1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Umoja wa Afrika waishambulia mahakama ya ICC

Admin.WagnerD19 Novemba 2015

Umoja wa Afrika umeishambulia mahakama ya kimataifa ya Uhalifu ICC kwa kuliandama bara hilo na kujikita zaidi katika kesi zinazowahusu wanasiasa barani Afrika .

https://p.dw.com/p/1H8nY
Niederlande Kenia Anhörung zu Gewalt nach Präsidentenwahl in den Haag William Samoei Ruto
Picha: dapd

" Tumefikia uamuzi ya kuwa mahakama hii ambayo kwa ujumula bara la Afrika liliunga mkono kuanzishwa kwake, inaonekana kutotenda haki kwa watu wote" alisema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ethiopia, Tedros Adhanom Ghebreyesus.

Waziri huyo wa mambo ya nchi za nje wa Ethiopia alikuwa akizungumza kwa niaba ya umoja huo wa Afrika katika mkutano mkuu unaohusisha mataifa yapatayo 123 yaliyotia saini uanzishwaji wa mahakama hiyo ya uhalifu ya kimataifa ya ICC iliyoko The Heague nchini Uholanzi.

Rais wa Kenya Uhuru Kenyata na makamu wake William Ruto walifunguliwa mashitaka na mahakama hiyo kwa tuhuma za kuchochea machafuko baada ya uchaguzi mkuu nchini humo katika kipindi cha mwaka 2007-2008 ambayo yalisababisha kiasi cha watu 1,200 kupoteza maisha nchini humo.

Hata hivyo mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama hiyo Fatou Bensouda alimfutia mashitaka Rais Uhuru Kenyata mwezi desemaba mwaka jana baada ya kukosekana ushahidi wa kutosha kuweza kumtia hatiani.

Hatua hii ilionekana kuwa mkwamo wa kutosha kwa mahakama hiyo tangu kuanzishwa kwake kwa lengo la kushughulikia mashitaka yanayohusu mauaji ya kimbari , uhalifu wa kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Kenya yasisitiza kutupiliwa mbali kwa kesi hiyo

Kenya kwa sasa inataka mkutano huo wa sasa unaohusisha mataifa yaliyotia saini uanzishwaji wa mahakama hiyo kujadili uhalali ulioumpa nguvu mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama hiyo kutumia ushahidi ambao ulionekana haufai hapo awali na sasa kutumika katika kesi inayomkabili makamu wa Rais wa Kenya William Ruto.

Fatou Bom Bensouda
Fatou Bensouda-mwendesha mashitaka mkuu wa mahakama ya uhalifu ya ICCPicha: picture-alliance/dpa/MARCEL BIERI

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Kenya Amina Mohamed alisema ," Tuna amini kuwa majaja wanaohusika na kesi hii hawakuwa na sababau za msingi za kukubali kutumika kwa ushahidi ambao ulikwishatupiliwa mbali na pia tunaona hakukuwa na sababu za msingi za kuwepo kwa kesi hii dhidi ya William Ruto".

Kenya na Afrika Kusini ambayo imekumbwa na mzozo na mahakama hiyo ya uhalifu kwa kushindwa kumkamata Rais awa Sudan Omar Hassan al-Bashir alipokuweko Afrika Kusini kuhudhuria Mkutano wa Viongozi wakuu wa nchi za kiafrika mwezi Juni, zimetishia kujitoa kwenye mahakama hiyo ya kimataifa .

Kwa upande wake mwendesha mashitaka mkuu wa ICC Bibi Bensouda aliliambia Shirika ala habari la Ufaransa AFP katika mahojiano kwamba kuna ukosefu wa imani ya kisiasa nchini Kenya kuhusu kesi hizo na kwamba amalalamiko ya Umoja wa Afrika hayaendani na hali halisi na ukweli ulivyo , akiongeza kwamba malalamiko hayo ni ya juu juu tu na yasio na msingi.

Mwandishi: Isaac Gamba

Mhariri: Mohammed Abdul-rahman