina kamwe haitotoa eneo lolote lile ambalo ni haki yetu. Ikiwa tuliwapa Waisraeli hiyo wanayoiita Al Jazeera kama Jerusalem kubwa kabisa, kwa nini basi Israel haikusaini mkataba wa makubaliano?" Amesema Erakat.

Lakini si kila mtu anaamini kwamba Erakat na wenzake katika Mamlaka ya Ndani ya Palestina hawakutoa mapendekezo ya kuihalalishia au kuipa Israel maeneo mengi zaidi ya ardhi yao. Abed Dandis, muuza duka wa Kipalestina katika sehemu ya mji mkongwe ya Jerusalem, aliliambia Shirika la Habari la AFP, kwamba viongozi wao wamekuwa kila siku wanalaza shingo zaidi wanapokuwa mbele ya Israel.

"Kilichowekwa hadharani na Al-Jazeera si kipya. Tumekuwa tukijuwa muda mrefu. Unaweza kufahamu kwamba katika makubaliano, lazima ukubali kutoa baadhi ya mambo ili kupata kitu fulani, lakini sisi Wapalestina tunatoa tu bila ya kupokea chochote." Amesema Dandis.

Kwa mujibu wa waziri wa zamani ya mambo ya nje wa Israel, Shlomo Ben-Ami, anasema kwamba kile kinachosemwa kuwa ni sadaka ambayo Erakat na wenzake walikubali kuipa Israel, ilikubalika hivyo tangu wakati wa kiongozi wa Palestina, Marehemu Yasser Arafat.

"Mapendekezo haya ni kama yale ambayo Wapalestina walikubaliana nayo katika Camp David, kupitia upatanishi wa Bill Clinton na ugawaji wa mji wa Jerusalem kwa kutegemea misingi ya kidini, yaani sio kuwa na Jerusalem ya Mashariki na ya Magharibi, bali kusema kuwa kila cha Kiyahudi ni cha Israel na kila cha Kiarabu ni cha Palestina." Ben-Ami amekiambia kituo cha habari cha Al-Jazeera.

Wakati huo huo, taarifa zinasema kwamba wakaazi wa mji wa Ramallah katika eneo la Gaza wameanza kufanya maandamano ya kuupiga utawala wa ndani ya Palestina kutokana na taarifa zilizoibuliwa na Al-Jazeera.

Mwandishi: Mohammed Khelef/AFP/Reuters
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman