1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Baba mtakatifu Ikulu Marekani

17 Aprili 2008

Baba mtakatifu Benedikt wa XVI alipokewa jana rasmi Ikulu mjini Washington na akatoa risala yake.

https://p.dw.com/p/DjZp
Papa Benedikt na mwenyeji wake rais BushPicha: AP

Baba mtakatifu Benedikt wa XVI ameitaka Marekani kuweka uadilifu kama msingi wa siasa zake."demokrasia bila ya uadilifu yaweza ikapoteza roho yake."-alisema jana baba mtakatifu mjini Washington,anakoendelea leo na ziara yake.

"Happy Birthday" wamarekani walimtakia heri baba mtakatifu jana akitimu umri wa miaka 81 huko Ikulu.

Zaidi ya wageni 10.000 walikusanyika uwanjani katika uwa wa Ikulu (white House) kuhudhuria sherehe kubwa katika historia ya Jumba hilo.Na rais George Bush alionesha kuridhika mno.

"Kwa desturi,mtu husherehekea siku yake ya kuzaliwa na marafiki zake wa chanda na pete.Ndio maana taifa letu zima linahisi limepata heshima kwa uamuzi wako mwaka huu siku hii maalumu kuisherehekea pamoja nasi.

Tunakutakia afya njema na furaha hii leo na kwa miaka mingi ijayo."

Alisema rais George Bush kwa mwenyeji wake huko Ikulu.

Papa Benedikt,akionesha amestarehe kabisa na akionesha bashasha katika mapokezi aliopewa kwa heshima yake huko Ikulu.

Katika hotuba yake huko alipongeza uongozi wa Marekani inaotoa ulimwenguni.Akasifu imani ya kidini ya wamarekani.

"Nina hakika wamarekani katika imani yao ya dini, ni chemchem ya thamani kubwa ya ujuzi na maarifa inayowavutia kuongoza mazungumzo ya kuwajibika na kuheshimika ili kujenga jamii huru na ya ubinadamu."

Alisema baba mtakatifu.

Kile hasa rais Bush na baba mtakatifu benedikt walikizungumza faraghani,hakuna anaejua.Mazungumzo ya kukosoana ya kisiasa, hakuna alietazamia kufanyika baina yao.Ingawa baba mtakatifu alipinga vikali vita vya Irak, hivi sasa anaangalia mbele na hasa anapendelea kuona amani ikipatikana haraka nchini Irak.

Rais Bush anaheshimu mchango wa baba mtakatifu na kuwa mshirika wake katika vita vya kupambana na ugaidi ulimwenguni:

"Katika dunia hii ambamo baadhi ya watu watumia jina la Mungu kuhalalisha ugaidi,tunahitaji risala yako kuwa Mungu ni mwenye rehema.Na ili kujipatia rehema zake , njia ya uhakika kabisa ni wanadamu kujizuwia kuwa mateka wa mafunzo ya siasa kali na ugaidi."

Alisema rais Bush.

Hata hivyo kiongozi wa kanisa katoliki ulimwenguni Benedikt wa 16 ameitumia pia hafla hiyo kubwa katika bustani ya ikulu ya Marekani kuitanabahisha Marekani umuhimu wa kutanguliza mbele zaidi diplomasia.Matumaini yamekewa hotuba yake atakayoitoa kesho mbele ya umoja wa mataifa mjini New-York.