1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Bado hakuna ufumbuzi vifo vya Loveparade

Wolfgang Dick24 Julai 2015

Imetimia miaka mitano tangu watu 21 walipopoteza maisha yao kwenye tamasha la muziki wa aina ya techno linalofahamika kama Loveparade na lililofanyika mjini Duisburg nchini Ujerumani.

https://p.dw.com/p/1G41M
Duisburg Loveparade
Picha: DW/Wolfgang Dick

Kwanini? Hilo ndilo swali ambalo kila siku linavuruga mawazo ya Jörn Teich. Kwa nini palikuwa na kibali cha kufanya tamasha hili kwenye uwanja ambao usingetoshea idadi kubwa hivyo ya watu? Jörn Teich mwenye miaka 41 ni muuzaji wa maua. Anahofia kwamba hatakaa apate majibu ya maswali yake. Kila wakati Jörn anakumbuka siku hiyo ilivyokuwa, jinsi alivyokazana kutoka nje ya uwanja wa tamasha. Amepata matatizo ya kisaikolojia, hawezi tena kufanya kazi. "Maisha yangu yamebadilika kwa asilimia 100. Mimi si yule niliyekuwa zamani," anasema Jörn. "Zamani nilikuwa natoka na kustarehe. Sasa hivi sichangamani na watu, niko kivyangu. Nimebakiwa na marafiki wachache sana. Naishi mwenyewe na binti yangu na nimekubaliana na hali halisi."

Mara kwa mara Jörn anakwenda kwenye ngazi fulani ya kwenye uwanja wa tamasha ilipofanyika Loveparade. Ni ngazi ambayo kwake ilikuwa ukombozi, yeye aliweza kupanda na kutoka, wengine walifia hapo kwa kukanyagwa na wengine.

Maisha yabadilika

Katika ngazi hiyo amekaa mtu anayejitambulisha kwa jina la Georg. Yeye alikuwa mtaalamu wa kutoa huduma ya kwanza, alihudhuria tamasha, si kikazi bali kwa ajili ya kuburudika na muziki. Balaa lilipoanza kutokea, Georg aliwasaidia majeruhi. Mama mmoja alifia mikononi mwake, juhudi zote za kumwokoa ziligonga mwamba. Hakuruhusiwa kuendelea na kazi yake ya kutoa huduma ya kwanza. Mwajiri wake alimwambia ni kwasababu ya athari za kisaikolojia alizopata. "Ilikuwa ngumu sana kwangu, nilikuwa na uchungu. Katika miaka mitatu ya kwanza nilikaribia kujiua."

Ngazi hii iliokoa baadhi huku wengine wakifia hapa
Ngazi hii iliokoa baadhi huku wengine wakifia hapaPicha: DW/Wolfgang Dick

Jörn Teich anasema yeye sasa amekuwa mwangalifu zaidi: "Nikifika kwenye sherehe yoyote ile, cha kwanza ninachofanya ni kuangalia mlango wa dharura ulipo. Nafikiria namna nitakavyoweza kutoka kwa haraka. Hicho ndicho tunachowaza sisi tuliokuwepo siku hiyo"

Miaka mitano baada ya maafa ya tamasha la Loveparade, bado hakuna aliyehukumiwa kwa makosa yaliyofanyika. Wahusika wanatupiana lawama. Jörn, Georg na wenzake wanasema wameshakata tamaa na hawaamini kama ipo siku ambayo watashuhudia mtu akipelekwa gerezani kwa damu ya watu 21 iliyomwagika miaka mitano iliyopita.

Mwandishi: Wolfgang Dick

Tafsiri: Elizabeth Shoo

Mhariri: Daniel Gakuba