1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Asilimia 14 ya waislamu hapa Ujerumani wanaunga mkono machafuko na uhasama dhidi ya demokrasia.

Josephat Charo21 Desemba 2007

Hayo kwa mujibu wa ripoti ya uchanguzi uliofanywa na wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani.

https://p.dw.com/p/CeyV
Waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani Wolfgang SchaeublePicha: AP

Takriban waislamu 2,000 walihojiwa kwa njia ya simu katika uchunguzi huo, idadi ambayo inaelezwa kuwa kubwa ikilinganishwa na watu waliohusishwa katika tafiti za aina hiyo zilizowahi kufanywa. Baadhi ya matokeo ya uchunguzi huo yanatisha lakini tofauti ni ndogo ikilinganishwa na maoni ya Wajerumani wenyewe.

Ongezeko la uwezekano wa itikadi kali ni jambo ambalo limekuwa likimsusua waziri wa mambo ya ndani wa Ujerumani, Wolfgang Schäble. Kufutia matokeo ya uchunguzi mpya uliofanywa, waziri Schäuble amerudia onyo lake na kutoa mwito kuwepo ushirikiano kati ya waislamu na wale wasio waislamu hapa nchini, ili kuondoa kitisho kinachozidi.

Ripoti hiyo ya kurasa 515 imetayarishwa na profesa Peter Wetzels na profesa Katrin Brettfeld wa chuo kikuu cha Hamburg. Miongoni mwa mambo mengine ripoti hiyo inaonyesha kuwa karibu asilimia 40 ya waislamu wote nchini Ujerumani, wana mawazo ya itikadi kali ya kidini. Matokeo hayo yanadhihirisha wazi dhahiri shahiri hofu ambayo waziri Wolfgang Schäuble amekuwa nayo kuhusu itikadi kali ya kiislamu. Uchunguzi huo umeonyesha waislamu wa Ujerumani hawana tofauti kubwa na watu wengine wanaoishi humu nchini ambao si waislamu.

Werner Schiffauer, mtaalamu wa elimu ya binadamu katika chuo kikuu cha Frankfurt an der Oder, ameonya wakati wa mahojiano yake na redio hii kwamba matokeo ya uchaguzi huo yanatakiwa yazingatiwe.

´Ipo haja ya kuutilia maanani uchunguzi huu. Inatakiwa ifahamike wazi kwamba waislamu na hata wale wasio waislamu wote kwa pamoja wanakabiliwa na tatizo. Katika makundi yote mawili kuna asilimia 14 ya mawazo ya kupinga demokrasia. Hiyo si idadi ndogo. Tunalazimika kwa pamoja kutafuta njia za kuyatatua matatizo yaliyopo na la muhimu juu ya yote, katika jamii ya waislamu tuwahusishe wale walio na itikadi kali.´

Profesa Peter Wetzels, mmoja wa watu walioiandika ripoti hiyo, pia ameonya juu ya kuwepo uangalifu isije ripoti hiyo ikanonekana ikipendekeza kuwa idadi kubwa ya waislamu hapa Ujerumani hawafuatilii maadili ya uislamu na hawaungani na wenzano kuipinga demokrasia. Aidha profesa Wetzels amekanusha madai kwamba wizara ya mambo ya ndani imekuwa na ushwawishi mkubwa katika utayarishaji wa ripoti hiyo.

´Hakukuwa na tume maalumu. Uchunguzi umefanywa kwa misingi ya utafiti tulioufanya hapo kabla kuhusu uhusiano kati ya dini na uhalifu. Wizara ya mambo ya ndani ya Ujerumani imedhamini mradi huu wa utafiti lakini haikutoa amri utafiti ufanywe. Wizara hiyo pia haijakuwa na usemi wowote kuhusiana na yaliyo katika ripoti ya uchunguzi huu.´

Profesa Wetzels amesema matokeo ya uchunguzi huo yanatoa picha ilivyo na yanaweza kutumiwa kuendeleza mdahalo na maridhiano.

´Mdahalo ambao tayari umeanza na unaozijumulisha pande mbalimbali za serikali ya Ujerumani, na unaoendelea hata katika majimbo, kwa maoni yangu ya mwisho kabisa, ni muhimu mno na hakuna chaguo lengine. Hakuna chaguo lengine mbali na mdahalo. Haina maana kwa sisi kujaribu kulikaripia tatizo linalosababishwa na kundi la watu wachache ambalo linavuruga umoja wa kundi hilo. Tukifanya hivyo tutakuwa tunaliongezea makali tatizo lenyewe.

Lengo kubwa la uchunguzi huo lilikuwa kutafuta ni kwa umbali gani misimamo ya waislamu wa hapa Ujerumani inavyoenea na katika misingi gani na hatimaye kujaribu kutafuta njia za kuzuia ubaguzi katika kuendeleza juhudi za kuwajumulisha raia wa kigeni hapa nchini.