1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amnesty: 2016 ulikuwa mwaka mbaya wa haki za binadamu

Grace Kabogo
22 Februari 2017

Shirika la kimataifa la haki za binaadamu, Amnesty International, limesema mwaka 2016 ulikuwa mwaka mbaya katika suala zima la haki za binaadamu, huku uhalifu wa kivita ukiwa umefanywa duniani kote.

https://p.dw.com/p/2Y1UL
Südsudan UN denken über Verstärkung von Unmiss nach
Picha: picture alliance/AP Photo/J. Patinkin

Ripoti mpya ya mwaka ya Amnesty International iliyotolewa jana mjini Paris, Ufaransa inaeleza jinsi 2016 ulivyokuwa mgumu na wenye huzuni, ambapo habari mbaya zilikuwa haziishi, kuanzia matokeo ya kushangaza ya uchaguzi na kura ya maoni, hadi kwenye mashambulizi ya kigaidi yasiyo na idadi, kuongezeka kwa wakimbizi na mizozo mikubwa kama vile Syria, Yemen na Sudan Kusini. Pia inaeleza jinsi wakimbizi wanavyohujumiwa, huku mataifa yenye nguvu duniani yakishindwa kukabiliana na changamoto hiyo.

Katibu Mkuu wa Amnesty International, Salil Shetty amesema mwaka 2016 ulikuwa mbaya zaidi kuwahi kushuhudiwa katika rekodi za haki za binaadamu. Shetty amesema ukweli ni kwamba mwaka wa 2017 unaanza huku kukiwa na hofu na bila ya kuwa na uhakika kuhusu mustakabali wake. Amesema ripoti hiyo imebainisha kuwa moja ya tatizo kubwa la mwaka 2016, lilikuwa ni kuongezeka kwa matamshi ya chuki kwenye maeneo mengi ya Ulaya na Marekani na kuongezeka kwa hofu zaidi hadi kufikia kiwango ambacho hakijawahi kushuhudiwa tangu miaka ya 1930.

Südsudan Juba SPLA-IO Soldaten
Waasi wa Sudan KusiniPicha: picture-alliance/AP Photo/J. Patinkin

''Ulikuwa mwaka ambao sumu ya ubaguzi wa kisiasa ya ''sisi dhidi ya wao'' ilishika kasi duniani kote. Tulishuhudia kuongezeka siasa za woga na chuki. Wanasiasa duniani walizigawa jamii, waliwahujumu wachache, wahamiaji na wakimbizi. Na matokeo ya haya yote yanasababisha ukiukwaji wa haki za binaadamu,'' amesema Shetty

Ripoti hiyo ya mwaka imehusisha utafiti kuhusu ukiukwaji mkubwa wa haki za binaadamu kwenye nchi 159, ambapo 23 kati ya hizo pia zilihusika na uhalifu wa kivita, ikiwemo Sudan Kusini, Myanmar na Ufilipino. Shetty anasema cha kushangaza miongoni mwa nchi 159 zilizokiuka haki za binaadamu, ziko zile ambazo zinaongoza kupigia debe demokrasia kama vile Ufaransa, Uingereza na Marekani.

Trump ashutumiwa kuhusu wakimbizi

Ripoti ya Amnesty International imemshutumu Rais wa Marekani, Donald Trump pamoja na viongozi wengine wa dunia wakiwemo wa Hungary, Uturuki na Ufilipino, katika kile ilichosema kuwatumia vibaya wakimbizi kwa maslahi yao kisiasa, badala ya kutafuta kiini kilichosababisha wakimbizi hao wayakimbie mataifa yao.

Tirana Hassan
Mkurugenzi anayeshughulikia mizozo Amnesty International, Tirana HassanPicha: Amnesty International

Mkurugenzi wa kushughulikia mizozo wa Amnesty International, Tirana Hassan amesema sio kweli kwamba eneo moja la dunia limekuwa bora au limefanya vibaya zaidi ya jingine, bali mwaka 2016 umekuwa ni mwaka uliokiuka haki za binaadamu duniani kote, hali inayopaswa kukomeshwa mara moja.

Hassan ameiambia DW kwamba kilicho hatari zaidi lugha ya ''sisi dhidi ya wao'' ambayo imepata umaarufu mkubwa imechochea kuongezeka kwa siasa kali za kizalendo, huku mbinu kama hizo zikiwa zinawalenga zaidi wakimbizi na wahamiaji. Hassan amesema mwaka 2017 utakuwa ni mwaka wa kutoa wito kwa jumuiya ya kimataifa, serikali na wanasiasa kuchukua hatua na kuanza kuziweka mbele haki za binaadamu.

Hata hivyo, ripoti hiyo imesema kuwa mwaka 2017 uwe wa kupigania haki za binaadamu kwani maeneo ya mapambano yako kila sehemu na kila mmoja anaweza kuwa mwanaharakati wa haki za binaadamu. Aidha, shirika la Amnesty International limesema watu ambao tayari wanapigania kuzilinda haki za binaadamu, wanahitaji kuungwa mkono.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/AFP, RTR, DW http://bit.ly/2kXwtpg
Mhariri: Yusra Buwayhid