1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Albino mwingine akatwa mkono Tanzania

17 Februari 2013

Visa vya kunyofolewa viungo maalbino vinavyoongezeka kwa kasi mpya vimeanza kuwatisha watu wenye ulemavu huo wa ngozi na mashirika ya kutetea haki za binadamu nchini Tanzania

https://p.dw.com/p/17fja
Kijana mwenye ulemavu wa ngozi akitazama televisheni na nduguze
Kijana mwenye ulemavu wa ngozi akitazama televisheni na nduguzePicha: picture alliance/CTK

Washambuliaji wanaokusanya viungo vya mwili vya watu wenye ulemavu wa ngozi, (Albino) kwa ajili ya itikadi za kishirikina wamemkata mkono kijana wa kiume mwenye umri wa miaka 7 nchini Tanzania, ikiwa ni tukio la hivi karibuni kabisa katika mfululizo wa mashambulizi ya kinyama dhidi ya watu hao.

Taarifa hizo zimetolewa leo Jumapili na maafisa nchini Tanzania.Kijana huyo Mwigulu Magessa ambaye yuko Hospitali kwa sasa alikatwa mkono wake Jumamosi usiku katika wilaya ya Milepa iliyoko Kusini Magharibi ya Tanzania. Kwa mujibu wa taarifa za afisa wa serikali katika eneo hilo, Apolinary Macheta, kijana huyo alishambuliwa na watu watatu wakati alipokuwa akitembea kuelekea nyumbani kwao akiwa pamoja na marafiki zake wanne wakitokea shule.

Viuongo vya maalbino vinatumiwa sana na waganga wa kienyeji barani Afrika kuvutia utajiri
Viungo vya maalbino vinatumiwa sana na waganga wa kienyeji barani Afrika kuvutia utajiriPicha: AP

Imani za kishirikina

Tukio hilo limefanyika siku kadhaa baada ya mwanamke mmoja mwenye ulemavu huo wa ngozi na mama wa watoto wanne aliponyofolewa mkono wake na watu waliokuwa na mapanga. Polisi inasema wameshawakamata watu watano kufuatia tukio hilo baada ya kugundua mkono huo uliokuwa unaoza ukiwa umefichwa kwenye shamba.

Nchini Tanzania watu wanaoishi na ulemavu wa ngozi wanauwawa na kutengwa kufuatia fikra potovu za kishirikina zilizoenea kwamba viuongo vya mwili vya watu hao vinaleta bahati na utajiri kupitia shughuli za kichawi. Kimsingi ulemavu huo wa ngozi unatokana na hitilafu za kinasaba zinazohusishwa na upungufu wa seli za Melanin zinazotengeneza rangi ya ngozi,nywele na macho kwa ajili ya kuvikinga dhidi ya miale ya jua.

Watoto wakiandamana pamoja bila ya kujali tofauti ya maumbile yao
Watoto wakiandamana pamoja bila ya kujali tofauti ya maumbile yaoPicha: LAIF

Watu wenye ulemavu huo wanakabiliwa na hali ya kutengwa pamoja na kuwa katika hatari ya kuuwawa katika nchi nyingi za Kiafrika.

Itakumbukwa kwamba mwezi wa Januari mtoto mmoja aliyekuwa albino alifariki katika mkoa wa Tabora baada ya wachambuliaji kumkata mkono wake kwa kutumia panga. Kijo Bisimba kutoka kituo cha sheria na haki za binadamu nchini Tanzania amesema kwamba mashambulio hayo yanaongezeka kwa kiasi cha kushtusha hali ambayo inazusha tena wasiwasi mpya baada ya miezi kadhaa ya utulivu.

Mauaji ya aina hiyo ya kishirikiana yamekuwa pia yakitokea katika nchi jirani ya Burundi na baadhi ya washambuliaji wanashukiwa kutokea nchini Tanzania ambako viuongo vya maalbino vinaweza kumletea mtu maelfu ya dola.

Mwandishi:Saumu Mwasimba

Mhariri:Bruce Amani