1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran itafanya nini Trump akijiondoa kwenye mkataba-nyuklia

7 Mei 2018

Rais Trump anatarajiwa kuiondoa Marekani kwenye mkataba wa nyuklia wa Iran mwezi Mei tarehe 12. Iran ilitia sahihi makubaliano ya mpango wa kudhibiti silaha za nyuklia pamoja na mataifa manane makubwa ulimwenguni.

https://p.dw.com/p/2xKM2
Korea Asien-Reise des US-Präsidenten | Protest in Seoul
Picha: picture alliance/ZUMAPRESS/Seung Il Ryu

Mataifa hayo ni pamoja na China, Ufaransa, Urusi na Marekani yaliyotia sahihi mkataba huo mwaka 2015. Iran ilikubali kutia sahihi makubaliano hayo kwa kuondolewa baadhi ya vikwazo, lakini kujiondoa kwa Marekani huenda kukasambaratisha makubaliano hayo. 

Iwapo hilo litatokea, huenda Iran ikajibu kwa kuhujumu maslahi ya Marekani na washirika wake Mashariki ya Kati. Rais wa Iran Hassan Rouhani alisema siku ya Jumapili kuwa nchi hiyo inayo mipango ya kujibu hatua yoyote itakayochukuliwa na Rais wa Marekani Donald Trump, na kuongeza kuwa Marekani itajutia uamuzi wake wa kujiondoa katika mkataba huo.

Vitisho vya Trump 

Trump amesema hadi pale washirika wa Ulaya warekebishe kile anachokitaja kuwa kasoro katika makubaliano hayo ya nyuklia ya Iran kufikia Mei 12, atakataa kurefusha nafuu ya vikwazo vya Marekani kwa Iran. Uingereza, Ufaransa na Ujerumani zinaendelea kujifunga kwenye mkataba huo, lakini katika juhudi za kuibakisha pia Marekani, zinataka mazungumzo kuhusu programu ya makombora ya Iran, shughuli zake za nyuklia baada ya mwaka 2025 - wakati ambapo vipengele muhimu vya makubaliano hayo vitakapoisha muda wake - pamoja na ushiriki wake katika migogoro ya Mashariki ya Kati kama vile Syria na Yemen.

Rais Hassan Rouhani wa Iran
Rais Hassan Rouhani wa Iran Picha: picture alliance/AP Photo/Iranian Presidency Office

Hata hivyo jana Jumatatu, Rais Rouhani alibadili msimamo akisema Iran  itakuwa tayari kuendelea kuheshimu mkataba huo hata Marekani itaamua kujitoa. Akizungumza wakati wa mkutano na maafisa wa serikali katika mji wa kaskazini-mashariki wa Mashhad, Rouhani alisema wanachokitaka ni kwa makubaliano kulindwa na kudhaminiwa na mataifa yasiyo Marekani - akimaanisha mataifa mengine yaliotia saini makubaliano ya mwaka 2015. Akaogeza kuwa katika mazingira kama hayo, Marekani inaweza kujitoa.

Wadadisi wanasema iwapo Marekani itajitoa katika makubaliano, Iran inaweza kuchukuwa hatua zinazoweza kuhujumu maslahi ya Marekani, kama vile kuyahimiza makundi ya wanamgamo wa Kishia iliyosaidia kuwapa mafunzo wakati wa mapambano dhidi ya kundi la Dola la Kiislamu, na ambao wanaitaka Marekani kuondoka nchini Iraq, kuzidisha vita vya maneno au hata kuanza kuwashambulia wanajeshi wa Marekani walioko Iraq.

Huenda kukawa na hofu ulimwenguni

Mkutano wa Umoja wa Ulaya kuhusu mkataba wa nyuklia
Mkutano wa Umoja wa Ulaya kuhusu mkataba wa nyuklia Picha: Getty Images/AFP/J. Klamar

Nchini Syria ambako Iran ina ushawishi mkubwa juu ya makundi ya wapiganaji wa Kishia wanaokadiriwa kufikia elfu 80, huenda ikakosa marali ya kuwadhibiti wapiganaji hao kutofanya mashambulizi kw amfano dhidi ya mshirika wa Marekani Israel, na hata pia kuwasababishia matatizo washauri wa kijeshi wa Marekani walioko Syria wapatao 2,000.

Iran pia ina fursa kadhaa kuhusiana na mpango wake wa kinyuklia. Maafisa wa Iran wamesema kuwa moja ya fursa wanazoangalia ni kujiondoa kabisa kwenye makubaliano yanayolenga kukabiliana na uueneaji wa silaha za nyuklia. Kiongozi mkuu wa kidini wa Iran Ayatollah Ali Khamenei anasema kuwa taifa hilo halina nia ya kutengeza silaha za nyuklia. Lakini Iran ikijiondoa kwenye mkataba huo, itasababisha taharuki kote ulimwenguni.

Hata Iran ikijiondoa kwenye makubaliano yanayolenga kukabiliana na ueneaji wa silaha za nyuklia, tayari imeonesha kuwa itaboresha mpango wake wa urani inayoibua hofu ya kutengeneza bomu la atomiki.

Juma hili mkuu wa shirika la la Nishati ya Atomiki, Ali Akbar Salehi, alisema kuwa Iran ina uwezo wa kuboresha mipango yake ya madini ya urani kwa kiwango kikubwa kabla ya makubaliano.

Mwandishi: Shisia Wasilwa, Reuters

Mhariri: Mohammed Khelef