1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Anelka '' achekeshwa'' na marufuku aliyopewa

Nina Markgraf18 Agosti 2010

Mshambulizi wa Ufaransa, Nicolas Anelka ameudhihaki uamuzi wa kumpiga marufuku asishiriki katika mechi 18, hukumu aliyopewa kufuatia sakata ya timu ya Ufaransa katika michuano ya Kombe la dunia

https://p.dw.com/p/OqS3
Nicolas Anelka, akiwa mazoezini na timu ya Ufaransa.Picha: AP

Anelka ambaye anasakata kabumbu, katika klabu ya Chelsea ya Uingereza alisema amechekeshwa sana na hatua ya tume hiyo ya spoti kumpiga kalamu kutoichezea timu ya taifa kwa miezi kumi na nane, baada ya kumtolea kocha Raymond Domenech maneno makali wakati wa mashindano yaliopita ya fainali za kombe la dunia

Lile jinamizi la mambo kuwaendea sege mnege, timu ya Les Blues ya Ufaransa katika michuano ya kombe la dunia, sasa limeanza kuwaandama wachezaji nyota wa timu hiyo.

Raymond Domenech und Nicolas Anelka
Raymond Domenech, kulia Nicolas Anelka.Picha: AP

Nicolas Anelka ambaye aligonga vichwa vya habari kwa kutimuliwa kutoka michuano hiyo, baada ya ugomvi na kocha wake Raymond Domenech, sasa amejikuta tena pabayani baada ya tume iliyopewa jukumu la kuchunguza nini kilichokwenda mrama, kutoa maamuzi.

Adhabu, Anelka kupewa marufuku ya miezi kumi na nane kutoichezea timu ya taifa. Lakini Anelka ambaye anachezea timu ya Chelsea nchini Uingereza alipokea uamuzi huo kwa kejeli kubwa.

'' Kwa muujibu wangu, maamuzi ya tume hii ilikuwa ni mchezo mtupu na njama ya kuficha ukweli.'' Alisema Anelka.

Anelka aliongeza kusema kwamba tayari alikuwa ametangaza kwamba hatoichezea tena timu ya Ufaransa, baada ya kutimuliwa katika kombe la dunia, kwa hivyo uamuzi wa tume hiyo ya nidhamu ya chama cha kandanda cha Ufaransa haukuwa na maana yeyote.

Mbali na Anelka- wengine waliopewa adhabu ni Nahodha Patrice Evra , aliyefungiwa kuichezea Ufaransa kwa mechi tano, Frank Ribery akapewa marufuku ya mechi tatu na mchezaji wa Lyon wa kiungo cha Kati Jeremy Toulalan mechi moja.

Karl Heinz Rummenigge Franck Ribery Louis van Gaal Arjen_RobbenDiego_Contento FC Bayern Muenchen Empfang Double Feier NO FLASH
Frank Ribery pia apewa marufuku ya mechi tano.Picha: AP

Tofauti na malumbano katika timu ya Ufaransa yalijitokeza hadharani katika mechi yao ya pili, dhidi ya Mexico katika muda wa mapumziko. Anelka anasemekana alimtolea maneno makali kocha Raymond Domenech, baada ya kocha huyo kukosoa uchezaji wake. Mexico iliicharaza Ufaransa mabao 2-0 baadaye na ikawa ndio mwisho wa safari ya Le Blues Afrika Kusini.

Sakata hii ilipochapishwa katika vyombo vya habari, Anelka alitimuliwa kutoka kambi ya Ufaransa, Afrika Kusini, hatua iliyowasha moto zaidi, pale timu ya Ufaransa ilipofanya mgomo wa siku moja.

Hapa Ujerumani, timu ya Werder Bremen leo usiku inaingia uwanjani , dhidi ya Sampdoria kujaribu kufuzu kwa kombe la mabingwa barani Ulaya- Champions League bila ya stadi wao Mesut Ozil. Ozil ameihama Bremen na kujiunga na Real Madrid. Ozil alikuwa mchezaji nyota wa timu ya Ujerumani katika michuano ya Kombe la dunia.

Mwandishi: Munira Muhammad/AFPE

Mhariri: Abdul-Rahman