1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ukweli kuhusu baa la njaa

Mohammed Khelef
24 Februari 2017

Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) linasema kuwa takribani watoto milioni 1.4 wanaweza kufa kutokana na njaa kwenye mataifa ya Nigeria, Somalia, Sudan Kusini na Yemen.

https://p.dw.com/p/2YBj7
Somalia Puntland
Picha: DW/A. Kiti

Ingawa baa hilo la njaa lilitangazwa rasmi siku ya Jumatatu (20 Februari) katika baadhi tu ya maeneo ya Sudan Kusini, ukweli ni kuwa tayari watu wameanza kufa kutokana na njaa kwenye mataifa yote manne.

Shirika la Chakula la Umoja wa Mataifa (WFP) linasema maisha ya watu zaidi ya milioni 20 yako hatarini ndani ya kipindi cha miezi sita ijayo.

Kwa mujibu wa Umoja wa Mataifa, hali huitwa "baa la njaa" pale inapotokezea kuwa kwa uchache asilimia 20 ya familia kwenye eneo husika zinakabiliwa na uhaba mkubwa wa chakula, kiwango cha utapiamlo kinapopindukia asilimia 30, na pale ambapo katika kila watu 10,000, wawili au zaidi wanakufa kila siku kwa kukosa chakula. 

Baa la njaa ni moja ya majanga ambayo yamemkumba mwanaadamu kwa kipindi kirefu katika historia yake. Roho nyingi zimepotea kwa sababu ya janga hili. Zifuatazo ni dondoo za mabaa makubwa ya njaa duniani kwa kipindi cha karne moja iliyopita:

Somalia

Mnamo mwaka 2011, Somalia ilikabiliwa na baa la njaa ambalo liliangamiza maisha ya watu 260,000 katika mikoa ya kati na kusini. Ingawa janga hilo lilitangazwa rasmi mwezi Julai, lakini watu wengi walikuwa tayari wameshakufa kufikia mwezi Mei. 

Umoja wa Mataifa ulitangaza baa la njaa limekwisha nchini Somalia mwezi Februari 2012 kufuatia mavuno makubwa kabisa baada ya mvua kunyesha kwa kiwango kizuri na kufikishwa kwa misaada ya chakula.

Somalia Puntland
Mifugo yapoteza maisha Puntland, Somalia.Picha: DW/A. Kiti

Lakini sasa, miaka kadhaa baadaye, ukame umezikumba nchi za eneo hilo - zikiwemo Kenya na Ethiopia - na kuyaangamiza mazao na, kwa upande mwengine, mapigano kati ya kundi la al-Shabaab na serikali ya Somalia yanayafanya mashirika ya misaada kushindwa kuzifikia jamii zilizoathirika sana kwa njaa kusini mwa nchi hiyo.

Ethiopia

Sera za Kimaksi za Mengistu Haile Mariam ziliingiza nchi hiyo kwenye hali mbaya sana kiuchumi, njaa na migogoro, ambayo ilikula nusu ya bajeti yake. Katika baa la njaa la mwaka 1984 hadi 1985, raia wapatao milioni moja walikufa kwa njaa. 

Kwa miezi kadhaa ya mwaka 1984, utawala wa Mengistu ulikanusha kuwepo kwa njaa kwenye eneo la kaskazini la nchi yake, badala yake wafanyakazi wa misaada waliripoti kuwa alisafirisha kreti kadhaa za ulevi kuadhimisha mapinduzi yake, huku njaa ikizidi kuenea.

Cambodia

Watu wapatao milioni 2 walikuwa kwa njaa kutokana na muongo mzima wa vita vya wenyewe kwa wenyewe, yaliyofuatiwa na utawala wa kikatili wa Khmer Rouge hadi mwaka 1978 na hatimaye uvamizi wa Vietnam uliokomesha utawala wa Khmer Rouge mwaka 1979.

China

Mpango wa Mao Zedong wa China ulioitwa "Mchupo Mkubwa Kusonga Mbele" mwishoni mwa miaka ya 1950, ulisababisha vifo vya kati ya watu milioni 10 na 30. Mpango huo ulijumuisha kukifanya kilimo kuwa cha kisasa na kuongeza uzalishaji wa ngano. 

Sudan Dürre bei El-Fasher
Ukame waathiri sehemu nyingi za duniaPicha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Kwa kutaka kumuonesha kiongozi wao kuwa wamefikia ndoto yake, wasaidizi wake walikuwa wakitia chumvi kwenye ripoti za kiwango cha mavuno na kwenye maeneo mengi waliyachukuwa mavuno yote kutoka kwa wakulima na kuyapeleka maghala makubwa ya serikali.

Ilikuwa ni hadi mwaka 1961, ndipo viongozi wa juu wa China walipokuja kuujuwa uhalisia, lakini wakiwa tayari wameshaongeza maradufu usafirishaji nje wa chakula na kukata kabisa uingizaji wa chakula.

Umoja wa Kisovieti

Watu wapatao milioni 8 walikufa njaa kutoka na mkakati mkubwa wa Josef Stalin kuugeuza Umoja wa Kisovieti kuwa taifa linaloongoza kwa viwanda duniani mwanzoni mwa miaka ya 1930. Katika kipindi hicho, serikali ilichukuwa ngano yote na kuisafirisha nje ili kupata pesa kwa ajili ya kununulia vifaa vya viwandani.

Watu wa Ukraine walipolalamikia baa la njaa, Stalin aliwaadhibu kwa kukataa kuwapelekea chakula cha msaada.

Mwandishi: Mohammed Khelef/Reuters
Mhariri: Saumu Yussuf