1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ANC katika hatua za mwisho kumuondoa Zuma

Lilian Mtono
12 Februari 2018

Viongozi wakuu wa chama tawala nchini Afrika Kusini - cha African National Congress, ANC wanakutana hii leo kwa kile kinachotajwa kuwa ni "kumalizia" hatua za kumuondoa rais wa taifa hilo Jacob Zuma.

https://p.dw.com/p/2sVPc
Südafrika Präsident Jacob Zuma & Vize-Präsident Cyril Ramaphosa
Picha: Reuters/GCIS

Viongozi wakuu wa chama tawala nchini Afrika Kusini - cha African National Congress, ANC wanakutana hii leo kwa kile kinachotajwa kuwa ni "kumalizia" hatua za kumuondoa rais wa taifa hilo Jacob Zuma baada ya kiongozi wake Cyril Ramaphosa kuahidi kuutamatisha mzozo huo.

Ramaphosa alisema katika mkutano wa chama cha ANC mjini Cape town jana Jumapili kwamba alitaka kubadilisha kile alichokiita "kipindi kigumu, mgawanyiko na kutoelewana, na kuleta mwanzo mpya kwa chama hicho".

Ramaphosa alisema, huku akishangiliwa kwa makofi kwamba anafahamu umma unataka suala hilo kufikia tamati, akiapa kupambana na rushwa iliyoharibu sifa ya serikali ya rais Jacob Zuma.

Zuma ameendelea kung'ang'ania madarakani baada ya kukataa ombi kutoka maafisa waandamaizi wa chama chake la kumtaka ajiuzulu mnamo wiki iliyopita.

Kamati kuu ambayo ina nguvu zaidi kwenye chama hicho inaweza kumtaka kuachia wadhifa wake, ingawa hawajibiki kwa namna yoyote kikatiba kuheshimu agizo la kamati hiyo.

BG Pierre Cardin | 95. Geburtstag
Ramaphosa alizungumza hayo kwenye kumbukumbu ya miaka 28 ya tangu kuachiwa huru kutoka gerezani, Nelson Mandela.Picha: picture alliance/AP Images/M. Hutchings

Ramaphosa awahakikishia raia kutekeleza mahitaji yao.

Ramaphosa alisema watafanya linalowezekana kuhakikisha suala hilo linafikia mwisho lakini kwa maslahi ya umma. Alisema, kamati kuu ya ANC itakutana hii leo kujadili suala hili, na kwa kuwa umma unataka kuhitimishwa kwa suala hilo, ndicho kile kamati hiyo itakifanya.

Litha Madita, ambaye ni mtumishi wa shirika moja lisilo la kiserikali mjini Cape Town, ameikaribisha taarifa ya kikao hicho cha kamati tendaji. Hata hivyo alisema wanatakiwa kumuheshimu Zuma kama kiongozi wa zamani wa ANC. Ni muhimu ili kuepusha taifa hilo lisiingie kwenye mzozo, alisema Litha.

Kipindi cha uongozi wa Zuma kiligubikwa na kashfa za rushwa, ukuaji hafifu wa uchumi na rekodi mbaya ya ukosefu wa ajira, ambayo kwa pamoja yameibua ghadhabu kubwa miongoni mwa raia.

Mkwamo kuhusu kuondoka Zuma umeliacha taifa hilo lililoendelea zaidi kiuchumi barani Afrika katika hali ya sintofahamu, huku baadhi ya shughuli za umma zikifutwa mnamo wiki iliyopita, ikiwa ni pamoja na hotuba ya hali ya taifa iliyotarajiwa kutolewa siku ya Alhamisi bungeni. 

Wirtschaft in Afrika
Afrika Kusini ni taifa lilikua zaidi kiuchumi barani Afrika, lakini ukuaji wake umeshuka katika enzi ya utawala wa Jacob ZumaPicha: AP

Vyama vya upinzani wiki iliyopita vilitishia kusababisha kile vilichokiita mkwamo katika huduma, ili kujibu hatua ya Zuma ya kukataa kujiuzulu, ingawa haikuwa dhahiri iwapo hili litafanyika.  

Mkutano wa hadhara wa jana ulikuwa sehemu ya maadhimisho ya ANC ya miaka 100 tangu kuzaliwa kwa kiongozi wake wa awali, Nelson Mandela, pamoja na jitihada zinazochukuliwa na Ramaphosa za kujaribu kurejesha sifa ya chama hicho, wakati taifa hilo likielekea kwenye uchaguzi mkuu mwakani. 

Ramaphosa alizungumza hayo katika siku ya kumbukumbu ya miaka 28 ya baada ya Mandela kuachiwa huru toka gerezani. 

Profesa wa siasa Mcebisi Ndletyana ameliambia shirika la habari la AFP kwamba hata kama ANC itaamua hii leo Zuma ajiuzulu, bado anaweza kukataa kwa kuwa hawana mamlaka ya kisheria. Upinzani wanataka kupigwa kwa kura ya kutokuwa na imani nae. 

ANC kimesisitiza kwamba hakutakuwa na ucheleweshaji wa bajeti, inayotarajiwa kusomwa Februari 21. Zuma hajazungumza hadharani tangu alipoombwa kujiuzulu na maafisa waandamizi wa ANC Februari 4 mwaka huu.

Mwandishi: Lilian Mtono.
Mhariri: Iddi Ssessanga