1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AMMAN: El Baradei kuzuru Jordan

1 Aprili 2007
https://p.dw.com/p/CCDN

Kiongozi wa shirika la kimatiafa la kuzuia utapakazaji wa silaha za kinyuklia, IAEA, bwana Mohammed El Baradei, ataitembelea Jordan baadaye mwezi huu kuzungumza na viongozi wa nchi hiyo.

Wizara ya mashauri ya kigeni nchini Jordan imesema mazungumzo hayo yatatuwama juu ya azma ya Jordan kutaka kuwa na nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani.

Mohammed El Baradei atafanya ziara ya siku tatu mjini Amman kuanzia tarehe 14 mwezi huu. Msemaji wake amesema kiongozi huyo atazungumza kwa kina na viongozi wa Jordan wanaotaka nchi yao iwe na teknolojia ya nyuklia na ataitembelea baadhi ya miradi inayodhaminiwa na shirika la IAEA nchini humo.

Mfalme Abdullah II wa Jordan alisema katika mkutano wa kilele wa viongozi wa kiarabu uliofanyika wiki iliyopita mjini Riyadh, Saudi Arabia kwamba nchi za kiarabu zinahitaji nishati ya nyuklia kwa matumizi ya amani kuziwezesha kujenga jamii na kuziendeleza sekta za sayansi, viwanda, kilimo na afya.

Alitoa mwito kuundwe kituo cha kiarabu cha matumizi ya nishati ya nyuklia kwa amani.