1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Arsenal wapewa kipigo na Liverpool

Bruce Amani
28 Agosti 2017

Sio wakati mzuri wa kuwa shabiki wa Arsenal. Maana kote mitandaoni kuna kila aina ya gumzo, kuanzia kwa utani, hasira, vichekezo na hata maoni tofauti ya mashabiki wa kandanda kuhusiana na maangamizi yaliyotokea Anfield

https://p.dw.com/p/2izB3
Arsenal Coach Arsene Wenger
Picha: Reuters/H. McKay

Kocha wa Arsenal Arsene Wenger ameyaelezea matokeo yao ya jana kuwa "yasiyokubalika” baada ya kubumburushwa kwa kufungwa mabao manne kwa sifuri na Liverpool.

Wenger alisema kila kitu kilikwenda mrama. Kuanzia dakika ya kwanza hadi ya mwisho. Wachezaji hawakuwa sawa kimwili na kiakili na wakaadhibiwa.

Liverpool chini ya kocha Mjerumani Jurgen Klopp, ilicheza kwa kasi na kupata mabao kupitia Firmino, Sadio Mane, Mohammed Salah na Daniel Sturridge.

Matokeo hayo yameanzisha tena mjadala wa kuhusu mustakabali wa Wenger ambaye alisaini mkataba mpya wa miaka miwili licha ya shinikizo la msimu uliopita kutoka kwa baadhi ya mashabiki la kutaka ajiuzulu.

UK | Fußball | Crystal Palace vs Chelsea - Premier League -  Selhurst Park Stadium
Conte anasema kazi yake hufanyika uwanjaniPicha: picture-alliance/ZUMAPRESS/D. Klein

Tukitoka upande mwekundu wa London, tuelekee katika upande wa bluu wa London, ambapo…Antonio Conte amesema ataendelea kutekeleza majukumu yake katika klabu ya Chelsea hata kama hatapewa wachezaji wapya anaowataka kabla ya dirisha la usajili wa kufungwa rasmi Alhamisi.

Conte hajaweza kuficha hisia zake kuhusiana na ukosefu wa Chelsea kushindwa kuwasajili wachezaji nyota aliowatamani na ripoti mwishoni mwa wiki ziliashiria kuwa kocha huyo wa Blues angeamua kujiuzulu kama muda wa usajili wa wachezaji wapya ungemalizika bila sura mpya kujiunga na mabingwa hao. Chelsea waliwasajili msimu huu Alvaro Morata, Tiemoue Bakayoko na Antonio Rudiger.

"nadhani ujumbe wangu kwa mashabiki ni ule ule. Nimejitolea kuwaimarisha wachezaji wangu na timu yangu ya Chelsea". Mimi ni kocha, sio meneja, kazi yangu bora inafanyika uwanjani. Alisema Conte.

Chelsea walipata ushindi wa mabao mawili kwa sifuri dhidi ya Everton hapo jana, na Morata, mmoja wa wachezaji waliosajiliwa msimu huu alifunga bao la pili baada ya Cesc Fabregas kufunga bao la kwanza.

Mwandishi: Bruce Amani/AFP/Reuters
Mhariri: Abdulrahman