1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

AU yazionya Sudan kusitisha mapigano

28 Machi 2012

Umoja wa Afrika (AU) umeeleza wasiwasi wake juu ya hali tete ya usalama katika mpaka wa Sudan na Sudan ya Kusini na kuyataka majeshi ya nchi hizo mbili kuondoka katika eneo la mpakani haraka iwezekanavyo.

https://p.dw.com/p/14TFH
Mwenyekiti wa kamisheni ya Au, Jean Ping
Mwenyekiti wa kamisheni ya Au, Jean PingPicha: Reuters

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika, Jean Ping, amesema kwamba migogoro yoyote kuhusu mpaka wa nchi inaweza kusuluhishwa kwa njia ya amani. Ping ameyataka majeshi ya Sudan na Sudan ya Kusini kurudi nyuma kwa umbali wa kilometa 10 kutoka katika eneo la mpaka unaozitenganisha nchi hizo ili kuzuia mapigano zaidi.

Wito wa Ping unakuja baada ya ndege za kijeshi za Sudan jana kuyashambulia maeneo yenye mafuta yaliyoko Sudan ya Kusini, ikiwa ni siku ya pili ya mashambulizi. Sudan ya Kusini nayo iliyashambulia majeshi ya Sudan na hivi sasa kila nchi inamlaumu mwenzake kwamba ndiye aliyeanzisha mashambulizi hayo.

Umoja wa Afrika umekuwa ukifanya mazungumzo ya kuleta amani baina ya nchi hizo mbili. Migogoro ilianza baada ya Sudan ya Kusini kujitenga na Sudan na kuwa taifa huru mwezi Julia mwaka jana.

Maafisa wa ngazi ya juu kufanya mazungumzo

Kufuatia mapigano yaliyotokea katika eneo la mpakani, Sudan imeahirisha mazungumzo yaliyokuwa yamepangwa kufanyika tarehe 3 mwezi April kati ya Rais Omar al-Bashir wa nchi hiyo na mwenzake wa Sudan ya Kusini, Salva Kiir, mjini Juba. Lakini maafisa wa serikali ya Sudan ya Kusini wamesema kwamba kwa upande wao mazungumzo bado yanaweza kufanyika.

Rais Omar al-Bashir wa Sudan
Rais Omar al-Bashir wa SudanPicha: picture alliance / Photoshot

Hata hivyo, viongozi wa ngazi ya juu wa Sudan na Sudan ya Kusini wanatarajiwa kukutana wiki hii kwa ajili ya kufanya mazungumzo juu ya namna ya kurudisha amani kati ya nchi hizo mbili. Umoja wa Afrika umesema kwamba pande zote mbili zimeahidi kutuma wajumbe, ambao wataanza mara moja uchunguzi juu ya mapigano yaliyofanyika jana na juzi.

Waasi washambulia wanajeshi

Jean Ping wa Umoja wa Afrika, amezitaka Sudan na Sudan ya Kusini kuheshimu mkataba wa kutokushambuliana uliosainiwa na nchi hizo mwezi Februari mwaka huu. Tangu kusainiwa kwa mkataba huo, pande zote mbili mara kwa mara zimejihusisha na matendo yanayovunja makubaliano yaliyofikiwa.

Sudan na Sudan ya Kusini zinayapigania maeneo yenye mafuta
Sudan na Sudan ya Kusini zinayapigania maeneo yenye mafutaPicha: picture-alliance/Ton Koene

Msemaji wa jeshi la Sudan amewashutumu waasi wa kundi la Justice and Equality Movement, JEM, kutoka eneo la Darfur kujiingiza katika mapigano dhidi ya wanajeshi wa Sudan. Waasi wa kundi JEM wameyakanusha madai hayo.

Kwa upande mwingine kundi la waasi wa Sudan ya Kusini, Southern Sudan Liberation Army, SSLA, limeeleza kwamba limewashambulia wanajeshi wa nchini humo na kujisifia kwamba limefanikiwa kuua baadhi ya wanajeshi hao.

Mwandishi: Elizabeth Shoo/AFPE
Mhariri: Mohammed Khelef