1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baba mtakatifu Benedikti wa 16 akiri Vatican ilifanya makosa.

Jane Nyingi/ AFPE..Picha AFP12 Machi 2009

Baba mtakatifu na kisa cha kurejeshwa kundini maskofu wanne waliokuwa wametengwa na kanisa hilo.

https://p.dw.com/p/HAsI
Baba mtakatifu Benedikti wa 16Picha: dpa

Baba mtakatifu Benedikti wa 16 amekiri kuwa makao makuu ya kanisa katoliki, Vatikani, yalikosea katika juhudi zake za kuwarejesha kundini maskofu wanne waliokuwa wametengwa na kanisa hilo.Hata hivyo, amesema amechukizwa na matamshi yaliyotolewa dhidi yake hadharani kutokana na hatua hiyo.


Matamshi hayo yalikuwa katika barua iliyokuwa na ujumbe mzito wa baba matakatifu Benedikti wa 16 kwa maaskofu wote wa kanisa katoliki kote duniani. Barua hiyo iliyoandikwa tarehe 10 mwezi huu na papa, imetolewa hii leo kwa umma na Vatikani.


Katika barua hiyo iliyotafsiriwa kwa lugha sita, baba mtakatifu ametetea uamuzi wake wa mwezi Januari mwaka huu wa kuwarejesha kundini maaskofu hao wanne baada ya kutengwa mwaka wa 1998.


Amesema ni jambo la kusikitisha kuwa uamuzi wake uliotokana na imani yake, huenda ungesababisha ukosefu wa maridhiano kati ya Wakristo na Wayahudi, kufuatia msimamo wa askofu Muengereza, Richard Williamson, aliyekana kuwa mauaji makubwa ya halaliki dhidi ya Wayahudi yalitokea.


Askofu Williamson katika mahojiano na kituo kimoja cha televisheni, baada ya kurejeshwa kundini, alikanusha kutokea kwa mauaji hayo ya halaiki, na kusema anaamini Wanazi hawakutumia gesi kuwaua wayahudi.


Mzozo uliibuka, huku wayahudi wengi na baadhi ya waumini wa kanisa Katoliki na maafisa wa serikali, akiwemo Kansela wa Ujerumani, Angela Merkel, wakitaka ufafanuzi zaidi kuhusu hatua hiyo ya baba mtakatifu.


Makao makuu ya kanisa katoliki, Vatikani, hata hivyo, yalisema hayakuwa yanajua kuhusu msimamo wa askofu Williamson, lakini wakosoaji wanasema kuwa maoni ya askofu huyo kutilia shaka mauji ya halaiki dhidi ya Wayahudi yalikuwa katika mtandao wa internet kwa muda mrefu.


Katika barua iliyotolewa leo na Vatikani, baba matakatifu Benedikti wa 16 amekiri kuyaona maoni hayo katika mtandao wa internet, na kusema katika siku za baadaye watakuwa makini na vyanzo vya taarifa, ukiwemo mtandao wa internet.


Pia baba mtakatifu amesema amechukizwa na uhasama aliotokea kutoka kwa baadhi ya waumini wa kanisa katoloki ambao walimshambulia hadharani kufuatia suala hilo.


Hii leo baraza la kitaifa la wayahudi lililo na makao yake nchini Marekani, na ambalo lilikuwa katika mstari wa mbele kuikosoa Vatikani kwa kumrejesha askofu Williamson kundini, limempongeza baba mtakatifu.


Mwezi uliopita baraza hilo na mashirika mengine yanayowawakilisha Wayahudi yalikaribisha tangazo la Vatikani kwamba askofu Williamson alikiri kulitokea mauji hayo makubwa ya halaiki dhidi ya Wahahudi.


Tangu wakati huo uhusiano umeimarika na hasa kutokana na tangazo kuwa papa atazuru Israel mwezi Mei.