1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ANKARA:Uturuki yatisha kushambulia eneo la mpaka na Iraq

25 Oktoba 2007
https://p.dw.com/p/C7Ck

Viongozi wa Uturuki wanashikilia kuwa huenda wakashambulia eneo la mpaka na Iraq ili kuwafurusha waasi wa PKK baada ya ghasia mpya kuripotiwa.Saa chache kabla ya ujumbe wa ngazi za juu wa serikali ya Iraq kuwasili mjini Ankara Rais wa Uturuki Abdula Gul anaonya kuwa nchi yake imechoshwa na tatizo hilo huku Waziri Mkuu Recep Tayyip Erdogan akiongeza kuwa kauli ya Marekani ya kujizua haina msingi.Wiki jana bunge la Uturuki liliidhinisha serikali kuishambulia kijeshi eneo la kaskazini mwa Iraq ili kuwafurusha waasi wa PKK walio na kambi zao katika eneo hilo la milima mingi.Marekani kwa upande wake inasisitiza kujizua kwa upande wa Uturuki huku Uturuki yenyewe ikishikilia kuwa marekani pamoja na Iraq kushambulia ngome za waasi hao.

Kundi la waasi wa PKK limekuwa likipigania uhuru wa kujitenga tangu mwaka ’84 na lina ngome zake katika eneo la kaskazini mwa Iraq.Uturuki inadai kuwa waasi hao wanafanya mashambulizi dhidi ya wanajeshi wake wakiwa eneo hilo.

Waziri Mkuu Erdogan anasisitiza kuwa uamuzi wa mwisho kuhusu uvamizi wa eneo la mpakani ni wao na wala si wa Marekani.

Maafisa wa Iraq hawajatoa maelezo yoyote kuhusu mazungumzo yatakayofanyika punde ujumbe wa Iraq utakapowasili mjini Ankara.Mapema wiki hii Waziri Mkuu wa Iraq Nuri al Maliki aliagiza kufungwa kwa afisi za PKK nchini mwake ili kujaribu kupoza moto madai ya Uturuki.Uongozi wa Kikurdi katika eneo hilo unasisitiza kuwa hauna taarifa zozote kuhusu afisi hizo hivyo basi hazihitajiki kufungwa.