1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Antonio Guterres kuwa Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa

Caro Robi
6 Oktoba 2016

Waziri mkuu wa zamani wa Ureno Antonio Guterres anatarajiwa kutangazwa rasmi kuwa Katibu mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa baada ya kupigiwa kura nyingi kuliko wagombea wengine katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

https://p.dw.com/p/2QvIa
Antonio Guterres
Picha: picture-alliance/dpa/J.-Ch. Bott

Baada ya duru ya sita ya kura isiyo rasmi katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa siku ya Jumatano, Antonio Guterres anatarajiwa kutangazwa rasmi Alhamisi kuwa Katibu mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa.

Guterres ambaye alikuwa mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu wakimbizi UNHCR kwa miaka kumi iliyopita, alipata kura 13 kati ya 15 za nchi wanachama wa baraza hilo la usalama huku nchi zote tano wanchama wa kudumu walio na kura ya turufu wakimuunga mkono.

Balozi wa Urusi katika Umoja wa Mataifa Vitaly Churkin alitangaza kuwa ni bayana kuwa Guterres ndiye atachukua wadhifa unaoshilikiwa na Ban Ki Moon mwenye umri wa miaka 72, waziri wa zamani wa mambo ya nje wa Korea Kusini ambaye anakamilisha mihula yake miwili ya miaka kumi katika wadhifa huo.

Kura ya mwisho ya kumuidhinisha katibu mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa itapigwa hii leo. Guterres mwenye umri wa miaka 67 ameahidi kuuboresha Umoja wa Mataifa, kuimarisha juhudi za kulinda amani na kulinda haki za binadamu.

European Parliament in Strasbourg Ban Ki Moon
Katibu mkuu wa sasa wa Umoja wa Mataifa Ban Ki MoonPicha: picture-alliance/dpa/P. Seeger

Guterres ambaye alikuwa waziri mkuu wa Ureno kuanzia mwaka 1995 hadi 2002, amekuwa akiongoza katika kura zisizo rasmi za kumchagua katibu mkuu mpya tangu Julai lakini uamuzi wa jana wa baraza la usalama la Umoja wa Mataifa karibu kwa kauli moja kumchagua mwanasiasa huyo wa kisosholisti haukutarajiwa.

Atakuwa kiongozi wa kwanza wa nchi kuwa mkuu wa Umoja wa Mataifa, wadhifa ambao umeshikiliwa na mawaziri kadhaa wa mambo ya nje ambao walikuwa wakichaguliwa katika vikao vya faragha vya Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa. Kipindi hiki; zoezi hilo liliendeshwa kwa uwazi zaidi na wagombea waliruhusiwa kuhudhuria vikao ili kujinadi mbele ya mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa.

Akishaidhinishwa na baraza la usalama, Guterres atawasilishwa kwa mkutano mkuu wa Umoja wa Mataifa ili kuidhinishwa rasmi kuwa katibu mkuu wa tisa wa Umoja huo. Katibu mkuu mpya ataanza kutekeleza majukumu yake tarehe 1 Januari kwa kipindi cha miaka mitano ijayo.

USA Antonio Guterres in New York
Katibu mkuu mtarajiwa wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Getty Images/AFP/K. Betancur

Balozi wa Ufaransa Francois Delatter amesema kumchagua Guterres anayezungumza kiingereza, kifaransa, kihispani na kireno ni habari njema kwa Umoja wa Matifa huku balozi wa Uingereza Matthew Rycroft akisema atakauwa katibu mkuu shupavu.

Katika kinyang'anyiro hicho cha kumchagua katibu mkuu mpya wa Umoja wa Mataifa kumekuwa na wito wa kuchaguliwa kwa mara ya kwanza mwanamke. Kulikuwa na wanawake saba waliogombea wadhifa huo. Pia kulikuwa na wito wa kuchaguliwa mtu kutoka Ulaya mashariki, eneo ambalo mpaka sasa halijawakilishwa katika wadhifa huo kwa miaka 70 iliyopita.

Mwandishi: Caro Robi/afp/Reuters

Mhariri:Josephat Charo