1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

ASEAN: China yaonya kuhusu vizingiti vya kibiashara

Daniel Gakuba
13 Septemba 2018

Kongamano la Kimataifa la Uchumi kwa kanda ya Asia Kusini (ASEAN) ambalo kwa siku tatu limekuwa likifanyika nchini Vietnam linahitimishwa leo, kwa miito ya kupinga vizuizi vinavyojitokeza katika biashara duniani.

https://p.dw.com/p/34nKb
Indonesien Weltwirtschaftsforum & ASEAN in Hanoi, Vietnam
Picha: Laily Rachev/Biro Pers Setpres

Akizungumza katika kongamano hilo linalofanyika mjini Hanoi, naibu waziri mkuu wa China Hu Chunhua ameonya kuhusu sera ya kulinda masoko ya ndani unaofanywa na baadhi ya nchi, akisema ni kitisho kwa ustawi wa kiuchumi duniani. Ingawa hakutaja kwa jina nchi zenye sera hiyo, inaaminika kuwa Hu alikuwa akiilenga Marekani na sera ya Rais Donald Trump ya ''Marekani Kwanza'', ambayo inasababisha mgongano wa kibiashara kati ya nchi hizo mbili zinazoongoza kwa uchumi mkubwa duniani.

''Mipango inayochukuliwa na baadhi ya nchi kivyake inahujumu utaratibu wa biashara ya kimataifa unaofuata sheria, na ni kitisho kikubwa kwa uchumi wa dunia. Tunapaswa kulaani wazi wazi wanaolinda masoko ya ndani kwa kujichukulia sheria mkononi, tuunge mkono ushirikiano wa mataifa na utandawazi, na uhuru katika biashara na uwekezaji.'' Amesema Hu.

Innere Mongolei Parteichef Kommunistische Partei Hu Chunhua
Hu Chunhua, Naibu Waziri Mkuu wa ChinaPicha: Getty Images

Suala la vizuizi vya kibiashara limepewa kipaumbele katika kongamano hilo, huku viongozi wa nchi za Asia Kusini wakipendekeza kupungua kwa vizingiti hivyo mnamo ambapo Marekani inaupa kisogo ukanda huo, chini ya utawala wa Rais Donald Trump.

Washirika wenye mtazamo sawia

Waziri Mkuu wa Singapore Lee Hsien Loong amesema ukanda wa Asia Kusini unafanyakazi na washirika wenye mawazo kama yao, kuimarisha mfumo wa biashara huria ya kimataifa, ambayo inazingatia kanuni zilizowekwa.

Mzozo wa kibiashara baina ya China na Marekani unafuatiliwa kwa karibu na nchi za Asia Kusini, kwa sababu baadhi ya nchi hizo ambazo uchumi wake unategemea mauzo ya nje zinaweza kunufaika na mzozo huo.

Kwa mfano, kupanda kwa gharama za uzalishaji nchini China kumevilazimisha baadhi ya viwanda kuhamia nchini Vietnam na Cambodia mbako bidhaa zinaweza kutengenezwa kwa gharama ya chini. Vile vile makampuni kadhaa ya China yanahamishia viwanda vyao katika nchi nyingine za kanda, yakikwepa vikwazo vya kiushuru ambavyo Rais Trump ameiwekea China.

Kuvuma kwa uchumi wa ASEAN -nguvu ya soda?

Vietnam World Economic Forum/ASEAN Aung San Suu Kyi
Aung San Suu Kyi, Kiongozi mwenye nguvu zaidi kisiasa nchini MyanmarPicha: Reuters/Kham

Hata hivyo mchambuzi wa uchumi wa Asia Kusini Rajiv Biswas anasema matumaini ya kuvuma kwa uchumi wa eneo hilo yanaweza kuwa ya muda mfupi, kwa sababu ukweli kwamba tegemeo lao kubwa ni biashara ya nje, unalifanya kuwa tete ikia vizingiti vya kiushuru vitaendelea kwa muda mrefu.

Mada kuu ya kongamano hili la Dunia la Uchumi kwa kanda ya Asia Kusini ni kujadili namna ya kushirikiana kukabiliana na kile kilichotajwa kuwa ''teknolojia ya kutibua hali ya mambo'' kama ile ya kuunda mashine na maroboti yanayoweza kufanya kazi badala ya wanadamu, ikitishia fursa za ajira katika mataifa yanayoinukia.

Kiongozi mwenye nguvu zaidi kisiasa nchini Myanmar Aung San Suu Kyi ambaye anashiriki katika kongamano hilo, akizungumzia mzozo unaoendelea nchini mwake, amesema akitazama nyuma anaamini kwamba serikali yake ingeweza kuushughulikia vyema zaidi mzozo wa Warohingya. Hali kadhalika ametetea kufungwa jela kwa waandishi wawili wa shirika la habari la Reuters hivi karibuni, akisema hawakulengwa kwa sababu ya kazi yao, bali kwa kuvunja sheria. Suu Kyi amesema waandishi hao wanao uhuru wa kukata rufaa.

Mwandishi. Daniel Gakuba/afpe, ape, dpae

Mhariri: Yusra Buwayhid