1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baa la njaa: Uko wapi umoja wa Afrika?

Iddi Ssessanga
6 Aprili 2017

Ugaidi, vita, rushwa, ukame na mavuno hafifu. Umoja wa Mataifa unazungumzia janga kubwa kabisaa la kibinadamu tangu kumalizika kwa vita kuu vya pili vya dunia, linalotokea Yemen na katika baadhi ya mataifa ya Afrika.

https://p.dw.com/p/2apHm
Sudan Dürre bei El-Fasher
Picha: Getty Images/AFP/A. Shazly

Mamilioni ya watu wanakabiliwa na kitisho cha njaa. Na hali ni mbaya hasa katika mataifa ya Ethiopia, Somalia, Sudan Kusini na kanda ya Ziwa Chad. Mashirika ya misaada yanaomba ufadhili zaidi. Jumuiya ya kimataifa imeshtushwa - lakini imeweza kupata sehemu ndogo tu ya misaada ilioahidiwa na mataifa yaliostawi kiviwanda. Mshikamano kati ya mataifa ya Afrika kuhusiana na janga hilo hauonekani, licha ya ukweli kwamba Umoja wa Afrika unaitisha vikao vya kujadili janga hilo na baadhi ya mataifa yakifanya kila yawezalo.

Matthew Rycroft anayo picha kamili ya njaa. Akiwa katika ujumbe wa Umoja wa Mataifa, mwakilishi huyo wa Uingireza katika baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa alizitembelea Ethiopia, Sudan Kusini, Somalia na maeneo yanayozunguka ziwa Chad, ambako kundi la kigaidi la Boko Haram limekuwa likiendesha harakati zake kwa miaka kadhaa kati ya mataifa ya Nigeria, Niger, Kamerun na Chad. Maelfu ya watu wameuawa, kutekwa na vijiji vyao kuangamizwa, na sasa kwa mujibu wa Rycroft, ukame pia umeongezeka.

"Kulikuwepo na swali la iwapo mgogoro huu wa kibinadamu umetiliwa chumvi. Mimi sidhani kama umetiliwa chumvi, tumejionea hali inavyozidi kuwa mbaya. Ukame unazuwiwa tu kutokana na ukarimu wa wafadhili na ufanisi wa uitikiaji wa mataifa husika, lakini ni hilo tu," anasema Rycroft.

USA UN-Sicherheitsrat beschließt Beobachtermission in Kolumbien in New York
Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa Matthew Rycroft (kushoto) alizuru Afrika na kujionea hali halisi ya njaa.Picha: Reuters/M. Segar

Afrika inahitaji kujisaidia pia

Picha za wakimbizi waliokondeana tayari zinazunguka duniani, na Matthew Rycroft anafahamu kwamba anapaswa kuitia kishindo jumuiya ya kimataifa kwa sababu kuna kitisho kwa jumuiya hiyo kushindwa tena. Lakini pia anapaswa kuzungumza kwa lugha bayana na washiriak wake wa Kiafrika, hata kama matamshi yake yake atayavisha joho la kidiplomasia.

"Haihusu tu uitikiaji wa kimataifa, bali pia wa kitaifa, na ndiyo maana tumekuwa tukiihamasisha serikali ya Nigeria, na serikali nyignine tulizozitembelea kuhakikisha kwamba hata wao wanaimarisha uitikiaji wao kama taifa mmoja mmoja na kwa pamoja pia. Tunesikia mambo mazuri na sasa tunataka kuona utekelezaji kamili wa ahadi hizo," anafafanua balozi huyo wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa.

Tafsiri ya hii ni kwamba: Ni zamu yenu sasa. Hata hivyo serikali ya taifa tajiri wa mafuta la Nigeria imeahidi kutenga kiasi cha dola bilioni moja, hata kama hakuna pesa zilizoanza kutolewa mpaka sasa. Lakini madai ya ukosefu wa pesa siyo tatizo pekee katika mapambano dhidi ya njaa, anasema Omolola Adele-Oso kutoka shirika la Act4Accountability.

"Kwa sababu kuna pia rushwa. Nchini Nigeria kwa mfano, tumeona picha za mchele ukipakizwa tena katika magunia mapya na kuuzwa tena, kwa hiyo tuna chakula kinachopelekwa mahala kisipotakiwa kwenda."

Ni aibu na kashfa

Ni jambo la aibu na lisilokubalika, anasema waziri wa maendeleo ya Ujerumani Gerd Müller, kwamba dunia inachukuwa hatua kwa kujikongoja. Lakini jambo la kufedhehesha ni kukosekana kwa mshikamano kwanza kabisaa miongoni mwa wafrika wenyewe, anasema Moussa Faki Mahamat - mwenyekiti mpya wa Halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika.

Hungerkrise in Somalien
Mtoto wa miezi tisa anaekabiliwa na utapiamlo akiwa katika kabi ya wakimbizi mjini Mogadidhu, Somalia. Somalia ndiyo moja ya nchi zilizoathirika zaidi na ukame na njaa.Picha: picture alliance/dpa/F. Abdi Warsameh/AP

"Kitisho cha njaa kinachoikumba sehemu kubwa ya Afrika ni aibu kubwa kwetu. Uwezo mkubwa wa bara letu na ukuaji wa kiuchumi wa mataifa kadhaa wanachama wa Umoja wa Afrika vinatupokonya hoja za kuendelea kulitazama tu janga hili baya," alisema mwenyekiti huyo wa halmashauri kuu ya Umoja wa Afrika. 

Wakati huohuo hali inazidi kuwa mbaya katika baadhi ya mataifa wanachama wa Umoja wa Afrika kama vile Somalia ambako sehemu kubwa ya nchi hiyo inadhibitiwa na kundi la itikadi kali la Al-Shabaab, Au Sudan Kusini, ambako serikali na waasi wanashiriki mapigano yanayowagharimu zaidi raia. Ni nchi chache tu za Afrika zinazowajibika. Uganda inachukuwa wakimbizi kutoka Sudan Kusini, na Ethiopia inafanya kila iwezalo kuwasaidia wahanga wa njaa kutoka nchi jirani ya Somalia.

Ethiopia na Uganda zinategemea misaada ili kuendelea kutoa msaada huo. Lakini maombi ya ndani kwa ndani barani Afrika husikika kwa nadra. Umoja wa Afrika unashughulikia tu migogoro midogo midogo na umetenga mfuko wa dola laki mbili tu kwa ajili ya kuwahudumia watoto wanaokabiliwa na utapiamlo, na umeitaka jumuiya ya kimataifa kuendeleza utoaji wa misaada.

Mwandishi: Alexander Göbel/ARD

Tafsiri: Iddi Ssessanga

Mhariri: Saumu Yusuf