1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Al-Qaeda waachia huru mamia ya wafungwa Yemen

2 Aprili 2015

Wanamgambo wa Al-Qaeda wamevamia gereza moja kusinimashariki mwa nchi hiyo na kuwaachia huru mamia ya wafungwa akiwemo mmoja wa viongozi wake Khalid Bartafi

https://p.dw.com/p/1F1mf
Moshi ukifuka kutoka kiwanda cha maziwa kilichoshambuliwa na vikosi washirika
Moshi ukifuka kutoka kiwanda cha maziwa kilichoshambuliwa na vikosi washirikaPicha: Reuters

Wanamgambo wa Al-Qaeda wamevamia gereza moja kusinimashariki mwa nchi hiyo na kuwaachia huru mamia ya wafungwa akiwemo mmoja wa viongozi wake.Afisa wa usalama aliyetoa taarifa hizi amesema walinzi wawili na wafungwa watano wameuwawa katika mapambano yaliyozuka.Upande mwingine wapiganaji wahouthi warudi nyuma katika mapambano yanayoendelea kusini mwa nchi hiyo.

Wanamgambo wa A-Qaeda waliovamia gereze na kuwaachia huru wafungwa zaidi ya 300 huku Kusini mashariki mwa Yemen pia walipambana na vikosi vya ulinzi wa jengo la serikali katika mji wa Mukalla ambako kuna tawi pia la benki kuu na makao makuu ya polisi.Mapigano yalizuka kwenye eneo hilo na katika eneo la makaazi ya rais kwenye mji huo kwa mujibu wa maafisa wa polisi.

Wafuasi wa Houthi wakiandamana kupinga Uingiliaji Kati wa Saudi Arabia
Wafuasi wa Houthi wakiandamana kupinga Uingiliaji Kati wa Saudi ArabiaPicha: picture-alliance/epa/Y. Arhab

Aidha maafisa wamesema wanamgambo hao hawakukabiliwa na upinzani wakati wakiiyateka makao makuu ya kituo kimoja cha redio na kutatiza matangazo ya kituo hicho.Wanamgambo hao wa Alqeda wamemkomboa kutoka gereza walilolivamia,katika mkoa wa Hadramawt mmoja wa kiongozi wa juu wa kundi hilo Khalid Bartafi anayefahamika kwa dhima aliyobeba mwaka 2011 hadi 2012 katika mapambano na wanajeshi wa serikali ya Yemen wakati makundi ya itikadi kali yalipotwaa sehemu kubwa ya kusini na mashariki.

Bartafi ni mmoja wa makamanda wa ngazi ya juu wa kundi la Al-Qaeda katika rasi ya Uarabuni AQAP kundi ambalo Marekani imeliweka katika orodha ya mitandao hatari kabisa,wakati waangalizi wakionya kwamba kundi hilo linaweza kuutanua mgogoro kujiimarisha katika nchi hiyo.Wakati huohuo upande wa Kusini katika mji wa Aden inaarifiwa wapiganaji wa Kihouthi wamerudi nyuma kutoka maeneo waliyokuwa wakiyadhibiti baada ya kuzidiwa nguvu na mashambulizi ya anga yanayofanywa na vikosi washirika yakiongozwa na Saudi Arabia.

Inaelezwa kwamba kundi la wapiganaji hao wakihouthi pamoja na washirika wao waliokuwa wamesogea mbele kwa kutumia vifaru na magari ya kijeshi hadi wilaya ya Khor Maksar huko Aden walibidi kurudi nyuma.Wapiganaji wakihouthi hivi karibuni walipata nguvu Aden na kuonekana kudhibiti eneo hilo ambalo ni ngome ya mwisho ya wafuasi wa rais anayeungwa mkono na Saudi Arabia Abd-Rabbu Masour Hadi licha ya kuweko mashambulizi ya anga kwa muda wa wiki nzima yakifanywa na Saudi Arabia na majeshi washirika hasa kutokea nchi za Kiarabu za kisunni.

Mapambano ya Aden
Mapambano ya AdenPicha: Reuters

Kutokana na wasiwasi kwamba huenda wahouthi wakafanikiwa kuudhibiti kimamilifu mji huo wa Aden,jana waziri wa mambo ya nje katika serikali ya Hadi Reyad Yassin Abdulla alitowa mwito wa kuchukuliwa hatua zaidi za Kimataifa kuwazuia wapiganaji hao wakishia wanaoungwa mkono na Iran kabla ya kuudhibiti mji wa Aden.Fauka ya hayo inaarifiwa zaidi ya raia 350 wa India waliokuwa wamekwama nchini Yemen wamewasili nyumbani leo na kukaribishwa kwa furaha na familia zao na marafiki.

Raia hao wa India waliondolewa kwenye mapigano na meli ya kijeshi ya nchi yao kutoka mji wa Aden hadi Djibouti na baadae kusafirishwa kwa ndege mbili za kijeshi kutoka Djibouti hadi Mumbai na Kochi.Kwa mujibu wa wizara ya mambo ya ndani ya Yemen kuna raia kiasi 4000 wa India wanaofanya kazi Yemen,wafanyabiashara na wauguzi na wengi wamekwama katika miji ya Aden na Sanaa.

Mwandishi:Saumu Mwasimba/DPA/RTRE

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman