1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Navalny akamatwa katika maandamano ya Urusi

Yusra Buwayhid
5 Mei 2018

Kiongozi wa upinzani Urusi Alexei Navalny na watu wengine 200 wamekamatwa na polisi katika maandamano ya nchi nzima ya kupinga kuapishwa urais Vladimir Putin. Navalny alizuiwa kushiriki uchaguzi wa rais wa Machi.

https://p.dw.com/p/2xDpz
Proteste in Russland Moskau
Picha: DW/M. Komadovsky

Polisi wa Urusi katika mji mkuu wa Moscow imemkamata kiongozi wa upinzani wa kisiasa Alexei Navalny katika maandamano dhidi ya Rais Urusi Vladimir Putin. Kukamatwa huko kwa Navalny kumetokea katika maandamano ya maelfu ya watu kati kati ya mji mkuu, kulingana na taarifa za vyombo vya habari vya Urusi.

Aidha watu wapatao 200 wanaomuunga mkono Navalny wamekamatwa katika maandamano ya nchi nzima yaliyoanza Jumamosi kabla ya Putin kuapishwa Jumatatu kwa muhula mwengine wa nne kama rais.

Navalny aliyezuiliwa kushiriki katika uchaguzi wa rais mwezi Machi dhidi ya Putin, amewatolea wito raia wa Urusi kuandaa siku ya maandamano nchini kote kabla ya Putin kuapishwa.

Maandamano yalianza katika maeneo ya Urusi ya Mashariki ya Mbali na Serbia, huku waandamanaji kadhaa wakiwa wameshakamatwa na polisi, imesema timu ya Navalny pamoja na wachunguzi wa kujitegemea.

Katika mji wa Krasnoyarsk mashariki mwa Serbia, watu 15 akiwamo mwandishi habari wamekamatwa na polisi, limesema kundi la wachunguzi wa kujitegemea la OVD-Info.

"Ukamataji unafanywa kwa kutumia nguvu," limesema kundi hilo, na kuongeza baadhi ya waliokamatwa wamepata majeraha na mikwaruzo mwilini.

Russischer Oppositionsführer Alexei Navalny
Kiongozi wa upinzani wa kisiasa Urusi, Alexei NavalnyPicha: picture alliance/AP/E. Feldman

Waandamanaji wapatao kumi wamekamatwa katika mji wa Serbia wa Barnaul, imesema timu ya Navalny. Watu wengine kumi na nane wakiwamo wachimba migodi wamekamatwa Novokuznetsk kusini magharibi mwa Serbia, kwa mujibu wa OVD-Info. Katika mji wa Chelyabinsk uliopo eneo la milima la Urals, polisi imewatia mbaroni watu watatu kabla ya kuanza maandamano, ameandika mwanaharakati  Boris Zolotaryovsky katika ukurasa wake wa Facebook. Katika miji ya Moscow na St.Petersburg --- ambako maandamano yanatarajiwa kufanyika Jumamosi mchana-- serikali haikutoa ruhusu ya kufanyiak maandamano.

Wafuasi wa Putin nao waandamana

Kabla ya kuanza maandamano hayo, wanaharakati kadhaa wa Putin walimiminika katika uwanja uliopo katikati ya mji mkuu wa Urusi, walipokuwa wamekusanyika wafuasi wa Navalny, kulingana na taarifa za waandishi habari wa AFP.

Wanaharakati wanaomuunga mkono Putin wakipiga mayowe "Nchi yetu, sheria zetu" pamoja na "Tunamuunga mkono Putin."

Putin ameshinda ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa mwezi Machi, na kuendeleza utawala wake katika taifa kubwa zaidi duniani kwa miaka mengine sita hadi 2024. Hatua hiyo itamfanya kuwa kiongozi aliyebaki madarakani kwa muda mrefu zaidi tokea kuondoka kwa kiongozi wa kidikteta wa uongozi wa Kisovieti Josef Stalin alieongoza kwa zaidi ya miaka 30.

"Tutailazimisha serikali ya matapeli na wizi kukabiliana na mamilioni ya raia ambao hawakumpigia kura Putin." yanasema maandishi ya bango la Navalny akiwahamasisha watu kuandamana mapema kabla ya maandamano hayo kuanza.

Navalny amekuwa akiwekwa jela na polisi mara kwa mara kwa kuandaa maandamano sawa na hayo katika siku za nyuma. Ameitisha maandamano katika zaidi ya miji 90 mikubwa na midogo, ukiwamo mji wa Moscow na St.Peterburg.

Taarifa za habari pamoja na taarifa zionazasambazwa katika mitandao ya kijamii zinasema kwamba maandamano hayo yamevutia mamia ya watu au zaidi ya idadi hiyo katika takriban miji 10 pamoja na maeneo mengine ya Mashariki ya Mbali na Serbia.

Putin ameshakuwepo madarakani kwa miaka 18!" mwanaharakati mmoja ameliambia kundi la watu katika mji wa Urusi wa Khabarovsk.

Putin, 65, amekuwa madarakani, kama rais au kama waziri mkuu, tokea mwaka 2000.

Akiungwa mkono na kituo cha televisheni cha serikali pamoja na chama tawala, huku akiwa na uungwaji mkono wa asilimia 80, anatazamwa na wafuasi wake kama baba wa taifa ambaye ameirejesha tena ari ya nchi hiyo, na kuupanua ushawishi wa Urusi kwa kuingilia kati vita vya Syria na Ukraine.

Russland Wladimir Putin, Präsident
Rais wa Urusi Vladimir PutinPicha: picture-alliance/AP Photos/Sputnik/Kremlin/M. Klimentyev

Maandamano yaliyo kinyume na sheria

Serikali ya Urusi inayatazama maandamano hayo kuwa ni kinyume na sheria, ikidai kwamba haikuafiki wakati na sehemu yanapofanyika maandamano hayo.

Polisi ya Urusi imekuwa ikivunja maandamano ya aina hayo katika siku za nyuma, wakati mwengine kwa kutumia nguvu na kuwatia mbaroni mamia ya waandamanaji.

Putin amempuuzilia mbali Navalny, aliyepigwa marufuku kushiriki katika uchaguzi huo wa rais kama mtu matata anaetaka kuleta vurugu nchini kwa niaba ya Marekani.

Waziri Mkuu wa Urusi Dmitry Medvedev, mshirika wa karibu wa Putin, amemwita Navalny kuwa ni laghai wa kisiasa. Putin anatarajiwa kuapishwa katika sherehe kubwa Jumatatu mjini Moscow.

Akiwa ameshinda asilimi 77 ya kura ambayo ni sawa na kura milioni 56, ushindi wa uchaguzi wa Machi ulikuwa ni mkubwa zaidi kuliko wa kiongozi yeyote mwengine wa baada ya utawala Kisovieti. Ni ushindi ambao anaamini -akiungwa mkono na washirika wake - kuwa unampa mamlaka ya kutawala.

Hata hivyo, waangalizi wa Ulaya wamesema hakujakuwa na jinsi nyingine yoyote katika uchaguzi huo, na kulalamika kwamba kulikuwa na shinikizo dhidi ya sauti za wakosoaji.

Wakosoaji kama Navalny wanamshutumu putin kwa kuongoza mfumo wa mamlaka uliogubikwa na rushwa na kwa kulitwaa eneo la Ukraine la Crimea kinyume na sheria mwaka 2014, hatua iliyopelekea Urusi kutengwa na jumuiya ya kimataifa.

Mwandishi: Yusra Buwayhid/afp/rtre/ap

Mhariri: Jacob Safari