1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Assad ni sehemu ya suluhisho asema Mistura

14 Februari 2015

Suluhisho lolote katika mapigano nchini Syria linapaswa kumuhusisha pia rais Bashar al-Assad , mjumbe maalum wa Umoja wa Mataifa nchini Syria amesema katika hatua ya kwanza ya Umoja wa Mataifa kukiri hilo.

https://p.dw.com/p/1Ebdr
Syrien UN-Gesandt Staffan de Mistura bei Baschar al-Assad in Damaskus
Mjumbe maalum wa UN Staffan de Mistura akizungumza na rais wa Syria Bashar al-AssadPicha: picture-alliance/dpa

"Rais Assad ni sehemu ya suluhisho," Staffan de Mistura ameuambia mkutano wa waandishi habari pamoja na waziri wa mambo ya kigeni wa Austria Sebastian Kurz mjini Vienna jana Ijumaa(13.02.2015).

"Nitajaribu kuendelea kuwa na majadiliano muhimu pamoja nae," de Mistura ameongeza, akidokeza kwamba "Suluhisho pekee ni la kisiasa."

Staffan de Mistura
Mjumbe maalum wa Umoja wa mataifa nchini Syria De MisturaPicha: Raveendran/AFP/GettyImages

Hii ni mara ya kwanza kwa mjumbe wa Umoja wa Mataifa nchini Syria kutamka wazi na kumtaja Assad kuwa sehemu ya suluhisho la amani baada ya miaka karibu minne ya mapigano kati ya majeshi ya serikali na waasi wanaotaka kuuangusha utawala wake.

Matamshi ya de Mistura yamesababisha shutuma kutoka kwa kundi la upinzani la muungano ya kitaifa pamoja na wanaharakati nchini Syria.

"Nafikiri de Mistura anajidanganya mwenyewe iwapo anafikiri kuwa Assad ni sehemu ya suluhisho," mwanachama wa kundi hilo la muungano wa kitaifa Samir Nashar ameliambia shirika la habari la AFP kwa simu kutoka Istanbul.

"Assad ni tatizo, na sio sehemu ya suluhisho."

Bashar al-Assad Syrien Präsident 4.12.
Rais Bashar al-AssadPicha: Reuters/Sana

Najib Ghadbian , mjumbe wa muungano wa kitaifa katika Umoja wa mataifa, ameueleza ukatili wa utawala wa Assad kuwa ndio chanzo cha mzozo huo.

Pia ameuonya muungano unaoongozwa na Marekani unaopambana na kundi la Dola la Kiislamu -- ambalo limekamata maeneo makubwa ya ardhi nchini Syria na Iraq-- kwamba juhudi zake zinaweza kushindwa hadi pale mataifa yenye nguvu duniani yatakapochukulia kwa dhati mpango ya amani wa syria.

"Tunakaribisha muungano huu lakini tunahitaji kuwa na mkakati maalum kusisitiza sababu ya msingi: Assad na ukatili wa Assad," amesema Ghadbian.

De Mistura, ambaye alikuwa mjini Damascus wiki hii kukutana na Assad, anatarajiwa kutoa ripoti yake kuhusu ujumbe wake katika baraza la usalama la Umoja wa Mataifa Februari 17.

Syrien Armee
Mji wa Homs katika eneo la soko la Hamidiya ulivyoharibiwa na majeshi ya serikaliPicha: picture-alliance/dpa

Kundi la ISIS ndilo litafaidika na ghasia hizi

Iwapo halitapatikana suluhisho katika mzozo huu, "kundi pekee litakalochukua fursa ya mzozo huu ni kundi la Dola la Kiislamu ISIS Daesch," de Mistura amesema, akitumia jina lingine la kundi la IS.

Kundi hili ni "zimwi linalosubiri mzozo huu kuanza ili kuweza kuchukua fursa hiyo," amesema.

Lakini Nashar hakubaliani , akisema: "Iwapo Assad kweli alikuwa anataka kupambana na Daesh, angetuma majeshi yake kwenda Raqa badala ya Douma."

Raqa ni mji uliotangazwa na kundi hilo la Dola la Kiislamu kuwa mji mkuu wao kaskazini mwa Syria, wakati Douma ni ngome kuu ya waasi katika eneo la mashariki la Ghouta mashariki mwa Damascus ambao umezingirwa na majeshi ya serikali kwa zaidi ya mwaka mmoja sasa.

Syrien Opposition Istanbul Türkei Syrischer Nationalrat Samir Nashar Abdulrazzak Eid
Samir Nashar (kulia) mjumbe wa muungano wa kitaifa nchini SyriaPicha: Reuters

Zaidi ya watu 183 wameuwawa katika mashambulizi ya karibu kila siku mjini Douma katika muda wa wiki chache zilizopita, kwa muijibu wa shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria, ambalo limesema watoto 29 ni miongoni mwa waliouwawa.

"Inaelekea de Mistura hajasikia juu ya mauaji ya kiholela mjini Douma," amesema Nashar.

Mwanaharakati kutoka Douma, ambaye amejitaja kuwa ni Mohammed salaheddin, pia amepinga tathmini hiyo ya mjumbe wa Umoja wa Mataifa.

"Assad anaweza tu kuchangia katika suluhisho la kisiasa kwa kuyaamuru majeshi yake kusitisha mashambulizi ya makombora dhidi ya raia na kwa -- kuondoa mzingiro katika mji wa mashariki wa Ghouta," ameliambia shirika la habari la AFP kuitia Skype.

Mwandishi: Sekione Kitojo / afpe