1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel asema ana wasiwasi na idadi ya mashabiki viwanjani

Saleh Mwanamilongo
2 Julai 2021

Kansela Angela Merkel amefanya mazungumzo na Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson. Merkel amesema anataka kuona nchi hizo mbili zinashirikiana kwa karibu.

https://p.dw.com/p/3vxSI
London | Angela Merkel bei Boris Johnson
Picha: Stefan Rousseau/PA/picture alliance

Katika mkutano wao, Merkel na Johnson wamegusia mipango ya usafiri baina ya Ujerumani na Uingereza wakati huu wa janga la Covid-19.

Merkel amesema wasafiri wa Uingereza ambao tayari wamechomwa dozi mbili ya chanjo wataruhusiwa kuingia nchini Ujerumani bila ulazima wa kukaa karantini.

''Tutafuata maelekezo ya kisayansi''

Aidha, Merkel amesema ana hofu juu ya hatua ya shirikisho la kandanda barani ulaya UEFA kuruhusu mashabiki wengi kuhudhuria mechi za mataifa ya Ulaya zinazoendelea za Euro 2020 viwanjani, akitahadharisha kuwa hatua hiyo huenda ikaongeza maambukizo ya virusi vya Corona.

Hata hivyo Waziri Mkuu wa Uingereza Boris Johnson amesema hadhamiri kupunguza idadi ya mashabiki kwenye mechi zilizosalia za Euro ambazo zitachezwa mjini London. Kwenye mechi ya nusu fainali inayotarajiwa kuchezwa katika uwanja wa Wembley, takriban mashabiki elfu sitini wanatarajiwa kuhudhuria.

 ''Bila shaka tutafuata maelekezo na ushauri wa wakisanyansi, ikiwa tutapewa mwelekezo huo. Lakini kwa sasa msimamo ni wazi hapa Uingereza, ambao ni kufuatialia kwa makini na kupima kila mtu anaye kwenda huko'',alisema Johnson.

Ushirikiano wa kiuchumi na kiutamaduni

Merkel amesema anataka kuona nchi hizo mbili zinashirikiana kwa karibu kuhusu maswala ya uchumi, nishati na utamaduni.
Merkel amesema anataka kuona nchi hizo mbili zinashirikiana kwa karibu kuhusu maswala ya uchumi, nishati na utamaduni.Picha: Patrick Semansky/AP Photo/picture alliance

Mbali na swala la Corona ,viongozi hao pia wamejadiliana juu ya masuala kadhaa ikiwemo kuanzia kufanya mkutano wa pamoja wa kila mwaka wa baraza la mawaziri la nchi hizo mbili.

Johnson amempongeza Merkel kuhusu utawala wake kama Kansela wa Ujerumani, na kusema uhusiano kati ya Uingereza na Ujerumani umeimarishwa tena.

Kansela wa Ujerumani alipendekeza kuweko na suluhisho la dhati baina ya Uingereza na Umoja wa Ulaya kufuatia mzozo wa mpakani. Merkel amewambia waandishi habari kwamba anaamini kuweko na suluhisho kuhusu tofauti hizo.

Ziara hiyo ya Merkel imekuja baada ya Uingereza na Umoja wa Ulaya kukubaliana juu ya kipindi cha mpito cha miezi mitatu kwa ajili ya kanuni za kuagizwa kwa nyama kutoka Ireland ya kaskazini.

Mwezi uliopita, Umoja wa Ulaya uliionya Uingereza dhidi ya vitendo zaidi vya upande mmoja ambavyo vinakiuka itifaki ya makubaliano ya Brexit kuhusu Ireland ya Kaskazini.

Merkel kuhutubia baraza la mawaziri la Uingereza

Ofisi ya Waziri Mkuu huyo wa Uingereza imesema Merkel atakuwa kiongozi wa kwanza wa kigeni kulihutubia baraza la mawaziri la Uingereza tangu rais wa zamani wa Marekani, Bill Clinton, alipohutubia baraza la mawaziri mwaka 1997 kwa mwaliko wa waziri mkuu wa wakati huo, Tony Blair.