1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Aung San Suu Kyi akutana na utawala wa kiejshi wa Myanmar

Josephat Charo26 Oktoba 2007

Mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa Ibrahim Gambari ametoa mwito kuwepo mazungumzo zaidi kati ya utawala wa kijeshi wa Myanmar na Aung San Suu Kyi baada ya kiongozi huyo anayetetea demokrasia kukutana kwa mara kwanza na afisa wa ngazi ya juu wa utawala wa kijeshi.

https://p.dw.com/p/C77T
Aung San Suu Kyi
Aung San Suu KyiPicha: AP

Bwana Ibrahim Gambari, mpatanishi wa Umoja wa Mataifa katika mzozo wa Myanmar amesema hii ni hatua ya kwanza tu kuelekea kufikia ufumbuzi wa mzozo wa Myanmar. Akizungumza na waandishi wa habari mjini Tokyo Japan, baada ya kukutana na waziri mkuu Yasuo Fakudam bwana Gambari amesema mazungumzo kati ya Sung San Suu Kyi na utawala wa kijeshi huenda yakafungua mlango kwa kuanza tena mazungumzo yatakayoleta matokeo ya maana.

Mazungumzo kati ya utawala wa kijeshi wa Myanmar na Aung San Suu Kyi ni juhudi za kufuta shutumua za matumizi ya nguvu kupita kiasi katika kuzima maandamano ya watawa wa kibuda kabla ziara ya mjumbe maalumu wa Umoja wa Mataifa nchini humo wiki ijayo.

Aung San Suu Kyi jana aliruhusiwa kwa muda mfupi atoke nyumbani kwake ambako amekuwa akizuiliwa kwa miaka 12 kati ya miaka 18 ya kifungo chake cha nyumbani, ili akutane na waziri wa kazi Aung Kyi, aliyeteuliwa afanye mazungumzo kutafuta maridhiano na upinzani.

Ingawa hakuna habari zilizotolewa kuhusu mazungumzo kati ya Aung San Suu Kyi na waziri wa kazi Aung Kyi yaliyodumu muda wa saa moja, mazungumzo hayo yalionyeshwa katika runinga ya taifa, jambo ambalo ni nadra katika nchi ambayo Aung San Suu Kyi amekaa miaka mingi bila kuonekana hadharani. Kiongozi huyo amewahi kusema kwamba hatua ya kwanza kufikia demokrasia nchini Myanmar itakuwa ngumu.

´Hatua ya kwanza. Hatua kubwa itakayofaa kuleta madadiliko kutoka utawala wa kiimla hadi utawala wa kidemokrasia itakuwa ngumu. Lakini mara tu hatua hiyo itakapochukuliwa nina hakika kwamba watu wetu wataweza kukabiliana na changamoto za jamii iliyo na demokrasia.´

Chaichoke Chulsiriwong, mtaalamu wa maswala ya Myanmar katika chuo kikuu cha Chulalongkorn mjini Bangkok, amesema ni hatua muhimu kwamba utawala wa kijeshi umefanya mazungumzo na kiongozi wa upinzani, Aung San Suu Kyi, lakini akaonya kuwepo na uangalifu.

Debbie Stothard wa shirika la kutetea haki za binadamu la Alternative ASEAN Network, amesema mkutano baina ya serikali ya kijeshi ya Myanmar ni porojo za kujisafisha maovu iliyoyafanya dhidi ya raia huku hali ikiwa bado haijabadilika na watu wakiendelea kuzuiliwa.

Kwa kumchagua waziri wa kazi azungumze na kiongozi wa upinzani utawala wa kijeshi umeashiria uko tayari kuwa na mawasiliano na upinzani kinyume cha msimamo wake mkali wa hapo awali, huku Ibrahim Gambari akitarajiwa nchini Myanmar wiki ijayo.

Ibrahim Gambari amekamilisha mazungumzo yake na China kuhusu Myanmar bila mafinikio makubwa lakini msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni ya China, Li Jianchao, amesema China itaendelea kuchangia katika kutafuta ufumbuzi wa mzozo nchini Myanmar kwa amani.

´Hii ni hali tete nchini Myanmar ambayo inakumbusha historia ya nchi hiyo. Lazima itatuliwe na serikali na wananchi. Jumjui ya kimataifa inatakiwa isielemee upande wowote na iwe na busara katika kusaidia na kujenga uaminifu.´

Wakati huo huo utawala wa kijeshi wa Myanmar leo umetuma maafisa wa polisi waliojihami na silaha katika eneo la Shwedagon Pagoda na Sule Pagoda katikati ya mji wa Yangon ili kuzuia kutokea tena maandamano kama ya mwezi uliopita yaliyoongozwa na watawa wa kibuda.