1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aliyemuua mbunge Uingereza anatibiwa maradhi ya akili

Isaac Gamba17 Juni 2016

Taifa la Uingereza limekumbwa na hali ya majonzi kufuatia kuuawa kwa mbunge mmoja kutoka katika chama cha upinzani nchini humo cha Labour Jo Cox .

https://p.dw.com/p/1J8ff
Mbunge wa chama cha Labour Jo Cox aliyeuawa
Mbunge wa chama cha Labour Jo Cox aiyeuawaPicha: Reuters/N. Hall

Tayari taarifa kuhusu mshukiwa wa mauaji ya mbunge huyo, Thomas Mair, zimeanza kujitokeza. Kwa mujibu wa nduguye wa kiume, bwana huyo mwenye umri wa miaka 52, anatibiwa ugonjwa wa akili. Kituo kinachopinga ubaguzi nchini Marekani, Southern Poverty Law, kimesema mtuhumiwa huyo amekuwa akiliunga mkono kwa miaka kadhaa kundi la wanazi mambo leo la National Alliance na amewahi kulichangia kifedha. Kwa mujibu wa polisi, chanzo cha shambulio hilo bado hakijulikani.

Jo Cox , mwenye umri wa miaka 41 na ambaye amekuwa msitari wa mbele katika kampeni ya kuhamasisha Uingereza kuendelea kubaki katika Umoja wa Ulaya, aliuawa nje ya maktaba moja ambako mara nyingi amezoea kukutana na wananchi wa jimbo lake la uchaguzi katika kijiji anachotoka cha Birstall kilichoko kaskazini mwa Uingereza hapo jana tarehe 16,06,2016.

Mashahidi wa mkasa huo wanasema mwanasiasa huyo ambaye ni mama wa watoto wawili alipigwa risasi mara kadhaa na pia kuchomwa kisu.

Mmoja wa mashahidi wa tukio hilo Clarke Rothwell alisikika akisema kuwa mtu aliyehusika na mauaji hayo alisikika akipaza sauti kabla na baada ya tukio akisema " Uingereza kwanza "

Kampeni kuelekea kura ya maoni Uingereza zasimamishwa kwa muda

Zikiwa zimesalia siku sita kabla ya kuitishwa kwa kura ya maoni pande zinazohasimiana ambazo zinapiga kampeni kuu nga mkono kujiondoa au kubaki kwa Uingereza katika Umoja wa Ulaya zilisimasha kampeni zake hizo na wanasiasa nao wameungana kupinga mauaji hayo.

Wapelelezi nchini Uingereza wakiendelea na uchunguzi wa tukio la mauaji ya Jo Cox
Wapelelezi nchini Uingereza wakiendelea na uchunguzi wa tukio la mauaji ya Jo CoxPicha: Reuters/C. Brough

Hata hivyo wachambuzi wamehoji iwapo muuaji anaweza kuchochewa na maudhui ya kampeni hizo ambazo zimekuwa zikiendelea ambazo zimeibua mvutano mkubwa kwa kugusia masuala ya kitambulisho cha kitaifa pamoja na masuala ya uhamiaji.

Gazeti la Times nchini humo limeripoti kuwa Cox ambaye anakuwa mbunge wa kwanza kuuawa tangu mwaka 1990 amekuwa akiandamwa na ujumbe wa vitisho uliotumwa kwake katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita. Kwa mujibu wa gazeti hilo polisi nchini humo walikuwa wakifikiria kuweka ulinzi wa ziada na kuongeza kuwa kulikuwa hakuna uhusiano na ujumbe huo uliotumwa na tukio hilo la mauaji hapo .

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron ashitushwa na mauaji ya Jo Cox

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron naye pia ameshtushwa na tukio la mauaji ya mwanasiasa huyo akisema haya ni maafa makubwa na ni habari za kushitusha. Ametoa rambirambi kwa mume wa mawanasiasa huyo Brendan, watoto wake wawili na familia yake kwa ujumla. Cameron amesema Uingereza imempoteza mwanasiasa na mbunge ambaye alikuwa hodari katika masuala ya kampeni na akifanya hivyo kwa moyo wake wote na kuwa watu wameshitushwa na mauaji hayo.

Waziri Mkuu wa Uingereza David Cameron
Waziri Mkuu wa Uingereza David CameronPicha: Getty Images/Sky News/Pool/C. Lobina

Awali watu kadhaa waliokuwa na nyuso za majonzi walikusanyika nje ya jengo la bunge la nchi hiyo katika hafla ya kumkumbuka mwanasiasa huyo, tukio ambalo limehudhuriwa pia na kiongozi wa chama cha Labour, Jeremy Corbyn.

Cox ambaye alichaguliwa kuwa mbunge mwaka jana tayari alikuwa amejijengea umaarufu kutokana na jitihada zake za kuishawishi serikali ya nchi hiyo kufanya zaidi katika kuwasaidia wakimbizi wanaotokea nchini Syria na pia kampeni yake ya kuhamasisha Uingereza kuendelea kubakia katika Umoja wa Ulaya.

Mwandishi : Isaac Gamba/ AFPE

Mhariri: Josephat Charo