1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Assad:Ushindi hauko mbali

31 Mei 2013

Rais Bashar al Assad wa Syria anazungumzia shinikizo la kufungua uwanja wa mapigano katika milima ya Golan katika wakati ambapo wanajeshi wake wamepania kuukomboa mji wa Qusseir unaoshikiliwa na waasi.

https://p.dw.com/p/18hiZ
Rais wa Syria Bashar al-AssadPicha: Reuters

Katika mahojiano na kituo cha televisheni cha Hisbollah-Al Manar,rais Bashar al Assad amekiri amepokea makombora ya kimambo leo ya kinga dhidi ya mashambulio ya kutoka angani kutoka kwa washirika wake,Urusi na kuzungumzia shionikizo linalozidi kukua la kufunguwa uwanja mwengine wa mapigano katika milima ya Golan dhidi ya Israel.

Amesema kwa mara nyengine tena anaamini wanajeshi wake wataibuka na ushindi dhidi ya waasi na kwamba haondoi uwezekano wa kugombea tena kiti cha rais uchaguzi utakapoitishwa nchini Syria mwakani.

Licha ya shida za kuandaa mkutano wa kimataifa uliolengwa kusaka amani ya Syria,Umoja wa mataifa umesema kikao cha maandalizi ya mkutano huo kitaitishwa June 5 ijayo mjini Geneva kati ya wawakilishi wa Marekani,Urusi na Umoja wa mataifa.

Serikali ya Bashar al Assad imeridhia kimsingi kushiriki katika mkutano huo bila ya masharti.Upande wa upinzani lakini unasema hautoshiriki katika mazungumzo yoyote kwa muda wote ambao vikosi vya Hisbollah na vile vya Iran vinakutikana nchini Syria.

Urusi itaheshimu mikataba yote iliyofikiwa

Katika wakati ambapo Israel inaangalia kwa jicho la hofu mpango wa Urusi kuipatia Damascus makombora chapa S-300,,rais Bashar al Assad anajinata akizungumzia uwezekano wa kufunguliwa uwanja mwengine wa mapigano katika milima ya Golan.Ameonya serikali yake itajibisha hujuma zozote kutoka Israel.

Russland S-300 Raketen
Makombora ya UIrusi chapa S-300Picha: AP

Duru kutoka Moscow zinasema Urusi haifikirii kuipatia Syria makombora hayo kabla ya msimu wa mapukutiko mwaka huu.Badala yake lakini Moscow inapanga kuheshimu mikataba yote iliyotiwa saini na kutuma ndege 10 za kivita chapa MiG-29 kama ilivyokubaliwa hapo awali.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Uingereza William Hague anaukosoa uamuzi wa Moscow wa kuipatia silaha Syria.Na mjini Washington msemaji wa baraza la usalama wa taifa la Marekani amesema Moscow ingefanya vyema,kumtanabahisha Assad aunde tume ya kusimamia kipindi cha mpito badala ya kuipatia silaha serikali ya mjini Damascus.

Al Nusra yajumuishwa katika orodha ya magaidi

Syrien Bürgerkrieg Kämpfer von Al Nusra Front
Wanamgambo wa al Nusra katika mapigano ya IdlbPicha: picture-alliance/AP

Nchini Syria kwenyewe mapigano yamepamba moto.Huko Qousseir,wanajeshi wakisaidiwa na wanamgambo wa Hisbollah wameanzisha opereshini ya kuikomboa ngome hiyo ya waasi katika wakati ambapo upande wa upinzani umeitolea wito jumuia ya kimataifa iwahui raia elfu moja waliokwama.

Wazungu watatu,akiwemo bibi mmoja wa kimarekani na muingereza mmoja,wameuliwa na wanajeshi wa serikali huo Idlib.Walikuwa wakipigana upande wa waasi.Wakati huo huo huo Umoja wa mataifa umewajumuisha katika orodha nyeusi wanamgambo wa itikadi kali wa Al Nusra ambao ni sehemu ya makundi ya upande wa upinzani yanayopigana dhidi ya serikali ya rais bashar al Assar.Wanatuhumiwa kuwa na mshikamano na mtandao wa kigaidi wa Al Qaida.

Mwandishi:Hamidou Oummilkheir/AFP/Reuters
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman