1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ariel Sharon: Raia kutoa heshima zao Jumapili

12 Januari 2014

Rais Barack Obama wa Marekani amemuenzi jana Jumamosi(11.01.2014) waziri mkuu wa zamani wa Israel Ariel Sharon na kusema alikuwa na nia thabiti kwa taifa lake.

https://p.dw.com/p/1ApEB
Israels ehemaliger Ministerpräsident Ariel Sharon
Marehemu Ariel SharonPicha: Gali Tibbon/AFP/Getty Images

Makamu wa rais wa Marekani Joe Biden ataongoza ujumbe wa marekani katika ibada ya mazishi mjini Jerusalem.

Mwanajeshi huyo mzalendo wa Israel ambaye baadaye aliamua kuingia katika siasa amefariki siku ya Jumamosi(11-01.2014), miaka minane baada ya kupata kiharusi ugonjwa ambao ulisababisha kuzimia na kuwa hajitambui tena. Alikuwa na umri wa miaka 85.

Kunst Installation Ariel Scharon
Ariel Sharon akiwa mahututiPicha: picture-alliance/dpa

"Tunajiunga na watu wa Israel katika kutoa heshima kwa kujitoa kuitumikia nchi yake," Obama amesema katika taarifa ya maandishi. Obama pia ametumia tukio hilo kusisitiza kile kinachoelezwa kuwa ni "nia isiyoyumba ya usalama kwa Israel."

"Tunaendelea kupambana kutafuta amani ya kudumu na usalama kwa watu wa Israel," Obama amesema.

Brarack Obama Jahrespressekonferenz
Rais Barack ObamaPicha: picture-alliance/dpa

Biden amesema anamatumaini ya kupata fursa ya "kutoa heshima zake kwa mtu huyo na kutoa shukurani kwa ushirikiano usio yumba kati ya Marekani na Israel."

Rambi rambi

Rambi rambi zimemiminika kutoka kwa waziri wa mambo ya kigeni John Kerry, marais wa zamani Bill Clinton na George W. Bush na viongozi wengine wa Marekani.

Kerry amesema hatasahau siku alipokutana na "mtu huyu mkubwa kama dubu" baada ya sharon kuwa waziri mkuu.

"Katika miaka yake ya mwisho akiwa waziri mkuu , aliwashangaza wengi katika utafutaji wa amani na leo, tunakiri, kama alivyofanya , kuwa Israel ni lazima iwe imara kuweza kufikia amani, na kwamba amani pia itaifanya Israel kuwa na nguvu," amesema Kerry.

Tangu alipokuwa mwanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Marekani mwaka jana, Kerry amefanya ziara mara kumi katika mashariki ya kati, ikiwa ni pamoja na mwezi huu, katika matumaini ya kupatanisha amani ya kudumu kati ya Waisrael na Wapalestina.

Ariel Sharon und Bill Clinton
Bill Clinton akiwa na Sharon(kushoto)Picha: picture alliance / AP Photo

"Ilikuwa ni heshima kubwa kufanyakazi pamoja naye, kubishana nae, na kumuangalia kila mara akijaribu kutafuta njia sahihi kwa nchi yake," ameongeza Clinton.

Bush, ambaye ameshika uongozi wakati mmoja sambamba na Sharon, amemuita kuwa ni rafiki na "mtu jasiri."

Shujaa wa taifa la Kiyahudi

"Alikuwa shujaa kwa miaka kadha na mshirika katika kutafuta usalama wa eneo hilo takatifu na mashariki ya kati tulivu na ya amani, " Bush amesema.

Kiongozi wa kundi la maseneta wa chama cha Republican Mitch McConnell amesema Israel " imepoteza kijana wake shupavu na Marekani imepoteza rafiki."

Israel inatoa heshima zake za mwisho leo Jumapili(12.01.2014) kwa Ariel Sharon , ambaye wengine wanampenda na wengine wanashutumu kwa mtindo wake wa kutojali na wa ukaidi , na ambaye kifo chake kimeleza simanzi hata baada ya miaka minane ya kuishi bila kujitambua akiwa amezimia.

George Bush Mahmud Abbas und Ariel Sharon
George W. Bush (katikati)akiwa na Ariel Sharon (kulia)na Mahmud Abbas(kushoto)Picha: picture-alliance/dpa

Anashangiriwa kwamba ni shujaa wa vita kwa baadhi, na anatambulika kama mwanasiasa mwenye kuchukua hatua kwa wengine na anachukiwa na mahasimu wake kwa kuitwa mhalifu mwenye kiu ya damu tu.

Mwili wa Sharon utawekwa katika jengo la bunge la Israel Knesset leo Jumapili(12.01.2014) ili watu waweze kutoa heshima zao.

Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe / ape

Mhariri: Sudi Mnette