1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU kutuma wanajeshi 5,000 Burundi

Admin.WagnerD18 Desemba 2015

Baraza la usalama na amani la Umoja wa Afrika limekubaliana kutuma kikosi cha wanajeshi 5,000 wa kuweka amani nchini Burundi, baada ya mkutano wa nchi 54 kuonya kuwa hawatoruhusu mauwaji ya halaiki kufanyika.

https://p.dw.com/p/1HPax
Addis Abbba Afrikanische Union Friedens- und Sicherheitsrat
Picha: picture-alliance/dpa/D. Getachew

Mwana diplomasia mmoja amesema Baraza hilo linachukua hatua hii kwa mara ya kwanza kwa kutekeleza sheria ambayo inaruhusu kutuma kikosi cha wanajeshi bila idhini ya nchi husika. Burundi ambayo maafisa wa Umoja wa Mataifa wamesema inaelekea kutumbukia kwenye vita vya wenyewe kwa wenyewe,imesema hakuna haja ya kutuma kikosi cha kulinda amani nchini humo.

Uamuzi wa Umoja wa Afrika ambao ulifikiwa hapo jana jioni,unahitaji kuidhinishwa na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa,ambalo limekuwa likitafakari namna ya kuusuluhisha mzozo wa Burundi ikiwemo kutuma kikosi cha kulinda amani.

Afisa mkuu wa Umoja wa Afrika Bonaventure Cakpo Guebegde ameliambia shirika la habari la AFP kuwa wanajeshi hao watakuwa chini ya kikosi cha dharura cha Afrika Mashariki. Naye mwana diplomasia wa mojawapo ya nchi wanachama wa baraza hilo la amani na usalama la Umoja wa Afrika ameliambia shirika la habari la Reuters kuwa wamekubaliana kutumwa kwa kikosi cha wanajeshi 5000 ambapo mojawapo ya majukumu yao itakuwa kuwalinda raia.

Hofu ya kuongezeka kwa vurugu

Maafisa wa Umoja wa Mataifa na mabalozi wa mataifa ya magharibi wameelezea hofu yao juu ya kuongezeka kwa vurugu nchini Burundi nchi ambayo imetoka kwenye mapigano ya kikabila yaliyozuka mwaka 2005 baada ya nchi hiyo kushuhudia miaka 12 ya vita.

Maafisa wa kijeshi mjini wakishika doria Bujumbura
Maafisa wa kijeshi wakishika doria BujumburaPicha: Getty Images/AFP

Umoja wa Mataifa umesema watu wasiopungua 400 wameuawa tangu mwezi Aprili wakati mzozo ulipozuka baada ya Rais Pierre Nkurunziza kusema anawania muhula wa tatu uongozini.Mzozo huo unahusisha wapinzani waliopinga kuchaguliwa tena kwa Rais huyo na wanaomuunga mkono.

Mapigano hayo yamefanya kanda hiyo kuwa katika hali tete miongo kadhaa baada ya mauaji ya halaiki katika nchi jirani ya Rwanda.Vita hivyo vimetokea zaidi katika mji mkuu Bujumbura,ambapo wavamizi walivamia kambi za kijeshi siku ya Ijumaa.Karibu watu 90 waliuwawa kwenye ghasia hizo.

Orodha ya watakaowekewa vikwazo kuwasilishwa

Wanadiplomasia wanahofia mapigano hayo huenda yakazua migawanyiko ya kikabila.Mapigano hayo ya wenyewe kwa wenyewe yamehusisha jeshi ambalo wakati huo liliongozwa na kabila la watu wachache la Watusti dhidi ya makundi ya waasi ya kabila la wahutu walio wengi likiwemo moja linaloongozwa na Nkurunziza.

Baraza la usalama na amani la Umoja wa Afrika limemtaka mwenyekiti wa Tume ya Umoja huo Nkosazana Dlamini Zuma,kuwasilisha katika muda wa wiki moja orodha ya watu watakaowekewa vikwazo.

Rais wa Burundi alisema hapo jana nchi yake iko tayari kufanya mazungumzo .Wapinzani hata hivyo wamepuuza matamshi hayo hapo awali wakisema serikali haijajitolea kujadili maswala muhimu ikiwemo hilo la awamu mpya ya Rais Nkurunziza.

Mwandishi:Bernard Maranga/Reuters/AFP

Mwandishi:Yusuf Saumu