1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baada ya kujiuzulu Olmert ?

31 Julai 2008

Nani atashika wadhifa wa Bw.Olmert waziri mkuu wa Israel aliepanga kujiuzulu ?

https://p.dw.com/p/Enle

Tangazo la waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert jana kwamba anapanga kujiuzulu akikabiliwa na tuhuma za rushua ni hatua nyengine ya historia ndefu ya kinyan'ganyiro cha madaraka ya uongozi nchini Israel.

Nani atashika wadhifa wake atakapon'gatuka ? Ndilo swali linaloulizwa na wachunguzi wengi wa jukwaa la siasa za Israel.Miongoni mwa majina ya usoni kabisa ni waziri wa sasa wa mambo ya nje Tzipi Livni.Waziri mkuu wa zamani mwenye siasa kali kutoka chama cha LIKUD -Benjamin

►◄

Waziri mkuu wa Israel Ehud Olmert amekumbwa na kashfa ya rushua .Mwanabiashara mmoja wa kimarekani Morris Talansky alitoa ushahidi mbele ya Mahkama ya Israel mwezi Mei kwamba alimpa dala 150,000 taslim Bw. Olmert katika kipindi cha miaka 15.Na tangu Olmert hata Talansky wamekataa kufanya kosa.Waziri mkuu Olmert amedai fedha hizo ni michango halali kwa kampeni yake ya uchaguzi alioifanya kabla kuchaguliwa waziri mkuu hapo 2006.Alisema angejiuzulu endapo atakutikana na hatia.

Bw.Olmert aliwahi kuwa diwani mkuu wa jiji la Jeruselem kuanzia 1993 hadi 2003 .Alitumia cheo chake hicho kushika bendera ya majenzi ya maskani za walowezi wa kiyahudi katika sehemu ya waarabu ya jiji la Jeruselem.

Alijiunga na waziri mkuu wa zamani Ariel Sharon baada ya kukiacha mkono chama cha Likud 2005 ili kuunda chama cha KADIMA na akashika uongozi wa chama na wadhifa wa waziri mkuu pale Sharon alipopatwa na kiharusi Januari 2006.Miezi 2 baadae chama cha Kadima kikashinda uchaguzi.

Olmert pamoja na Rais wa Mamlaka ya Ndani ya wapalestina Mahmud Abbas, wakayafufua mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palestina hapo novemba chini ya usimamizi wa Marekani.Hii ilitanguliwa na kuvunjika kabisa kwa mawasiliano kwa muda wa miaka 7 kati ya pande hizo mbili.Azma ilikua kuifikia shabaha ya kuunda dola la wapalestina hadi mwisho wa mwaka huu-shabaha mabayo sasa kwa kupanga kujiuzulu Bw.Olmert yaonesha haitawezekana.

Hapo mei mwaka huu, Olmert alifichua kwamba amekuwa na mazungumzo yasio ya moja kwa moja na Syria kupitia upatanishi wa Uturuki.

Nani sasa atashika wadhifa wake akin'gatuka ?

Wakati waziri mkuu wa zamani kutoka chama cha LIKUD, Benjamin Netanyahu ameitisha uchaguzi mpya, fununu zinadai kwamba waziri wa nje wa Bw.Olmert bibi Tzipi Livni,mjumbe mkuu katika mazungumzo na wapalestina, ndie mwenye nafasi kubwa ya kurithi kiti chake.

Kama Bw.Olmert, Livni pia anatoka chama cha Kadima.Livni pia ndie mwanamke mwenye nguvu sana nchini Israel wakati huu tangu enzi za mama Golda Meir mnamo miaka ya 1970ini.

Ni mwaka jana tu pale Bibi Livni, mwenye umri wa miaka 50, alipomtaka waziri mkuu Olmert kujiuzulu. hii ilifuatia ripoti isiopendeza jinsi Olmert alivyoendesha vita vya Lebanon dhidi ya Hizbollah.

EHUD Barak, waziri wa ulinzi ameunda serikali ya muungano kati ya chama chake cha Leba na KADIMA.Lakini kwavile hana kiti bungeni cha kuchaguliwa, hawezi kuwa waziri mkuu.

Halafu kuna waziri wa sasa wa usafiri-zamani waziri wa ulinzi maarufu kwa kupambana na wapalestina kwa mkono wa chuma-mzaliwa wa Iran SHAUL MOFAZ.yeye alikwishaanzisha kampeni ya kumtimua madarakani Bw.Olmert.