1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baba mtakatifu amaliza ziara yake Afrika

Aboubakary Jumaa Liongo23 Machi 2009

Baba Mtakatifu Benedict wa 16 amemaliza ziara yake ya kwanza barani Afrika kwa kuwataka watu wa bara hilo wabadilishe fikra na mioyo ili wafikie maridhiano yatakayoliondoa katika madhila makubwa.

https://p.dw.com/p/HHaD
Pope Benedict wa 16Picha: AP

Baba mtakatifu alisema hayo katika misa ya wazi iliyofanyika jana Luanda Angola ambako inakadiriwa watu takriban watu millioni moja waliudhuria misa hiyo iliyofanyika katika uwanja uliyojirani na kiwanda cha cement.


Baba mtakatifu  amesema kuwa madhambi barani Afrika yamewasukuma watu masikini katika utumwa na kusisitiza kuwa ni kwa kuachana na dhambi ndiko kutakuwa suluhisho la matatizo yanayolikabili  bara hilo.


Aliuambia umati huo wa waumini wa katoliki mjini Luanda kuwa wingu la dhambi limeigubika Afrika, ikiwemo nchi hiyo ya Angola na kwamba wakati sasa umefikia wa kuliondoa wingu hilo.


Aidha katika kazi hiyo, Papa Benedict wa 16 alikuwa na ujumbe kwa kanisa na liambia.

´´Kanisa barani Afrika ni lazima lijiweke katika nafasi ya kuhubiri maridhiano, haki na amani.Huo ndiyo ujumbe wangu kwenu leo hii´´.


Papa Benedict alielezea kusikitishwa kwake na vifo vya wasichana wawili hapo siku ya Jumamosi kutokana na msongamano mkubwa.


Kwa mujibu wa msemaji wa Vatican Federico Lombardi wasichana hao wawili walikufa na wengine wapatao 40 walijeruhiwa wakati vijana zaidi ya elfu 30 wa Angola walipokusanyika kumsikiliza Papa.


Aidha Baba mtakatifu pia aliwahutubia wanawake wapatao elfu moja mjini humo ambapo alitaka kuheshimiwa kwa haki za wanawake.


Ziara yake hiyo barani Afrika imegubikwa na matamshi aliyoyatoa kwamba mipira ya kiume yaani kondomu haizuii kuenea kwa ukimwi bali inachangia kusambaa zaidi kwa maradhi hayo.


Kauli yake hiyo ambayo ni kukazia msimamo wa kanisa, imekabiliwa na upinzani mkali kutoka kwa  wanaharakati wa kupambana na ukimwi.


Mjini Paris watu 11 wamekamatwa baada ya makundi ya wanaharakati hao kuandamana hadi katika kanisa la Notre-Dame jijini humo kupinga kauli ya Papa.


Naye Rais wa Mkutano wa Afya Duniani, Waziri wa Afya wa Guyana Leslie Ramsammy amelaani matamshi hayo ya Baba Mtakatifu akisema kuwa anajaribu kuleta mkanganyiko.


Wakati huo huo zaidi ya asilimia 80 ya waumini wa dini hiyo waliyohojiwa nchini Ufaransa wanataka kanisa libadilishe msimamo wake wa kupinga matumizi ya vidonge vya uzazi, pia wanataka kuwepo na nafasi ya watu kuruhusiwa kuoana tena baada ya kuachana, pamoja na ndoa za jinsia mmoja.


Aidha asilimia 43 ya watu hao walihojiwa wanataka Baba mtakatifu ajiuzulu kwa kile wanachosema kuwa ameshindwa kutimiza majukumu yake.



Mwandishi. Abubakar Liongo/AFPE

Muhariri   Saumu Mwasimba