1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU yasita kutuma kikosi Burundi

31 Januari 2016

Viongozi wa Umoja wa Afrika wamesita kutuma kikosi cha kulinda amani nchini Burundi kutokana na upinzani mkali wa serikali ya nchi hiyo ya Afrika ya Kati iliokumbwa na vurugu.

https://p.dw.com/p/1Hmb8
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria (kushoto) na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika.
Rais Muhammadu Buhari wa Nigeria (kushoto) na Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika.Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Kwa sasa Umoja wa Afrika unapendekeza kufanyika kwa mazungumzo zaidi. Umoja wa Mataifa umeonya kwamba Burundi iko katika hatari ya kuzuka tena kwa vita vya wenyewe kwa wenyewe vya mwaka 1993-2006 wakati mamia ya watu wameuwawa tokea mwezi wa Aprili mwaka 2015 wakati Rais Pierre Nkurunzinza alipotangaza kuwania tena muhula wa tatu madarakani.

Takriban watu 230,000 wamekimbilia katika nchi jirani.

Burundi imekuwa ikipinga moja kwa moja wazo la Umoja wa Afrika kutuma kikosi cha wanajeshi 5,000 nchini humo ikisema kwamba uwekaji wa kikosi hicho cha kulinda amani bila ya kibali cha nchi hiyo kitakuwa sawa na kikosi cha uvamizi.

Ibara ya 4(h) ya katiba ya Umoja wa Afrika inakipa chombo hicho cha majumuyo ya Waafrika haki ya kuingilia kati katika nchi mwanachama wake kutokana pindipo hali inakuwa mbaya kama vile uhalifu wa kivita,mauaji ya kimbari na maouvu dhidi ya ubinaadamu.

Hakuna nia ya kuikalia Burundi

Mwanadiplomasia mwandamizi wa Umoja wa Afrika Ibrahim Fall amesema Jumapili kwamba kutuma vikosi hivyo bila ya ridhaa ya Burundi ni jambo lisilowazika na badala yake taasisi hiyo imeamuwa kutuma ujumbe kwa mazungumzo na serikali.

Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika.
Rais Uhuru Kenyatta wa Kenya katika Mkutano wa Kilele wa Umoja wa Afrika.Picha: Getty Images/AFP/T. Karumba

Mkuu wa Baraza la Amani na Usalama la Umoja wa Afrika Smail Chergui ameongezea kwa kusema "Hakuna nia ya kuikalia nchi hiyo kwa mabavu wala kuishambulia" na kwamba iwapo Burundi itakubali hicho kitakuwa kikosi cha kusalimisha silaha.

Mapambano kati ya watiifu wa serikali na upinzani yamezidi kuwa ya matumizi ya nguvu nchini Burundi.

Chergui amewaambia wandishi wa habari bila ya kufafanuwa zaidi kwamba wanataka mazungumzo na serikali na kwamba mkutano huo wa kilele umeamuwa kutuma ujumbe wa ngazi ya juu.

Kutokuchukuwa hatua

Rais Idriss Deby wa Chad akizungumza baada ya kuchukuwa wadhifa wa uwenyekiti wa Umoja wa Afrika kutoka kwa Rais Robert Mugabe hapo Jumamosi amewaonya viongozi wenzake juu ya uamuzi wa kutochukuwa hatua.

Rais Idriss Deby wa Chad Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.
Rais Idriss Deby wa Chad Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika.Picha: AFP/Getty Images/Seyllou

Deby amesema "Umoja wetu unatenda kama iivyokuwa kwa miaka 20 au 30 iliopita, tunakutana sana, tunazungumza sana,tunaandika sana lakini hatuchukuwi hatua za kutosha na mara nyengine hatuchukuwi hatua yoyote ile."

Wachambuzi wanasema mataifa ya Afrika yanahofu sana ya kuanzisha mwenendo wa kutuma vikosi dhidi ya matakwa ya serikali.

Viongozi wa Umoja wa Afrika wamekuwa wakijadili kwa siku mbili mzozo huo wa Burundi katika mkutano wao wa kilele wa nchi wanachama 54 mjini Addis Ababa Ethiopia.

Burundi yagomea kikosi cha AU

Waziri wa mambo ya nje wa Burundi Alaine Nyamwiti ameliambia shirika la habari la Ujerumani dpa kwamba Burundi haitoruhusu walinda amani wa Umoja wa Afrika kuwepo nchini humo.

Wanajeshi nchini Burundi.
Wanajeshi nchini Burundi.Picha: Getty Images/S. Platt

Akizungumza mjini Addis Ababa Jumapili pembezoni mwa mkutano huo wa kilele wa Umoja wa Afrika uliomalizika siku hiyo amesema iwapo nia ya Umoja wa Afrika ilikuwa ni kuishawishi Burundi kukubali kikosi hicho "tayari imeshindikana.".

Amesema hakuna ridhaa ya serikali na kwamba wana uwezo wa kuilinda nchi yao.Ameongeza kwamba "Lazima kuwepo ridhaa kutoka Burundi ya kuweka kikosi hicho.Tunashukuru Baraza la Amani na Usalama kwa uamuzi wake."

Rais wa Burundi Pierre Nkurunzinza ameahidi kupambana na walinda amani wowote wale watakaotumwa na Umoja wa Afrika kwa hoja kwamba hatua hiyo inakiuka uhuru wa Burundi.

Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP/dpa

Mahariri : Isaac Gamba