1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Badawi ashinda tuzo ya 'Freedom of Speech Award' ya DW

25 Februari 2015

Mwanaharakati wa Saudi Arabia aliyekuwa msitari wa mbele kutetea uhuru wa kujieleza Raif Badawi anapewa tuzo ya Uhuru wa Kujuieleza ya Deutsche Welle - Freedom of Speech Award.

https://p.dw.com/p/1EgyV
Raif Badawi Website-Gründer aus Saudi Arabien
Raif Badawi, mwanaharakati wa Saudi ArabiaPicha: privat

Mwanablogu huyo wa Saudi Arabia anapokea tuzo hiyo ya shirika la utangazaji la Deutsche Welle inayotolewa kwa mara ya kwanza kabisa. Badawi, ambaye amehukumiwa kifungo cha miaka kumi gerezani na viboko 1000 kwa harakati zake kupitia blogu yake, anaendelea kuzuiliwa gerezani na serikali ya Saudi Arabia.

Akielezea kwa nini Badawi anakuwa mtu wa kwanza kutunukiwa tuzo ya Freedom of Speech Award ya DW, Mkurugenzi wa Deutsche Welle Peter Limbourg amesema Badawi ni mtu shujaa asiyeogopa kupigania haki za binadamu na uhuru wa kujieleza. "Kwa mtizamo wetu Badawi ni mtu mwenye ujasiri na tunataka kusadia kutumia tuzo hii, ili watu wengine waweza kuchangia zaidi kuhusu uhuru wa kujieleza ulimwenguni. Na pia tuna matumaini tunaweza kuibadili japo kidogo hali inayomkabili Raif Badawi kwa sasa."

Limbourg aidha amesema ana matumaini tuzo hiyo itaongeza shinikizo kwa viongozi wahusika wa Saudi Arabia ili hatimaye wamuachie huru mwanaharakati huyo kutoka gerezani.

Peter Limbourg
Mkurugenzi wa Deutsche Welle, Peter LimbourgPicha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Mke wa Badawi anayeishi nchini Canada, Ensaf Haidar, amesema amefurahishwa sana na uamuzi wa DW kumtunza mumewe na tuzo hiyo. Akizungumza na DW kwa njia ya simu Haidar amesema tuzo ya "Freedom of Speech Award" inatoa ujumbe wa wazi kabisa kwa serikali ya Saudi Arabia.

"Kwangu mimi ujumbe ni kwamba; Ni aibu kwa serikali ya Saudi Arabia kuendelea kumzuia. Kufikia leo Badawi amekuwa kizuizini kwa miaka miwili na miezi minane. Ni aibu kwamba watu nje wanamuenzi lakini ndani ya Saudi Arabia amedhalilishwa, ametandikwa viboko na amehukumiwa kifungo cha miaka kumi jela."

Miaka 10 jela, viboko 1000

Deutsche Welle inaitoa tuzo hiyo kama sehemu ya mashindano ya kimataifa ya kutafuta tuzo bora ya blogu "The Bobs - Best of Online Activism". Katika mashindano hayo yanayofanyika kwa mara ya 11 mwaka huu, wanaharakati mahiri wa matandaoni na miradi ya mtandaoni watatuzwa.

Mshindi wa tuzo ya DW ya uhuru wa kujieleza "Freedom of Speech Award" Raif Badawi na mshindi wa mashindano ya "The Bobs" watatunzwa tarehe 23 mwezi Juni mwaka huu wakati wa Kongamano la Kimataifa la Vyombo vya Habari - Global Media Forum - linaloandaliwa na Deutsche Welle kila mwaka hapa mjini Bonn.

Ensaf Haidar Frau Blogger Raif Badawi
Mke wa Badawi, Ensaf HaidarPicha: picture-alliance/dpa/C. Burston

Mke wa Badawi, Ensaf Haidar, anaishi Quebec na watoto wao watatu na amekuwa akiihimiza serikali iingilie kati kwa niaba ya mumewe na isaidie juhudi za kuachiwa kwake kutoka jela ya Saudi Arabia.

Badawi, mwanablogu mwenye umri wa miaka 31 alihukumiwa na mahakama ya Saudi Arabia kifungo cha miaka kumi jala, viboko 1000 na kutozwa faini ya takriban euro 200,000 mnamo mwezi Mei mwaka uliopita. Januari 9 mwaka huu alitandikwa viboko 50 hadharani na alitakiwa kuchapwa viboko 50 kila siku ya Ijumaa, lakini tangu wakati huo adhabu hiyo imesitishwa kutokana na sababu za kiafya.

Ujasiri kwa ajili ya uhuru wa kujieleza

Kwa miaka kadhaa Badawi amekuwa akipigania uhuru wa kujieleza nchini Saudi Arabia. Katika tovuti yake "Waliberali huru wa Saudia" Badawi amekuwa akikosoa ukosefu wa haki za kisiasa na kijamii nchini humo. Amechapisha makala za stihizai kuhusu polisi wa kidini na kukitaja chuo kikuu kimoja kuwa maficho kwa magaidi. Aliwahi kuandika makala kuhusu siku ya wapendao ya Valentine, ambapo sherehe zote za siku hiyo zimepigwa marufuku Saudi Arabia.

Mnamo mwaka 2008 Badawi alitiwa mbaroni kwa mara kwanza kwa madai ya kuanzisha tovuti katika mtandao wa mawasiliano ya intaneti inayodhihaki Uislamu. Aliihama Saudi Arabia kwa miezi kadhaa lakini baadaye akarejea baada ya mashitaka dhiki yake kuwasilishwa tena. Mnamo mwaka 2009 serikali ya Saudi Arabia ilimpiga marufuku asisafiri nje ya nchi. Alitiwa mbaroni mnamo Juni 17 mwaka 2012 na kufikishwa mahakamani mwezi Desemba mwaka huo. Mashtaka yaliyomkabili ni kuwakejeli viongozi katika tovuti yake.

Mwandishi: Muno, Martin/Josephat Charo

Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman