1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

110908 Papst Grundsatzrede

Charo, Josephat12 Septemba 2008

Baba mtakatifu anatarajiwa kutoa hotuba kuhusu dini na utamaduni mjini Paris

https://p.dw.com/p/FGy6
Baba mtakatifu Benedict XVIPicha: picture-alliance/ dpa

Kiongozi wa kanisa Katoliki duniani, baba mtakatifu Benedict XVI amewasili mjini Paris nchini Ufaransa kwa ziara ya siku nne itakayompeleka pia mjini Lourdes. Ndege inayombeba kiongozi huyo wa kidini imetua katika uwanja wa ndege wa Orly mjini Paris ikitokea uwanja wa ndege wa Leornardo da Vinci mjini Roma Italia. Papa Benedict amelakiwa na mwenyeji wake rais wa Ufaransa, Nicholas Sarkozy na mkewe Carla Bruni.

Akizungumza kuhusu ziara yake nchini Ufaransa baba mtakatifu Benedict XVI amesema, ´´Nawajieni kama mjumbe wa amani na undugu katika Kristo. Nchi yenu naifahamu. Mara hii naja kwa sababu ya sherehe ya miaka 150 tangu mama Maria alipomtokea msichana mdogo katika mji wa Lourdes kama shani la ajabu. Marafiki zangu wapendwa nchini Ufaransa ombeni kwamba ziara yangu iwaletee matunda mema kwenu.´´

Baba mtakatifu Benedict XVI amewaambia waandishi wa habari walioandamana naye katika ziara yake ya Ufaransa kwamba anaipenda Ufaransa, utamaduni wake wa kuvutia na sanaa.

Baadaye kiongozi huyo wa waumini bilioni moja wa dini ya katoliki atakwenda katika ikulu ya Elysee kufanya mazungumzo na rais Sarkozy aliyezusha utata mwaka jana alipotaka kuwepo maadili ya kilimwengu yatakayoipa nafasi dini katika maisha ya kuutumikia umma. Baba mtakatifu Benedict XVI amewaambia waandishi wa habari walioandamana naye katika ziara yake ya Ufaransa kwamba anaipenda Ufaransa, utamaduni wake wa kuvutia na sanaa.

Ratiba ya ziara

Ziara ya siku nne ya kiongozi huyo nchini Ufaransa itajumulisha hotuba muhimu kuhusu jukumu la dini katika jamii atakayoitoa baadaye leo. Hapo kesho Jumamosi papa Benedict XVI ataongoza misa ya hadhara itakayofanywa katikati mwa mji wa Paris na baadaye atakwenda Lourdes kusini magharibi mwa Ufaransa maadhimisho ya miaka 150 tangu bikira Maria alipomtokea msichana katika mfano wa shani ya ajabu.

Papa Benedikt XVI anazuru Ufaransa kwa mara ya kwanza kama kiongozi wa kanisa Katoliki na ziara yake hiyo imetokana na azma yake kutaka kulitembelea eneo takatifu la mjini Lourdes kusini mwa Ufaransa ambako mama Maria alimtokea msichana mdogo miaka 150 iliyopita.

Mchanganyiko ya dini

Huku dini ya Katoliki ikiwa ndiyo dini kubwa ya kwanza nchini Ufaransa, taifa hilo pia ni nyumbani kwa idadi kubwa ya waislamu na jamii za wayahudi na imeshikilia na kulinda sheria msingi ya mwaka wa 1905 inayotaka kanisa liwe mbali na serikali. Rais Sarkozy aliwasilisha pendekezo kwa makao makuu ya kanisa Katoliki wakati wa ziara yake huko Vatican mwezi Disemba mwaka jana akisema dini haitakiwi kuonekana kama kitisho bali kama raslimali.

Ziara ya baba mtakatifu Benedict XVI nchini Ufaransa ni ya kumi katika nchi za kigeni tangu alipochaguliwa mnamo mwaka wa 2005 baada ya kifo cha mtangulizi wake John Paul II.