1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Amri ya kutotembea ovyo yawekwa katika jimbo la Diyala nchini Iraq.

Kitojo, Sekione12 Agosti 2008

Maafisa nchini Iraq wameweka amri ya kutotembea usiku katika mji mkuu wa jimbo la Diyala, Baquba baada ya gavana wa jimbo hilo kunusurika kuuwawa.

https://p.dw.com/p/Evgi
Kazi na dawa ,wanajeshi wa Marekani wakipata lepe la usingizi baada ya kazi ya kuwasaka wapiganaji nchini Iraq.Picha: AP





Maafisa nchini Iraq leo wameweka amri ya kutotembea ovyo katika mji mkuu wa jimbo lenye matatizo la Diyala , baada ya gavana wa jimbo hilo kunusurika katika shambulio la kujitoa muhanga katika msafara wa magari.




Watu wawili wameuwawa na wengine 12 wamejeruhiwa wakati mtu mmoja alijilipua karibu na msafara wa magari yaliyokuwa yakimsindikiza gavana wa jimbo la Diyala Raad Rasheed katika mji mkuu wa jimbo hilo Baquba, kilometa 65 kaskazini mashariki ya Baghdad.

Rasheed yuko salama. Rasheed ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa anashutumu vikali shambulio hilo na si mara ya kwanza kwa jaribio kama hilo dhidi ya maisha yake.

Televisheni ya taifa ya Iraqiya imesema kuwa amri hiyo ya kutotembea ovyo imeamriwa katikati tu ya mji kuanzia mchana leo Jumanne hadi Jumatano asubuhi.

Jimbo la Diyala limekumbwa na matukio kadha ikiwa ni msako mkubwa wa wiki mbili uliofanywa na majeshi ya Marekani yakisaidiwa na yale ya Iraq dhidi ya kundi la madhehebu ya Sunni linalounga mkono al-Qaeda pamoja na wapiganaji wengine, ambao hutumia mbinu ya mashambulizi ya kujitoa muhanga.

Shambulio la leo Jumanne la kujitoa muhanga , halitayumbisha juhudi za kuendelea na njia yetu ya kurejesha usalama kwa kupitia operesheni iitwayo dalili njema, Rasheed amesema.

Wakati kiwango cha ghasia kimeshuka nchini Iraq na kufikia kiwango ambacho hakijaonekana tangu mwaka 2004, jimbo hilo lenye mchanganyiko wa makabila na madhehebu ya dini linaonekana kuwa ni moja kati ya maeneo yaliyobaki ya maficho ya kundi la al-Qaeda.

Mashambulizi mengi ya hivi karibuni katika jimbo hilo yamefanywa na wanawake waliojitoa muhanga, mbinu ambayo imetumiwa sana na kundi la al-Qaeda mwaka huu.

Majeshi ya Iraq, yakisaidiwa na wanajeshi wa Marekani na helikopta yamefanya msako mwezi uliopita katika jimbo la Diyala, wakipekua nyumba, kukamata silaha na kuwakamata watu kadha. Polisi wamesema kuwa kiasi cha watu 370 wamekamatwa hadi sasa.

Wakati huo huo serikali ya Iraq imesema jana kuwa inasitisha kwa muda wa siku chache operesheni hiyo ili kuruhusu wapiganaji wajisalimishe. Lakini meja generali Mark Hertling, ambaye anaongoza majeshi ya Marekani katika eneo la kaskazini mwa Iraq, amesema kuwa wanajeshi wa Marekani wataendelea na operesheni hiyo. Hertling amewaambia waandishi wa habari jana Jumatatu kuwa msako huo wa kuleta usalama katika jimbo la Diyala katika muda wa mwaka mmoja umesababisha kukimbia kwa wapiganaji ambao amewaeleza kuwa kimsingi ni wapiganaji wazalendo ama makundi ya wahalifu kuliko wapiganaji wa kigeni kutoka katika miji ya jimbo la Diyala na kwenda sehemu nyingine nchini humo.

Ni muhimu sasa kuwakamata ama kuwauwa magaidi sugu ambao wanaishi hivi sasa ndani ya nchi hii, amesema generali huyo wa Marekani.



►◄