1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ashton Carter kuujadili mzozo wa Urusi na Ukraine

5 Juni 2015

Waziri wa ulinzi wa Marekani Ashton Carter ataongoza mkutano mjini Stuttgart utakaojadili masuala yanayoihusu Marekani barani Ulaya, na namna nchi hiyo inavyoshughulikia suala la Urusi kujiingiza katika mzozo wa Ukraine

https://p.dw.com/p/1Fbzx
Picha: Reuters/Y. Gripas

Carter atafanya mkutano na wanadiplomasia wa Marekani na makamanda wa kijeshi wa nchi hiyo kutoka kote barani Ulaya. Mkutano huo utaangazia masuala kadhaa yanayoikabili Marekani barani Ulaya lakini itatuama zaidi katika kutathmini jinsi Marekani imekuwa ikiichukulia Urusi kwa kipindi cha miezi kumi na nane iliyopita na kuunda mikakati kuhusu mzozo unaondelea kati ya Urusi na Ukraine.

Carter kujuzwa masuala ya kiusalama

Msemaji wa wizara ya ulinzi ya Marekani Brent Colburn amesema madhumuni ya mkutano huo ni kumfahamisha kwa kina Carter kuhusu masuala ya kiulinzi na kiusalama wakati akijiandaa kuhudhuria mkutano wake wa kwanza wa mawaziri wa nchi wanachama wa Jumuiya ya kujihami ya NATO mwishoni mwa mwezi huu.

Afisa wa ngazi ya juu wa wizara ya ulinzi wa Marekani amewaambia wanahabari kutakuwa na majadiliano kuhusu iwapo Marekani ilishughulikia ipasavyo kitendo cha Urusi kulichukua eneo la Ukraine la Crimea na kulifanya sehemu ya himaya yake, na hatua zinazoweza kuchukuliwa katika kuushughulikia vyema zaidi mzozo huo.

Vifaru vya jeshi la Ukraine vikishika doria katika jimbo la Donetsk
Vifaru vya jeshi la Ukraine vikishika doria katika jimbo la DonetskPicha: Getty Images/AFP/A. Stepanov

Marekani inatumai kuwa itawashawishi washirika wake barani Ulaya kuendelea kuiwekea vikwazo vya kiuchumi Urusi na kuendelea kuishinikiza nchi hiyo hadi suluhu la mzozo wa mashariki mwa Ukraine litakapopatikana.

Maafisa wa Marekani wamesema suala la kuipa silaha moja kwa moja Ukraine ni jambo ambalo linaendelea kutathiminiwa.Carter amenukuliwa katika kipindi cha nyuma akisema nguvu za kijeshi ni mojawapo tu ya sehemu ya mkakati wa kukabiliana na Urusi.

Carter anaamini kuwa vikwazo vya kiuchumi dhidi ya Urusi ndiyo shinikizo muhimu zaidi hivi sasa katika kuidhibiti nchi hiyo. Hata hivyo Marekani inazingatia kutuma makombora barani Ulaya kujibu madai kuwa Urusi inakiuka matumizi ya silaha za kinyuklia.

Urusi yadaiwa kufanya majaribio ya kinyuklia

Makombora hayo ambayo ni sehemu ya hatua za kiulinzi zinazozingatiwa na Marekani, yana uwezo wa kuziharibu mapema silaha za urusi. Inadaiwa Urusi imekuwa ikifanyia majaribio makombora ya kurushwa kutoka ardhini katika masafa ambayo hayaruhusiwi chini ya mkataba wa kudhibiti matumizi ya silaha za kinyuklia uliopitishwa mwaka 1987.

Viongozi wa nchi nane zenye nguvu zaidi za kiviwanda mwaka juzi
Viongozi wa nchi nane zenye nguvu zaidi za kiviwanda katika kipinid cha nyumaPicha: picture-alliance/dpa

Carter ameonya kuwa kukiukwa kwa mkataba huo kutasababisha majibu kutoka upande wa pili na kuibua uwezekano wa Marekani kuijibu kijeshi Urusi. Urusi hata hivyo imekanusha kuwa imekiuka makubaliano hayo na badala yake kuishutumu Marekani kwa kufanya hivyo.

Suala hilo la mzozo wa Ukraine pia linatarajiwa kuwa mojawapo ya mada kuu katika mkutano wa nchi saba zenye nguvu zaidi kiviwanda duniani, zinazounda kundi lijulikanalo kama G7, ambao utafanyika kuanzia Jumapili ijayo hapa Ujerumani.

Mwandishi: Caro Robi/dpa

Mhariri: Gakuba Daniel