Arsenal kujipima nguvu na Palace
10 Aprili 2017Ligi ya England , Premier League , Arsenal London ina kibarua dhidi ya Crystal Palece leo jioni (10.04.2017) na mtihani mkubwa kwa kocha wao Aserne Wenger wakati timu hiyo iliyoko katika nafasi ya 6 na pointi 54 ikiwania kurejea katika timu bora nne na kufuzu kucheza katika Champions League msimu ujao. Mafanikio ya Arsenal leo yatatuliza mzuka wa mashabiki ambao wanataka kocha huyo aachie ngazi baada ya kupata matokeo yasiyoridhisha msimu huu katika ligi ya nyumbani na pia michuano ya kimataifa.
Jana Jumapili (09.04.2017)Everton ilichafua rekodi ya kocha Craig Schakespeare wa Leicester City kwa kuirarua timu hiyo kwa mabao 4-2. Leicester ilishinda michezo mitano mfululizo ya ligi baada ya kumfuta kazi kocha aliyeitawaza timu hiyo bingwa wa Premier League kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo , Februari mwaka huu kufuatia matokeo mabaya ambayo yaliiweka timu hiyo karibu na kushuka daraja.
Sunderland ilishindwa kuhimili vishindo vya Manchester United kwa kukubali mabao 3-0, Chelsea ikaimarisha nafasi yake ya uongozi kwa ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Bournemouth. Man City ikapata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Hull City na Liverpool ikaimarisha nafasi yake ya kucheza michuano ya Champions League msimu ujao kwa ushindi wa mabao 2-1 dhidi ya Stoke City.
La Liga
Real Madrid inakaribia kutawazwa mabingwa wa La Liga kwa mara ya kwanza katika muda wa miaka mitano baada ya kutoka sare ya bao 1-1 na Atletico Madrid. Barcelona ilishangazwa na kipigo cha kushitua dhidi ya Malaga kwa mabao 2-0 na pia kadi nyekundu kwa nyota wao Neymar.
Edson Cavani alipachika wavuni mabao 2 na kutengeneza bao moja lingine wakati Paris Saint- Germain ikipata ushindi wa mabao 4-0 dhidi ya Guingmp na kuendelea na mbio za kuifukuzia Monaco katika ubingwa wa ligi ya Ufaransa .
Nice ambayo inatengana na PSG kwa pointi moja ikiwa katika nafasi ya tatu ilipata ushini wa mabo 2-1 dhidi ya Lille siku ya Ijumaa , wakati bao la Radamel Falcao liliipa ushindi Monaco wa bao 1-0 dhidi ya Angers siku ya Jumamosi.
Ligi ya mabingwa barani Ulaya , Champions League inaingia katika hatua yake ya robo fainali kesho Jumanne na Jumatano katika mkondo wa kwanza , ambapo Borussia Dortmund ya Ujerumani inaikaribisha Monaco ya Ufaransa katika uwanja wa Signal Iduna Park mjini Dortmund, na ni timu hizi zinazoelezwa kuwa viwanda vya vijana chipukizi wanaotengenezwa kuwa nyota barani Ulaya.
FC Barcelona nao watakuwa uwanjani kesho , wakipambana na Juventus Turin ikiwa ni pambano linaloonekana kuwa marudio ya fainali ya msimu wa mwaka 2014 / 2015.
Kwa upande wa michuano ya kombe la shirikisho barani Afrika klabu ya soka ya Tanzania Young Africans ilifanikiwa kuiangusha Mouloudia Alger ya Algeria kwa bao 1-0 jana Jumapili , wakati TP Mazembe ya Jamhuri ya kidemokrasi ya Congo iliiangusha JS Kabylie ya Algeria kwa mabao 2-0. Enugu Rangers ya Nigeria itatoka sare ya mabao 2-2 na Zesco Utd ya Zambia. KCCA ya Uganda ikaiangusha Al Maery ya Misri kwa bao 1-0 . Rivers United ya Nigeria itapambana na Rayon Sport ya Rwanda Aprili 15.
Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe / APE
Mhariri:Iddi Ssessanga